SOMO 1
Mwa. 37:3-4, 12-13, 17-28
Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana
ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba
yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, na hawakuweza kusema naye
kwa amani.
Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao
huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo
katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao.
Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko
Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shuri juu yake
ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja.
Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama
mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. Reubeni akasikia akamwokoa
katika mikono yao, akasema, Tusimwue. Reubeni akawaambia, Msimwage damu;
mtupeni katika birika iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika
mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake,
wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa
katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula
chakula.
Wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli
wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane,
wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini
kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli,
wala mikono yenu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake
wakakubali.
Wakapita wafanyabiashara Wamidiani; basi wakamtoa
Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa
vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 105:16-21 (K) 5
(K) Zikumbukeni ajabu zake Bwana alizozifanya.
Akaiita njaa iijilie nchi,
Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.
Alimpeleka mtu mbele yao,
Yusufu utumwani. (K)
Walimwumiza miguu yake kwa pingu,
Akatiwa katika minyororo ya chuma.
Hata wakati wa kuwadia neno lake,
Ahadi ya Bwana ilimjaribu. (K)
Mfalme alituma watu akamfungua,
Mkuu wa watu akamwachia.
Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake,
Na mwenye amri juu ya mali zake zote. (K)
SHANGILIO
Yn. 3:16
Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa
Mwanawe wa pekee; Kila mtu amwaminiye huwa na uzima wa milele.
INJILI
Mt. 21:33-43; 45-46
Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa watu,
Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba
la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake,
akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa
karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale
wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu
wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza,
wakawatenda vile vile.
Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi
mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa
wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata,
wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa
shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, Ataangamiza vibaya
wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa
matunda kwa wakati wake.
Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko,
Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; neno hili
limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia,
Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa, linguine lenye kuzaa
matunda yake.
Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano
yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata waliogopa
makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
0 blogger-facebook:
Post a Comment