Masomo:
Somo I: Mwa 12:1-4a
Zab: 33:4-5, 18-19, 20, 22
Somo II: 2Tim 1:8b-10
Injili: Mt 17:1-9
Nukuu
“Nami nitakufanya
wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka,”
Mwa 12:2
“Nami
nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote
za dunia watabarikiwa,” Mwa 12:3
“bali uvumilie mabaya pamoja nami
kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita
kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya
makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu
milele,” 2Tim 1:8-9
“na sasa
inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili
mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili,” 2Tim 1:10
“Na baada ya
siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya
mlima mrefu faraghani,” Mt 17:1
“akageuka sura
yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama
nuru,” Mt 17:2
“Alipokuwa
katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka
katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa
naye; msikieni yeye,” Mt 17:5
TAFAKARI: “Imani ya kweli ndiyo
msingi wa ufahamu wote.”
Wapendwa wana wa Mungu,
kuaminiana ni jambo la kawaida na la muhimu kwa maisha ya kawaida kabisa
tunapoishi zaidi ya mtu mmoja. Tendo hili la kuaminiana ni matokeo ya imani
tulinayo juu ya yule au wale tunaoishi nao. Mfano, ninaposafiri na kuingia duka
lolote au hoteli yoyote na kununua maji, ninayoimani maji yale ni salama. Kitu
cha kwanza kabisa ni Imani niliyonayo. Hatua ya pili ni ufahamu kama tokeo la
imani ile, yaani, ninapokuwa salama au kutokuwa salama baada ya kunywa maji
yale. Hatua hii ndiyo tunayoiita ufahamu wa jambo lile.
Abramu ni mfano thabiti wa Imani
ya kweli. Abramu ukiwa umri umeenda, yapata miaka 70, anapata ujumbe wa kutoka
mazingira aliyoyazoea na kwenda asipokujua. “Bwana
akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba
yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha,” Mwa 12:1. Embu fikiria
inavyotuwia vigumu kuondoka mazingira tunayoyajua na kwenda mazingira tusiyo
yajua inavyokuwa vigumu. Pili, Abramu anaondoka na mali zake zote kwenda katika
nchi ya ahadi asiyoijua, bali kwa kuonyeshwa kuwa ni nchi ya kanaan. “Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa
nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata
huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya
Kanaan,” Mwa 12:5. Hili ni tendo la ujasiri mkubwa sana kwa binadamu kufanya.
Abramu anaishinda hofu ya sintofahau kuhusu kesho.
Ingawa Abramu
anahaidiwa kubarikiwa na kupata ulinzi wa kutosha, jambo hili si rahisi
kuliamini kwa kirahisi. “Nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye
nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa,” Mwa 12:3. Tunakuwa
salama zaidi kwa mazingira tunayoyajua kuliko yale tusiyoyajua. Hapa ndipo
penye ugumu kwa binadamu kufanya maamuzi ya kina kuhusu maisha yake. Abramu
anashinda mtihani huu mgumu. Ni ukweli usiotia shaka kwamba kwa binadamu hakuna
mtihani mgumu kama kufanya maamuzi msingi ya maisha yake, yaani, kuacha njia
aliyoizoea na kuanza njia nyingine au kuacha maisha aliyoyazoea na kuanza
maisha mapya na mazingira mapya. Jambo la msingi hapa kuhusu Abramu ni uhusiano
wake na wakaribu na Mungu aliyemwamini na kuyaweka yote kwake. Mimi na wewe leo
kielelezo chetu Kristo aliye kila kitu kwetu. Kwake Yesu kuna Njia, Kweli, na
Uhai, Yoh 14:6.
Hivyo wapendwa katika Kristo,
lnjili ya leo inauweka sawa ukweli huu kwa mambo makuu matatu; Dira yetu ya
kufuata kama Wakristo, Utumilifu wa nyakati, na Hatma yetu iliyojengeka katika
agano la umilele. Haya yote yanafanyika katika tukio hili la kung’ara kwa Bwana
wetu Yesu Kristo kadiri ya simulizi la Injili ya leo.
Kwanza, ni dira yetu ya kufuata
kama Wakristo. Heshima na cheo chako kama Mkristo ni utakatifu wako. Hivyo
maisha yetu kama Wakristo kuelekea umilele yatafikika na kuwezekana kama ni
tokeo la utakatifu wetu kwa kuyaona maisha kama ni jukumu la muda fupi hapa
duniani na kama pia sehemu pekee ya maandalizi. Udhihirisho wa utakatifu huu
kama dira yetu ya maisha ni tendo lile la kung’ara Kristo Yesu. “Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na
Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, akageuka
sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama
nuru,” Mt 17:1-2.
Kristo anavikwa Utukufu wake
ambao ataunyakua rasmi mara baada ya mateso, kifo na ufufuko huko Yerusalemu.
