Na. James Waibina
Je wewe ni mzazi au mlezi,au mwalimu? Je unafanyaje
mtoto wako au mwanafunzi anapofanya vizuri katika kazi zake? Najua wengi
mtampongeza kwa namna tofauti. Maneno kama “wewe ni bora kuliko wote”,”una
akili sana” n.k.
Lakini unafahamu madhara ya kupongeza watoto? Ukweli ni
kwamba kuna madhara makubwa kwa kutoa pongezi za aina hii kwa watoto kuliko
ambavyo unaweza kufikiria. Kuna faida kwa muda mfupi tu na madhara makubwa siku
za mbeleni.
Watoto watafurahi sana watakapopongezwa, mfano “hongera
sana, umepata “A” hakika wewe ni mtoto mzuri sana” mtihani unaofuata mtoto
anapopata alama ”C”,unajua atakachofikiri? atakufa moyo sana na kujiona kwamba
“yeye si bora”,”si mtoto mzuri” sababu hakuweza kupata alama “A”.
Atajisikia vibaya na pengine hata kudanganya juu ya
matokeo yao kwasababu hatapenda kusikia vinginevyo toka kwa mzazi wake.
Wataalamu wa saikolojia ya watoto wanashauri kupongeza
watoto kwa njia tofauti na zile ambazo tunazitumia sana kama nilivyoeleza hapo
juu. Badala ya kupongeza matokeo peke yake badala yake tuangalie njia na
jitihada walizotumia kufikia matokeo hayo ya mwisho na kutoa maoni yetu
inavyofaa.
Njia iliyo bora zaidi kumpongeza mtoto aliyepata alama
“A” kwa mfano ingekuwa kumpongeza kwa jinsi alivyosoma kwa muda mrefu na
kuuliza maswali kwa walimu na wazazi ambavyo vimefanya kufikia matokeo hayo-“Hongera
sana,uliweka muda mwingi sana na umesoma kwa bidii,hakuna nguvu zinazoenda
bure,unastahili matokeo haya”.
Kwa kusema hivi unamfanya mtoto aelewe kuwa kumbe
mafanikio yanakuja kwa kufanya kazi na wala si kwa bahati mbaya au njia za
mkato kama ambavyo kushindwa hakuji kwa bahati mbaya pia.
Pongezi
ziendane nakuainisha juhudi na njia zilizopelekea mafanikio.
Pale mtoto anapofanya vibaya ni jukumu la mzazi au
mwalimu kutoa maoni yake ya kweli kwa mtoto.
Sema mfano“unajua kuna
wanafunzi wengi darasani kwako ambao wanasoma kwa bidii pia kama wewe,hivyo ili
upate matokeo bora zaidi kuliko haya inakupasa kuongeza jitihada ili uwe moja
ya kati ya wale wanaofaulu zaidi”.
Usiseme maneno ambayo yamvunja moyo wa kupenda masomo au
kazi zake. Kama ambavyo pongezi zinaumiza lawama zina madhara makubwa zaidi.
Hivyo tafuta jinsi ya kufanya kwa kipimo au kiasi kinachofaa. Maneno kama “wewe
ni mjinga wa kwanza,unaniabisha sana” au “wewe huwezi kufanya
sayansi” yanashusha kujiamini na uwezekano ni kuwa mtoto ataendelea
kufanya vibaya.
Lawama
pekee bila kuonyesha njia ya kuondokana na kushidwa hupelekea mtoto kushindwa
zaidi
Ujumbe mkuu hapa ni kuwa pongeza kwa jinsi ambavyo mtoto
ataelewa kuwa amefanikiwa kwa sababu alifanya kitu fulani. Kuwa matokeo mazuri
yanatokana na kufanya baadhi ya mambo kama kusoma kwa bidii,kufanya majaribio
mengi,ushirikiano na wanafunzi wengine n.k.
Hiyo italeta maendeleo endelevu na pale atakapo anguka
atajua hakufanya yale yanayostahili kuleta matokeo mazuri.
Nakutakieni malezi mema!!!.
0 blogger-facebook:
Post a Comment