Somo 1: Kumb 26:16-19
Zab: 119:1-2, 4-5, 7-8
Injili: Mt 5:43-48
“Umemwungama Bwana leo, kuwa
ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri
zake na maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake,” Kumb 26:17
“Lakini mimi nawaambia: Wapendeni
adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye
mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye
haki na wasio haki,” Mt 5:44-45
“Basi
ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48
TAFAKARI: “Kuishi ahadi zetu za ubatizo: Kuwapenda
Maadui zetu na kuwa wapatanishi.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo
tuyatafakari makuu ya Mungu kwa “kuishi ahadi zetu za ubatizo; kuwapenda maadui
zetu na kuwa wapatanishi.” Somo letu la wana wa Israeli wanamuungama Mungu kwa
kuzishika amri zake. “Umemwungama Bwana leo, kuwa ndiye Mungu wako, na kuwa
yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake na maagizo yake, na
hukumu zake, na kusikiza sauti yake,” Kumb 26:17. Nasi leo kama wafuasi wake
Kristo somo hili latukumbusha ahadi za ubatizo wetu. Ubatizo wetu ni kumwungama
Kristo kwa fumbo la mateso, kifo na ufufuko wake. Fumbo hili linatufanya
kuzaliwa upya kwa Roho Mtakatifu. Kuzaliwa huku ni kule Yesu anapomtaka
Nikodemo azaliwe upya. “Yesu akamwambia, Amin, Amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa
mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu,” Yoh 3:3.
Kuishi ahadi zetu za ubatizo ni
kutembea katika njia za Bwana wetu Yesu Kristo. Tu wakristo kwa sababu tu
wafuasi wa Kristo. Na kama tu wafuasi wa Kristo, yatupasa kutembea katika njia
zake. Tomaso alitaka kujua njia impasayo kuifuata kama mfuasi wa Kristo.
“Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia? Yesu
akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa
njia ya mimi,” Yoh 14:5-6.
Mpendwa katika Kristo, njia yetu
wabatizwa na wafuasi wa Kristo ni Yesu mwenyewe. Na njia aliyochagua ni njia ya
Msalaba. Hatuwezi kuukwepa Msalaba kama tu wafuasi wa Kristo. Msalaba ni
utukufu wetu na ushindi wetu. Ukweli wake ni yale anayotufundisha, nayo ni
habari njema ya Wokovu. Habari hii ya wokovu ni uhai na umilele ambao yeye
mwenyewe anasema, “ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema,
Tazama, upo, huku, au, kule kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu,”
Lk 17:20b-21. Mfano mzuri ni pale ufanyapo mtihani. Mwalimu anapokupa mtihani,
100% unayo wewe mwenyewe. Yakupasa kumwonyesha mwalimu asilimia hiyo 100. Maana
yake kufaulu kwa mtihani kupo kwako na ni juu yako.
Uzima katika Kristo tunaupata
tunaposhiriki masakramenti yake, na hasa sakramenti ya Ekaristi Takatifu tukiwa
na mioyo safi. “Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye
kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe,” Yoh 6:35.
Tunaishi ahadi zetu za ubatizo
kwa kuzishika amri zake na kufuata maagizo yake. Ni kuwa na hofu ya Mungu ndani
mwetu. Na amri iliyo kuu ni ya upendo. “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile
nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo,” Yoh 13:34. Amri hii ya
upendo na nyinginezo zatupasa kuzishika si kinadharia tu bali kwa matendo yetu
na yenye kumpendeza Mungu. Huku ni kudhihirisha tunampenda Yesu Kristo na yule
aliye mpeleka. “Yeye aliye na mri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye;
naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha
kwake,” Yoh 14:21. Tendo hili la kuzishika amri za Mungu ni kukaa katika pendo
la Mungu. Huku ni kumuishi Kristo aliyekaa katika pendo la Mungu kwa kushika
amri zake. “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi
nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10.