Hivyo Utukufu wa Kristo hautenganishwi na msalaba/mateso. Kwa maana nyingine
hakuna Utukufu pasipo msalaba. Kama Kristo ndiye njia, kweli na uzima, Yoh
14:6, nasi wafuasi wake itatupasa kupita njia hiyo ya
msalaba, ukweli huu anaotufundisha, ili tuufikie uzima ule, yaani, maisha ya
milele. Kristo ni masiha wa Msalaba, nasi twamfuata Masiha wa Msalaba ili
tuifikie taji ile ya Utukufu baada ya kuhesabiwa haki.
Pili, ni ukamilifu wa nyakati.
Katika tendo hili la kung’ara, tunaelezwa tokeo la watu wawili, yaani, Musa na
Eliya katika mazungumzano na Yesu. “Na
tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye,” Mt 17:3. Katika
tendo hili, Musa anawakilisha Torati, na Eliya Unabii. Hivyo leo Yesu
anaikamilisha Torati. Naye Yesu anatuambia, “Msidhani
ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali
kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi
zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka, hata yote
yatimie,” Mt 5:17-18. Torati inatimilizwa kwa amri ya upendo kwa Mungu na
jirani. “Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo;
maana hiyo ndiyo torati na manabii,” Mt 7:12. Ni ndani na katika Kristo Yesu
tunapata neema na kweli kwa mkono wake. “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa
Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,” Yoh 1:17. Na huku
ndiko kutimilika kwa sheria na kutamalaki kwa upendo, kweli, na neema.
Leo pia unabii wote ulionenwa juu
ya Kristo na historia nzima ya wokovu wetu unakamilika. Unabii huu unafika
ukomo wake kwa uwepo wa Kristo ambaye ni UPENDO WA MUNGU kwetu. Mtume Paulo
anasema, “Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii
utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika,” 1Kor
13:8. Huyu ndiye Kristo Yesu! Kung’ara kwake Bwana wetu Yesu Kristo
kulikoonyesha Ufukufu wake, kunaamsha furaha ya ndani ya Mtume Petro na
kuyasema ya moyoni mwake. “Bwana, ni
vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako
wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya,” Mt 17:4. Hata hivyo
hilo halikuwa kusudi la Yesu kubaki mlimani pale. Yesu inabidi ashuke na
kuukumbatia Msalaba kama alama ya ushindi na hapo ndipo wokovu wako na wangu
ulipotundikwa. Hii ndiyo safari kuelekea kilele kile cha wokovu kama Masiha wa
Msalaba.
Tatu, ni hatma yetu iliyojengeka
katika agano la milele. Kristo ndiye kielelezo chetu na wokovu wetu. Leo Mungu
Baba anauweka ukweli huu hadharani na kusema,Huyu
ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye,” Mt 17:5.
Hili ndilo agano la milele kati yetu na Mungu, na Kristo akiwa ndiye daraja na
mlango halisi wa sisi kupitia kwani ni kwake tu tutakuwa salama kama njia, ni
kwa Kristo tu tunalishwa kweli katika kweli, na Kristo tu ndiye uzima halisi.
Hivyo hapana tena ufunuo ulio wa wazi na kamili zaidi ya ufunuo huu wa Mungu
kupitia mwanaye Mpenzi. Tendo hili linathibitishwa na sauti ya Mungu mwenyewe
kwa viumbe vyote, Mt 17:5. Ndugu yangu, Je, unafuata sauti gani katika maisha
yako? Sauti hii kutoka mbinguni inampa Yesu Kristo Heshima, Mamlaka, na
Utukufu. “Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa
sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu,
ninayependezwa naye,” 2Pet 1:17. Nasi tunapoisikia sauti hiyo na kuishi kweli hiyo,
twajazwa nguvu, heshima na utukufu kwa kuishi ndani na katika Kristo.
Wapendwa wana wa Mungu, zipo
sauti nyingi katika maisha yetu. Je, sauti hizo zinatupeleka karibu na Kristo
Yesu au zinatutenganisha na kweli yake? Kusikia sauti hii ni kuyafanya mapenzi
yake. Na kufanya mapenzi yake Mungu maana yake tuyafanye kila mmoja kadiri ya
wito wake. Hapo ndipo ulipo msalaba wako, na kufaulu kwako ndipo ulipo utukufu
wa msalaba wako.
Ndugu yangu, “kuna furaha ya
kweli na heshima kuifia ‘kweli na haki’ kwa wajinga ili waijue kweli na haki,
kuliko kufa kama mfalme kwa pongezi na makofi ya wapumbavu wadhanio kuijua
‘kweli na haki ilhali hawaijui na wao wenyewe hawajijui.”Leo kuwa Mkristo kwa
kubatizwa tu haitoshi. Leo kuwa Mkristo kunakuhitaji kuwa mpiganaji halisi wa
Kristo kama Mfalme wa haki, kweli, upendo, unyenyekevu, huruma, msamaha, na
uwazi. Ulimwengu uliojaa dhuluma, ufisadi, na matendo ya uvunjifu wa haki za
binadamu, hauwezi kamwe kuukubali Ufalme wa Yesu Kristo kama nilivyosema.
