“yafaa nini kwa mtu kupata ulimwengu wote, akipoteza roho yake?”
Baba yake aliitwa Juan de Jassu alikuwa msomi maarufu, Daktari wa Sheria; na Mama yake aliitwa Maria de Alpilcueta. Ksaveri akiwa na umri wa miaka tisa tuu, baba yake alifariki. Mama yake alimlea katika mazingira ya sala daima. Mapadre waliokuja kuadhimisha Ibada ya Misa Parokiani kwao, walimfundisha Ksaveri Kilatini.
Mtakatifu Fransisko Ksaveri alikuwa na matamanio ya kuwa msomi maarufu kupata shahada ya udaktari wa falsafa. Akiwa na umri wa miaka kumi na tisa Ksaveri mzuri wa sura na mtanashati alijiunga na chuo cha Paris huko Ufaransa kilichokuwa maarufu Ulaya nzima. Fransisko alichukua sheria na falsafa alionesha bidii ya pekee katika masoma na alikuwa na kipaji cha kujifunza lugha, Kigriki na Kilatini zilizomsaidia katika masomo yake. Pamoja na masomo alipenda sana michezo hasa riadha na kuruka juu. Hili lilimpatia sifa katika mashindano kwani aliibuka kidedea na alifurahi sana.
Baadaye, Ksaveri alipangiwa chumba kimoja na Inyasi wa Loyola aliyekuwa mkubwa kwake kiumri na kimasomo. Alijifunza mengi kutoka kwa Inyasi hasa pale aliposisitiziwa; “Ksaveri Ksaveri, yafaa nini kwa mtu kupata ulimwengu wote, akipoteza roho yake?” Hapa Ksaveri aliamua atafanya kazi daima kueneza ufalme wa Mungu, kumtumikia Mungu na watu wake. Na kweli alitimiza ahadi hii kwa moyo wake wote na nguvu zake zote katika uhai wake.
Mnamo Agosti 15, 1534 Fransisko Ksaveri, Inyasi wa Loyola na wenzake watatu, waliweka nadhiri za kitawa katika kanisa la Montmatre, Paris na Shirika la Yesu (Wajesuit) likazaliwa rasmi, chini ya mkubwa wao Inyasi wa Loyola.
Tarehe 24 Juni 1537, Ksaveri alipadrishwa huko Venies Italia, alifanya mafungo ya siku arobaini kwa mazoezi ya kiroho kabla ya kuadhimisha Ibada yake ya kwanza ya Misa Takatifu. Hakika alimuiga Kristo aliyekwenda jangwani kufunga na kuomba kabla ya utume (Mk. 1:13).
Ksaveri mmisionari imara alifanya utume kwa bidii akifundisha Katekismu, kutembelea wagonjwa na wafungwa ili kuwafariji. Alitamani kwenda Mji Mtakaatifu na kuwaongoa Waislamu. Huko Bologna nchini Italia alifahamika kwa mahubiri yake mashuhuri. Ksaveri alienda pia Roma na kuwa katibu wa Inyasi. Mmisionari yupo tayari kwa lolote, ombi kutoka kwa Mfalme wa Ureno kutaka Wamisionari wawili waende India lilimfikia Inyasi; kwa moyo wa utayari mkubwa na upendo wa hali ya juu Fransisko Ksaveri alikubali kwenda India kueneza Habari Njema ya Ukombozi. Mwaka 1541 alianza safari ndefu na ngumu kuelekea India kwa merikebu, iliyochukua miezi kumi na tatu. Walipumzika Malindi-Afrika Mashariki, Msumbiji na Afrika Kusini, na tarehe 6 Mei 1542 walifika Goa-India.
Mtakatifu Fransisko Ksaveri mmisionari halisi hakupumzika katika utume wake. Akiwa Goa alifundisha Katekismu kwa watu wote, wafungwa na wagojwa; alifundisha kwa njia ya nyimbo ili waweze kukumbuka daima. Tunaambiwa alibatiza watu zaidi ya elfu hamsini. Pia hakuacha elimu nyuma alijenga Chuo cha Kikatoliki pale Goa ili kuwaelimisha wengi. Hakika kazi hii haikuwa rahisi kwani alipata upinzani kutoka kwa wafanyabiasha na wavuvi.
Kila siku aliungamisha mamia ya watu. Ksaveri alipita mitaani akipiga kengele ndogo ambapo watoto walimfuata na aliwafundisha sala, imani na amri za Mungu. Alitafsiri sala hizi kwa lugha zao na kuzisali kwa moyo. Barua yake kwa Mtakatifu Inyasi ilidhihirisha kazi yake.
“Tangu nifike hapa sijapumzika. Nimekitembelea kila kijiji, nikawaosha watoto wote wasiobatizwa bado kwa maji matakatifu. Hivyo kuna idadi kubwa sana ya watoto niliowaondolea dhambi ya asili. Watoto hawaniachii nafasi ya kusali Breviari, kula na kulala usingizi kabla ya kuwafundisha walau sala fulani. Hapo nimepata kung’amua kwamba “Ufalme wa mbinguni ni kwa ajili ya hao”. Kweli Ksaveri alikuwa ‘jembe’ la aina yake.
Mwaka 1549 alisafiri kwenda kuhubiri Indonesia, visiwa vya Moluk, Amboina Himalaya, Ceylon hadi Japan, kilometa hizi nyingi alitembea kwa miguu. Huko Japan hali ya kisiasa na hali ya hewa ilikuwa mbaya hivyo kazi yake ya Kimisionari ilikuwa ngumu sana. Sala ilikuwa ndiyo faraja yake, aliwahimiza wakristo kusali na kuchunguza dhamiri zao kwa siku mara mbili asubuhi na usiku.
Ksaveri alitamani kurudi Ulaya chuoni kuwaambia wanafunzi wote wasikilize sauti ya Mungu ili waweze kumtumikia. Mmisionari Ksaveri hakukata tamaa aliposikia watu wa China hawajapata Injili, alipanga kwenda kuhubiri huko japokuwa ilikuwa ngumu na hatari, daima Ksaveri alikuwa jasiri, neema ya Mungu ilikuwa naye. Alisafiri hadi kisiwa cha Sanchian maili sita karibu na China, ambapo aliadhimisha Ibada, kuungamisha na kusuluhisha ugomvi. Hapa Ksaveri aliugua homa kali akisubiri kibali cha kuingia China na tarehe 03 Desembe, 1552 Fransisko Ksaveri alifariki, baada ya kazi nzito ya kimisionari.
Fransisko alizikwa kwa kuwekewa chokaa ili aoze haraka waamishe masalia yake; cha ajabu baada ya miezi miwili alikutwa hajaoza yupo mbichi. Hivyo alipelekwa kuzikwa Goa kwenye Kanisa kuu la Yesu; na mkono wake ulipelekwa Roma walipojenga altare yake watu kuhiji. Alitangazwa Mtakatifu Machi 12, 1622 na Papa Gregory XV.
Mwaka 1927 Mtakatifu Fransisko Ksaveri akatangazwa kuwa msimamizi wa Wamisionari duniani, na Papa Pius X. Pia ni mlinzi wa mabaharia anajulikana kama Mtume wa India na Mashariki ya mbali. Kwa nguvu na matumaini makubwa aliungana na Mt. Paulo “Ole wangu nisipo ihubiri Injili” (1Kor. 9:16).
Sikukuu ya Mtakatifu Fransisko Ksaveri huadhimishwa Desemba 03 kila mwaka.
Amina tunaiga kutoka kwake
ReplyDeleteNdiye mt. wa jumuiya yangu
ReplyDeleteAksanti
ReplyDelete