SOMO 1
Yoe. 2:12-18
Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. N’nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia Baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa Bwana, Mungu wenu?
Pigeni tarumbeta katika Sayuni, takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, na hao wanyonyao maziwa; bwana arusi na toke chumbani mwake, na bibi arusi katika hema yake.
Hao makuhani, wahudumu wa Bwana, na walie kati ya patakatifu na madhabahu, na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee Bwana, wala usiutoe urithi wako upate aibu, hata mataifa watawale juu yao; kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?
Hapo ndipo Bwana alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 51:1-4, 10-12, 15 (K) 1
(K) Uturehemu, Ee Bwana, kwa kuwa tumetenda dhambi.
Ee Mungu, nirehemu,
Sawasawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu. (K)
Maana nimejua mimi makosa yangu,
Na dhambi yangu I mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako,
Na kufanya maovu mbele za macho yako. (K)
Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)
Unirudishie furaha ya wokovu wako;
Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
Na kinywa change kitazinena sifa zako. (K)
SOMO 2
2 Kor. 5:20 – 6:2
Ndugu zangu, basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu. Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.
Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure. Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nilikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Zab. 95:8
Msifanye migumu mioyo yenu; msikie sauti ya Bwana.
INJILI
Mt. 6:1-6, 16-18
Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampatai thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amini, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amini, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa nafunga, Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
0 blogger-facebook:
Post a Comment