Leo tulio wengi, yaani Wakristo,
tumewekwa katika kikaangio cha kukubaliana na mtazamo huo (dhuluma, ufisadi, na
uvunjifu wa haki za binadamu) au kuukataa kwa gharama kubwa sana hata kuutoa
uhai wako. Hakika njia iliyo rahisi na isiyo na mawaa ni kuusaliti Ukristo
(kumkana Kristo) wako kwa gharama nafuu kama alivyofanya Yuda Eskariote kwa
vipande thelathini vya fedha. Ndiyo maana leo wale tuliotegemea waseme na
kuukemea uovu wapo kimya, na wale waliojaliwa ufahamu wa kupembua mema na
mabaya wamekuwa wasaliti wa iliyo kweli na haki.
Ndugu yangu unayesafari nami
katika tafakari hii, kuwa Mkristo leo ni changamoto kubwa sana, kama ilivyokuwa
kwake Yesu Kristo kuutangaza Ufalme wa Mungu kwa Wayahudi kwa kauli mbiu yake
ile, yaani, “Wakati umetimia, na ufalme
wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15. Jamii ya Yesu wakati
ule ilikuwa kama ndoto kuupokea ujumbe huu-kutubu na kuiamini Injili. Je,
katika hali hii, Yesu alirudi nyuma katika hili kwa vigezo vya kutokukubalika?
La hasha!
Kwa
kuushindilia msumari wa moto katika kusisitiza na kumaanisha asemacho, Yesu
aliwapa wapinzani wake silabasi ya utendaji wake kwa miaka ile mitatu. Naye
anasema juu ya utendaji wake kama ifuatavyo na itakavyokuwa: “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa
maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia
wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru
waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19.
Silabasi hii ndiyo iliyokuwa hatma ya kifo chake kile cha aibu, yaani, kifo cha
Msalaba. Msukumo wa kifo hiki ni Upendo na furaha ya kweli katika haki, kwa
kujua kile akifiacho siyo kitu cha kubumba bali ndio ukweli wenyewe. Yesu
anakuambia wewe na mimi, “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu
kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Bwana wetu Yesu
Kristo amelifanya hili, nasi kama wafuasi wake ni changamoto kubwa kwetu leo.
Hakika Kristo amekupenda wewe na
mimi upeo, na kwa sababu hiyo alikuwa tayari na yupo tayari hadi sasa kufa kwa
ajili yako na mimi. “Basi, kabla ya sikukuu ya
Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika
ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu,
aliwapenda upeo,” Yoh 13:1. Kwa nini basi Mkristo mwenzangu unakuwa na
imani ya mwono wa chura? Hivi leo nikikuuliza uniambia ukweli kuhusu Chura
‘kama amesimama au kachuchumaa waweze nipa jibu sahihi? Kigugumizi hiki cha
kujua mkao wa Chura, ndicho kigugumizi juu ya imani ya Wakristo wengi wa leo.
Wapendwa wana
wa Mungu, yote niliyoyasema ni kukuandaa ili uzame vizuri katika tafakari ya
leo na kadiri ya masomo yake. Mtume Paulo licha ya changamoto alizozikuta baada
ya kuongoka kwake, hakuwa tayari kubadilishwa na mtazamo wa wakati wake na
kujivika koti la uovu. Haki na kweli ndani na katika Kristo Yesu ilibaki kuwa
msingi wa imani yake. Hivyo Barua yake ya pili kwa Timotheo anapenda wafahamu,
na tufahamu kiini na msimamo wa imani yake. Naye anasema, “Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa
dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima,
katika kuomba kwangu usiku na mchana,” 2Tim 1:3. Anaye kumbukwa hapa bila shaka
ni Timotheo mwenyewe aliye mfano halisi wa kweli na haki katika jumuiya yake.
Leo mambo hayako hivyo hata kidogo.
Baadhi yetu kama viongozi wa dini, na wenye kuijua iliyo kweli, na hata kama
hatuiamini kwa kupitia utaratibu uliowekwa kwa taasisi husika kama hatua ya
kuhesabiwa haki ya kuwa kile ulicho, tumekuwa waogeleaji wa kufuata mawimbi ya
maji bila kujali ustadi wa kuogelea kwetu tukitazama ng’ambo ile na iliyo
salama tunayotamani wote kuifikia. Hapa ndipo penye chimbuko la unafiki. Hapa
ndipo kwa makusudi makubwa kabisa katika fikiri, amua na tenda yetu, wafuasi
wetu hutushangaa kwa kwenda kinyume kabisa cha matazamio ya kweli ile
tunayoihubiri na matamanio yake. Hapa ndipo tunapoonekana si tu vituko, bali
watu tusiokuwa na maono na uelewa wa kile tukisemacho, na mwisho kuutabiri
unabii tusioujua ili tuenende na mawimbi ya nyakati zetu tusiyoyajua.
