Masomo:
Somo: Yer
17:5-10
Zab: 1:1
1-2, 3-4, 6
Injili:
Lk 16:19-31
Nukuu:
“Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu
yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake
amemwacha Bwana,” Yer 17:5
“Amebarikiwa mtu yule
anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake,” Yer 17:7
“Mimi, Bwana, nauchunguza moyo,
navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya
matendo yake,” Yer 17:10
“Wanao Musa na manabii; na
wawasikilize wao. Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu
akifufuka katika wafu.” Lk 16:29,31
TAFAKARI: “Kuishi bila hofu ya Mungu; kutotimiza wajibu
na kutokujali.”
Wapendwa wana wa Mungu, niwaalike
tena kwa siku ya leo, tutafakari pamoja, “kuishi bila hofu ya Mungu; kutotimiza
wajibu na kutokujali.” Somo letu la kwanza laelezea hathari za kuishi bila kuwa
na hofu ya Mungu. Injili yatuelezea hathari za kutotimiza wajibu na kutokujali.
Ndugu, tuanze safari yetu kwa
kutafakari kwa undani hathari za kutokuwa na hofu ya Mungu. Je, hofu ya Mungu
ni nini? Mpendwa, hofu ya Mungu ni kuishi kwa kumtegemea Mungu kwa kila jambo.
“Ee Bwana, Mungu wangu, umefanya kwa wingi Miujiza yako na mawazo yako kwetu;
Hakuna awezaye kufananishwa nawe; Kama ningependa kuyatangaza na kuyahubiri, Ni
mengi sana hayahesabiki,” Zab 40:5.
Ni kujenga mahusiano ya karibu na Mungu kiasi
kwamba huwezi fanya lolote bila kumshirikisha Mungu. Ndugu yangu, “mkabidhi
Bwana kazi zako, na mawazo yako yatathibitika,” Mit 16:3. Mtu anayeishi katika
hofu ya Mungu, upanga na Mungu, uwaza na Mungu, ushauriana na Mungu, na
uyakabidhi maisha yake mwenyewe na mipango yake yote kwa Mungu. Huku ni kuishi
katika baraka kama asemavyo Nabii Yeremia, “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea
Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake,” Yer 17:7
Kuishi bila hofu ya Mungu ni kujiamini
kusiko fikirika. Ni kuamini na kutegemea vitu na mali, watu na vyeo vyao. Huku
ndiko tunapochuma laana kama anavyosema Nabii Yeremia, “Bwana asema hivi,
Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake
Na moyoni mwake amemwacha Bwana,” Yer 17:5. Mtu wa mwono huu kimaisha hawezi
pata baraka. Mungu hana nafasi katika maisha yake. Na hapendi kumpa Mungu
nafasi.
Mtu asiye na hofu ya Mungu huishi
maisha linganishi mara zote. Mtu wa mtindo huu kimaisha hawezi jipokea alivyo;
na hivyo ni vigumu kufanya mabadiliko kimwili na kiroho. Mtu wa mtindo huu
awezi kuwa na furaha ya kweli. Muda wote huishi maisha ya ushindani na kusahau
jambo lililo la msingi katika maisha yake, yaani, Mungu hupendezwa nawe kama
ulivyo. Uwepo wako ulimwenguni hapa si bahati mbaya. Maisha bila Mungu ni sawa
na samaki bila maji. Hivyo ni wajibu wangu na wako kuitafuta sura ya Mungu kila
siku. “Bali mimi nikutazame uso wako katika
haki, Niamkapo nishibishwe kwa sura yako,” Zab 17:15. Kwa nini basi itakupasa
kuitafuta sura ya Mungu kila siku? Mtume Paulo anasema, “Na kama
tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye
aliye wa mbinguni,” 1Kor 15:49. Na sura ya yule wa mbinguni ni UTAKATIFU. Ndugu
yangu, bila Utakatifu hakuna mbingu. Kuitafuta Sura ya Mungu ni kuutafuta
Utakatifu na kuuishi huo utakatifu tungali hai kila mmoja wetu kadiri ya
mazingira na wito wake.
Furaha ya kweli haipatikani kwa
mali tulizonazo; bali twaipata kwa kujipokea kama tulivyo na kujua upendo wa
Mungu ndani yetu. Yeye Mungu yupo tayari kutupokea na kutufanya tena wana wake
tunapokiri kupotoka kwetu na kumuasi. Mungu huturudishia hadhi yetu na
mastahili yetu kama watoto wake. Hii ndiyo furaha ya kweli ndani mwetu. Hakuna
mamlaka yoyote au binadamu yeyote awezaye kuyafanya haya. Ni Mungu tu.
