Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 20 Machi
2017 amekutana na kuzungumza na Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye baadaye
amekutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican
aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa
Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa. Katika mazungumzo yao,
viongozi hawa wawili wamepongeza uhusiano wa dhati kati ya Vatican na Rwanda.
Kwa pamoja wameridhika na mchakato wa utulivu katika masuala ya kijamii,
kisiasa na kiuchumi nchini Rwanda.
Ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa, umesaidia
kukoleza upatanisho wa kitaifa na hivyo kuimarisha amani kwa ajili ya ustawi na
maendeleo ya taifa zima! Katika mazingumzo yao, Baba Mtakatifu Francisko
ameonesha kusikitishwa kwake na mauaji ya kimbari yaliyofanyika nchini Rwanda
dhidi ya Watutsi na kuonesha mshikamano wake wa dhati na wahanga wa mauaji haya
ambao bado wanaendelea kuteseka kutokana na athari zake.
Baba Mtakatifu akiwa ameungana na Mtakatifu Yohane
Paulo II kunako mwaka 2000 wakati wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka elfu
mbili ya Ukristo aliposali kwa ajili ya kuomba msamaha, Papa Francisko pia
amerudia sala hii kwa ajili ya wakleri, watawa na waamini walei waliojihusisha
na mauaji ya kimbari kiasi cha kusaliti utume wa Kiinjili. Kwa kutambua makosa
yaliyotendwa na watoto wa Kanisa ambayo yamelichafua Kanisa, kwa unyenyekevu
mkubwa, sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya
Mungu, anaungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda kuomba utakaso wa kumbu
kumbu ili kuendeleza matumaini na Imani iliyopyaishwa, ili kudumisha amani na
kushuhudia kwamba inawezekana kushirikiana kwa dhati, ikiwa kama utu wa
ninadamu na mafao yake msingi yanapewa kipaumbele cha kwanza. Mwishoni, Baba
Mtakatifu Francisko na Rais Paul Kagame wa Rwanda wamegusia masuala ya kisiasa
na kijamii Kikanda hasa zaidi katika maeneo ambayo yameathirika kwa vita na
majanga asilia. Wamesema kuna idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanaohitaji
msaada wa dharura kutoka kwenye Jumuiya ya Kimataifa na Mashirika ya Misaada
Kikanda.
Chanzo: Radio Vatican.
0 blogger-facebook:
Post a Comment