Mkristo mwenzangu, niyasemayo
siyo mageni mbele ya macho yako. Manabii hawa wa kubumba hawaoni shaka wala
haya hata kidogo leo kusema Edgar ndiye “chaguo lile la Mungu” leo kwa watu wa
Mungu. Je, kwa nini wanasema kama wasemavyo? Je, wanajua kile walicho na yale waliyoyalia
kiapo kwa ajili ya taifa la Mungu? Kwa nini basi wanadanganyika kiasi hicho?
Je, wanaifahamu karama ya Mungu ndani ya maisha na utume wao? Mtume Paulo
anamwambia Timotheo hivi, “Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya
Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu,” 2Tim 1:6. Kutokuchoka maana
yake, usitafute urahisi wa jambo na kuutafsiri vinginevyo na karama uliyonayo
kwa kuyaona mawimbi ya muda tu katika wakati wako. Kwa maana nyingine, palipo
na giza tusema giza, na tufanye kadiri iwezekanapo kuuleta mwanga, na palipo
mwanga tusema mwanga na uutetee mwanga huo ili udumu. Kwa nin basi katika hali
hii twaingiwa na woga? Kwa nini tunakufa gazi pasipo ganzi? “Maana
Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi,”
2Tim 1:7. Katika mazingira ya utata kama huu tufanye nini?
Wapendwa wana wa Mungu, katika
mazingira na utata kama huo yatupasa kusimama katika kweli, hata kama nikibaki
mwenyewe. Yesu Kristo kwa kutambua ugumu huu anakuambia wewe na mimi leo kwamba,
“tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. Basi Mwana
akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.” Yoh 8:32, 36. Mwana anatuweka huru,
unapokuwa tayari kujiachia katika minyororo ya upumbavu kwa kuwa tayari
kujifunza na kumsikiliza. Hii ndiyo habari njema ya wokovu, yaani, kulisikia
neno, kulipokea neno, kulitafakari neno, kulishirikisha neno, na kuwa shuhuda
ya neno hilo kwa maisha yako ya kila siku. “Basi usiuonee haya ushuhuda wa
Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja
nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa
akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa
kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo
Yesu tangu milele,” 2Tim 1:8-9. Je, hili lasema lolote juu ya maisha yako kama
Mkristo leo?
Leo mimi kama mfuasi wa Kristo na
muhudumu wake wa karibu, habari njema ya wokovu, yapaswa kuwa kipaua mbele
changu. Na habari njema ya wokovu kwa ufupi kabisa ni kulishinda giza (dhambi)
kwa kuukumbatia mwanga (utakatifu). Kwa habari hii njema ya wokovu,
“inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili
mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili; ambayo kwa ajili ya
hiyo naliwekwa niwe mhubiri na mtume na mwalimu,” 2Tim 1:10-11. Leo mimi kama
mfuasi wa Kristo, na kwa upekee kama mhudumu wa karibu (Mkleri), bila kuijua
habari njema, na kusoma alama za nyakati kadiri ya habari njema ile, ufuasi
wangu na ukaribu wangu hautakuwa na mguso wowote kati ya kile nilicho na
ushuhuda ule nipasao kuutoa. Nitabaki kuwa tukio kama utaratibu wa kawaida bila
historia kama sehemu ya mang’amuzi.
Ndugu yangu, unakuwa historia
kama sehemu ya mang’amuzi unapoyachukulia yale yaliyotokea katika maisha yako, ukitazama
kule unapokutamani kama hitimisho la kila kitu. Hapa tumaini lipo hata kama
linachelewa au kucheleweshwa. Hapa ndipo mateso kama matukio katika maisha ya
kila siku yanapata maana kama asemavyo Mtume Paulo, kwamba, “Kwa sababu hiyo
nimepatikana na mateso haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye
niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana
kwake hata siku ile,” 2Tim 1:12. Hapa siku ‘ile’ ya maanisha ‘uzima ule wa
milele’ tunao utamani.
Tumsifu Yesu Kristo!
"Huyu ni Mwanangu, mpendwa
wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye,” Mt 17:5
Tusali:-Ee Yesu na
Mchungaji wetu, tupatatie masikio hai na yenye kuisikia sauti yako daima hata
pale tunapochanganywa na kelele nyingi katika maisha yetu ya kila siku. Amina
0 blogger-facebook:
Post a Comment