Somo la Injili la tupa kisa cha
tajiri na maskini Lazaro. Tajiri anajulikana kwa mwono wake, na maisha yake ya
anasa. Lazaro anajulikana kwa jina lake, umaskini wake na unyonge wake. Kosa
kubwa la tajiri huyu ni dhambi ya kutotimiza wajibu. Ndugu yangu, kabla ya
kuendelea na tafakari hii nikuombe usali kwanza sala ya “NAKUUNGAMIA.” Dhambi
ya kutotimiza wajibu, ni kosa la nne tunalokiri katika sala hii ya “nakuungamia
Mungu mwenyezi.” Lazaro tunaambiwa mara zote alikaa kwenye mlango, ikimaanisha
kwamba kwa vyovyote vile tajiri huyu alimwona Lazaro katika dhiki yake na
ilimpasa tajiri huyu afanye kitu. Kutotimiza wajibu, ni kosa la kutokufanya
kitu wakati ulitakiwa kufanya kitu. Tajiri huyu anahukumiwa kwa kutokujali na kutokufanya
chochote.
Ndugu yangu, tazama mazingira
unayoishi, Je, akina Lazaro hawapo? Wale Mungu aliotubariki kuwa na Magari
binafsi, Je, unapofunguliwa geti hujamwona Lazaro pembeni akisubiri wema na
upendo wako? Wale ambao hula vizuri kila siku na asubuhi kumwaga viporo vya
wali na vipande ya samaki, Je, huwaoni akina Lazaro wakilichungulia shimo taka
kwa masikitiko? Wewe ambaye kila siku huingia ofisini na mkoba wako, Je,
humuoni Lazaro kwenye ‘benchi’ akisubiri wema na huruma yako?
Ukweli ni kwamba, wote tutakufa
na kujongea kiti cha ukumu. Tunapoishi hapa duniani, tunaaswa na mzaburi,
“usiogope mtu atakapopata utajiri, na fahari ya nyumba yake itakapozidi. Maana
atakapokufa hatachukua cho chote; utukufu wake hautashuka ukimfuata,” Zab
49:16-17. Mambo yote yatupayo ufahari ipo siku tutayaacha. Je mbele ya Mungu
tutafika na jambo gani kama utambulisho wetu?
Ndugu yangu, ijumaa ijayo,
nakualika wakati wa njia ya msalaba utafakari kituo cha tisa; Yesu anaanguka
mara ya tatu. Njia ya msalaba kwa kutumia misale ya waamini, kuna maneno haya
katika kituo hiki cha tisa; “Mara nyingi mno ninajibovusha kwa kupenda mno
starehe, anasa na tafrija. Ee Yesu mwema, nisaidie kuufuata mfano wa Mtakatifu
Paulo, niutese mwili wangu na kuutumikisha, ili nipate siku moja tuzo
mbinguni.” Katika kujibovusha huko, hujakutana na akina Lazaro?
Tunapojitesa na kuwajali wengine,
hakika tutapata tuzo mbinguni. Mateso aliyoyapata Tajiri, alitamani na kuomba
taarifa zile ziwafikie ndugu zake ili wasije patwa na mateso yale. Ibrahimu
anamjibu, “wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Wasipowasikia Musa na
manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu.” Lk 16:29,31. Ndugu
yangu, hapa Musa anawakilisha Sheri za Mungu na Amri zake. Manabii hapa ni wale
wahudumu wa neno la Mungu. Kwa maana nyingine tungesema, sisi kama wafuasi wa
Kristo tunajua taratibu zitupasazo kuishi, ikiwa ni pamoja na Amri za Mungu. Na
Amri kuu kupita zote ni Amri ya upendo. “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako
wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo
kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende
jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote
na manabii,” Mt 22:37-40 Pili, tumepewa wachungani, na wapo muda wote kwa
kutuhudumia hasa kiroho. Tunaonywa na kufundishwa kupitia mahubiri yao. Kwa
kuyashika haya mawili na kuyaishi, basi tuzo tutalipata. Nje ya hapo tutegemee
mateso makali.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye
Bwana ni tumaini lake,” Yer 17:7
Tusali:-Ee Yesu, tuepushe na dhambi ya
kutokujali na kutotimiza wajibu wetu. Amina
0 blogger-facebook:
Post a Comment