728x90 AdSpace

­
Latest News
March 1, 2017

SALA YA ASUBUHI: Sali Namna Hii Kila Uamkapo Asubuhi

SALA YA ASUBUHI.

Kwajina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.

Ee Baba yetu Mungu mkuu,Umenilinda usiku huu.
Nakushukuru kwa moyo,Ee Baba, Mwana na Roho.
Nilinde tena siku hii, Niache dhambi, nikutii.
Naomba sana Baba wee,Baraka zako nipokee.
Bikira safi, Ee Maria,Nisipotee nisimamie.
Mlinzi mkuu malaika wee, Kwa Mungu wetu niombee
Nitake nitende mema tu,Na mwisho nije kwako juu. Amina.

NIA NJEMA.
Kumheshimu Mungu wangu, Namtolea roho yangu
Nifanye kazi nipumzike, Amri zake tu nishike
Wazo, neno, tendo lote, Namtolea Mungu pote
Roho, mwili chote changu,Pendo na uzima wangu
Mungu wangu nitampenda, Wala dhambi sitatenda.
Jina lako nasifia,Utakalo hutimia.
Kwa utii navumilia,Teso na matata pia.
Nipe, Bwana, neema zako,Niongeze sifa yako. Amina.

SALA YA MATOLEO.
Ee Yesu, kwa mikono ya Bikira Maria, na kwa maungano na sadaka yako kuu, ninakutolea sala, matendo, masumbuko na furaha zangu zote za leo. Ee Yesu, ufalme wako utufikie.

BABA YETU.
Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe. Ufalme wako ufike. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni. Utupe leo mkate wetu wa kila siku. Utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi, lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALAMU MARIA.
Salamu, Maria, umejaa neema; Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu. Sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.

KANUNI YA IMANI.
Nasadiki kwa Mungu Baba mwenyezi. Muumba wa Mbingu na dunia. Na kwa Yesu Kristo Mwanae wa pekee, Bwana wetu. Aliyetungwa kwa Roho Mtakatifu, akazaliwa na Bikira Maria. Akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato. Akasulibiwa, akafa, akazikwa; akashukia kuzimu. Siku ya tatu akafufuka katika wafu. Akapaa mbinguni, amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi. Toka huko atakuja tena kuwahukumu wazima na wafu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa takatifu katoliki, ushirika wa watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo. Amina.

AMRI ZA MUNGU.
1. Ndimi Bwana Mungu wako, usiabudu Miungu wengine.
2. Usilitaje bure jina la Mungu wako.
3. Shika kitakatifu siku ya Mungu.
4. Waheshimu Baba na Mama upate miaka mingi na heri duniani.
5. Usiue.
6. Usizini.
7. Usiibe.
8. Usiseme uongo.
9. Usitamani mwanamke asiye mke wako.
10. Usitamani mali ya mtu mwingine.

AMRI ZA KANISA.
1. Hudhuria misa takatifu, dominika na sikukuu zilizoamriwa.
2. Funga siku ya jumatano ya majivu; usile nyama siku ya ijumaa kuu.
3. Ungama dhambi zako walau mara moja kila mwaka.
4. Pokea Ekaristi takatifu hasa wakati wa Paska.
5. Saidia Kanisa katoliki kwa zaka.
6. Shika sheria katoliki za ndoa.

SALA YA IMANI.
Mungu wangu, nasadiki maneno yote. Linayosadiki na linayofundisha Kanisa Katoliki la Roma. Kwani ndiwe uliyetufumbulia hayo. Wala hudanganyiki, wala hudanganyi. Amina.

SALA YA MATUMAINI.
Mungu wangu, natumaini kwako, nitapewa kwa njia ya Yesu Kristo. Neema zako hapa duniani, na utukufu mbinguni. Kwani ndiwe uliye agana hayo nasi, nawe mwamini. Amina.

SALA YA MAPENDO.
Mungu wangu, nakupenda zaidi ya chochote. Kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza. Nampenda na jirani yangu, kama nafsi yangu, kwa ajili yako. Amina.

SALA YA KUTUBU.
Mungu wangu, nimetubu sana dhambi zangu. Kwani ndiwe mwema, ndiwe nwenye kupendeza. Wachukizwa na dhambi, basi sitaki kukosa tena. Nitafanya kitubio, naomba neema yako, nipate kurudi. Amina.

SALA KWA MALAIKA MLINZI.
Malaika mlinzi wangu, unilinde katika hatari zote, za roho na za mwili. Amina.

MALAIKA WA BWANA
Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria.
  Naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
    Salamu, Maria,.....
Ndimi mtumishi wa Bwana.
  Nitendewe ulivyonena.
  Salamu, Maria....
Neno la Mungu akatwaa mwili.
  Akakaa kwetu.
  Salamu, Maria....
Utuombee, Mzazi mtakatifu wa Mungu.
  Tujaliwe ahadi za Kristu.


          Tuombe
Tunakuomba, Ee Bwana, utie neema yako mioyon mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika kwamba Mwanao amejifanya mtu kwa mateso na msalaba wake tufikishwe kwenye utukufu na ufufuko. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. AMINA..

ATUKUZWE BABA (mara tatu)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Kama mwanzo na sasa na siku zote na milele. Amina.

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 blogger-facebook:

Post a Comment

Item Reviewed: SALA YA ASUBUHI: Sali Namna Hii Kila Uamkapo Asubuhi Rating: 5 Reviewed By: Unknown