Wapendwa wana wa Taifa la Mungu,
somo la Injili latualika pia kutafakari juu ya upendo wetu na maadui zetu,
ambao tunda lake ni upatanishi. Si jambo rahisi kibinadamu kumpenda adui yako,
hasa pale unapoyakumbuka mabaya aliyokutendea. Ila tusipo enda zaidi ya
kuwapenda wale tu ambao wanatupenda, ukristo na ufuasi wetu bado haujakomaa, na
imani yetu bado changa. “Lakini mimi nawaambia: Wapendeni adui zenu, waombeeni
wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye
huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki,”
Mt 5:44-45. Huku ndiko kwenda zaidi ya yale yaonekanayo kwa mtazamo wa
kibinadamu ambayo kwayo hutupatia haki ya leo na sasa, na kukosa neema ya
huruma ya Mungu. Hivyo kwa kuyapata hayo tu huyafanya Maisha yetu ya kiroho
kuwa na ulakini.
Tunakuwa wana wa Mungu tu kwa
kuwapenda maadui zetu na kuwaombea. Kwa dhambi zetu tulikuwa maadui na Mungu.
Ila kwa kupitia mwanaye Yesu Kristo kwa mateso, kifo na ufufuko wake
tumepatanishwa na Mungu. Kristo ni kielelezo cha UPANANISHO HAI NA WA KWELI.
Nasi kwa kumfuata Kristo tunafanya kazi hiyo ya upatanisho kwa kuwaombea watesi
wetu kwa Mungu awabadili mienendo yao mibaya. “Maana
mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao
hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la
ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?” Mt 5:46-47. Wapendwa
inasikitisha sana kuona miongoni mwetu kadiri ya wito na utume wetu, tumekuwa
wakristo wazuri sana wa jumapili, twakiri kuwa askari imara wa Kristo, na
ifikapo jumatatu tunatoroka kambini na kufanya kinyume kabisa na utambulisho
wetu kwa kutowapenda na kutokuwa tayari kuwasamehe watesi wetu. Kwa kweli haya
ni zaidi ya maigizo.
Ndugu yangu, hatuwaombei mabaya
maadui zetu. Tukumbuke nao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, Mwa 1:27.
Mungu tu ndiye anayeweza kuwabadili kwa sababu ndani yao ipo chapa yake-sura na
mfano wake. Kwa upendo alio nao Mungu wetu kwa wema na waovu, hata kaa kimya
aache chapa yake ipotee bure. Kwa msaada wa sala zetu, Mungu yupo tayari
kuwabadili kwa tendo hili la sala na majuto. Tunakuwa pia wana wa Mungu kwa
kuwa wapatanishi. “Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu,” Mt 5:9.
Upatanisho ni tendo la ibada na
ukombozi. Misa Takatifu kama ibada ya neno na Ekaristi Takatifu ni tendo la
upatanisho. Tunapatanishwa nafsi zetu, wenzetu (wema na waovu), na Mungu. Huku
ndiko kumwilishwa kwa neno (Mwana wa Mungu), kuwa mwili. Ni tendo la upendo
mkubwa wa Mungu Baba kwetu wanadamu. Ni ufupisho wa historia yote ya wokovu
wetu.
Hivyo basi, kama mfuasi mwaminifu
na mwenye hofu ya Mungu, wewe na mimi yatupasa kufurahi na kushangilia pale
tunaposhutumiwa kwa ajili ya haki, tunapoudhiwa na kunenewa kila neno baya kwa
uongo kwa ajili ya Kristo. Hii ndiyo maana halisi na mapaswa ya kuwa mkristo wa
kweli na mfuasi wa Kristo. Yesu anasema, “heri ninyi watakapowashutumu na
kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na
kushangilia, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana ndivyo
walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12.
Ndugu yangu, hii ndiyo changamoto
ya kweli ya ishi yetu kama wakristo. Kuishi huku kunakuhitaji kuziishi ahadi
zako za ubatizo kuwapenda maadui zako, na kuwa wakili wa Kristo, yaani
mpatanishi. Ahadi hizi za ubatizo ndicho alichokifanya Yesu Kristo katika
safari nzima ya wokovu wetu. Je, upo tayari kuvivaa viatu vya Yesu?
Tumsifu Yesu Kristu!
“Basi ninyi
mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48
Tusali:- Ee Yesu, uliye Njia, Ukweli, na Uzima, kamwe
usituache katika fumbo hili la wokovu wetu, yaani kuziishi ahadi zetu za
ubatizo na kuwa mawakili wako, yaani Wapatanishi. Amina
0 blogger-facebook:
Post a Comment