Masomo:
Somo: Yer 18:18-20
Zab: 31:5-6 14, 15-16
Injili: Mt 20:17-28
Nukuu:
“Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize
sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana
wameichimbia nafsi yangu shimo,” Yer 18:19-20a
“Lakini haitakuwa hivyo kwenu;
bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye
yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa
Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya
wengi,” Mt 20:26-28
TAFAKARI: Tenda mema nyakati zote; KUTUMIKA ndiyo
sababu ya UKRISTO wetu, na UTAMBULISHO wetu mbele ya Mungu.
Wapendwa wana wa Mungu,
tumshukuru Mungu kwa zawadi ya kila mmoja wetu, kwa maisha na wito anaouishi.
Leo niwakaribishe tena kwa namna ya pekee tutafakari kiini cha maisha yetu kama
wafuasi wa Kristo, yaani, “Tenda mema nyakati zote; KUTUMIKA ndiyo sababu ya
UKRISTO wetu, na UTAMBULISHO wetu mbele ya Mungu.” Wapendwa tulio wengi katika
hili huwa tunakosa mwelekeo na kuanza kujilinganisha kimaisha. Wapo leo walio
kwenye maisha ya Ndoa wangependa kuishi kama watawa na Makleri; na wapo pia
walio watawa na Makleri wangependa leo kuishi kama wana Ndoa. Haya ni matamanio
ya kawaida ya mwanadamu aliye kamilika.
Ndugu yangu, hakuna wito ulio
bora zaidi ya mwingine mbele ya Uso wa Mungu. Kila mmoja wetu ni uzuri wa
Mungu, na Mungu anataka iwe hivyo kwa kumpendeza. Umoja wetu katika utofauti
ndio uzuri wa Mungu. Sote mbele ya Mungu tunamizania iliyo sawa. Na cheo chetu
sote ni kimoja tu, nacho ni UTAKATIFU wetu. Ni ukweli usiotia shaka kwamba,
kila mmoja wetu katika maisha na wito anaoishi, atapimwa kwa maswali haya
mawili mbele ya Mungu;
Swali la kwanza: Umefanya nini kuhusu Mwangu
Yesu Kristo, kwa kuutoa uhai wake kwa ukombozi wako, na kadiri ya wito wako?
Swali la pili: Je, umefanya nini na vipaji
nilivyokupa?
Tusipokuwa tayari kuyafanyia kazi
maswali haya mawili tungali hai hapa duniani; tuwe tayari kulia na kusaga meno,
na tusio na meno hakika tutasaga fizi. Usicheke! Ndugu yangu katika hili,
haijalishi hapa duniani ulikuwa nani, una umaarufu gani, cheo gani, nafasi
gani, na jina gani. Sote tunaitwa kuwa wakamilifu-watakatifu kama Baba yetu
alivyo mtakatifu, Mt 5:48. Tukiwa tu waaminifu kwa kuyaishi hayo maswali
mawili, tutahuzunishwa na kukatishwa tamaa kama Nabii Yeremia alivyofanyiwa.
Nabii Yeremia kwa uchungu na unyonge, anamlilia Mungu kwa kusema, “Niangalie,
Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya
mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo,” Yer 18:19-20a.
Ndugu yangu, wapo wanaotenda mema
kila wakati lakini mwisho wa siku ni kuambulia masengenyo na lawama. Tunapoona
jambo hilo, tusikate tamaa kabisa. Hiyo ni alama ya kwamba kazi uifanyao
yampendeza Mungu na si mwanadamu. Hakuna mti wa mwiba upigwao mawe. Ni mti ule
tu ulio na matunda, tena yalikomaa na kuwiva ndiyo hushambuliwao kwa mawe.
Katika hili Yesu anatuambia wazi, “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na
kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia;
kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii
waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12. Ndugu yangu, wana heri tu wale wafanyiwayo
hayo kwa jina la Yesu.
Tunapata neema na heri
tunapoteseka kwa ajili ya Yesu, na si vinginevyo. Kuteseka kwa ajili ya Yesu ni
kuishi, kutenda, kufikiri, na kupenda kama Yesu. Ni katika maana ya Ufalme wa
Yesu tunaweza kujifunza namna ya kutenda, kufikiri, kuishi, na kupenda. Kristo
Yesu, ni Mfalme wa Amani, Haki, Utii, Unyenyekevu, na Upendo. Kristo huyafanya
haya yote si kwa kutazamwa na watu, au kujipatia sifa binafsi, bali kwa
KUTUMIKA, na kuueneza Ufalme wa Baba yake. Hii ndiyo sababu ya Ukristo wetu.
Nabii Yeremia, anahuzunishwa na
mapigo anayoyapata kutoka kwa wale aliowapigania kwa jina la Mungu. Mema yote
aliyowatendea hawayaoni na badala yake wanakubali kuwa vipofu. Yeremia,
anasema, “Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili niseme mema kwa ajili
yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate,” Yer 18:20b.
Ndugu yangu, wakutulipa mema
tunapoteseka kwa ajili ya Mungu na Mwanaye Yesu Kristo, na kwa kujua sababu ya
mateso hayo, si mwanadamu. Ukweli ni kwamba, “wasio haki watapotea, nao
wamchukiao Bwana watatoweka, kama uzuri wa mashamba, kama moshi watatoweka,”
Zab 37:20. Tuwe tayari kutumika muda na nyakati zote. Tuwe tayari kusema na
kuimba, “Bwana ni jabalí langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu,
mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome
yangu. Na wokovu wa wenye haki una Bwana; Yeye ni ngome yao wakati
wa taabu,” Zab 18:2; 37:39.
Injili yetu ya leo inalizungumzia
kwa mapana swala hili la kutumika kwa ajili ya Ufalme wa Mungu, na ndiyo sababu
ya Ukristo wetu, na utambulisho wetu mbele ya Mungu. Utambulisho wetu mbele ya
Mungu hautokani na sababu ya kukaa kushoto kwake au kulia kwake. Jambo la
msingi ni kuyaishi yale maswali mawili ya Msingi. Tukiwa waaminifu katika hayo,
Yesu anasema, “kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri
kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu,” Mt 20:23b. Waliowekewa
tayari kwa maanisha wale walioyafanya mapenzi ya Mungu kwa uaminifu. Swala hili
halipo mwishoni mwa maisha yetu kama kupokea tunzo fulani, bali kila siku ya
maisha yetu twaishi tunzo hiyo, au kupokonywa tunzo hiyo. Kila siku ya maisha
yetu tupo darasani, na mtihani wetu ni UPENDO. Upendo ndiyo mizania ya kila
kitu tufanyacho.
Ndugu yangu tunayesafiri pamoja
katika tafakari hii, UTAMBULISHO wetu mbele ya Mungu, si maisha ninayoishi,
mfano; Maisha ya ndoa, Utawa, na Ukleri, au cho chote kile ninachoishi kadiri
ya wito wa Mungu, bali utambulisho wetu ni kwa namna tunavyotumika kwa kuyatoa
maisha yetu bila kujibakiza kwa upendo wake Mungu kwa kile tulichoitiwa, na
kama alivyofanya Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo. Utambulisho huu kwa maana nyingine
ni UTAKATIFU tunaojichotea kwa maisha tunayoyaishi hapa duniani kila mmoja
kadiri ya wito wake. UTAMBULISHO huu ndiyo tunzo na UTAKATIFU wetu mbele ya
Mungu.
Ndugu yangu, kwa Mungu hatuendi
na “CV” (Currículum vítae) zetu, kama tulivyozoea kusikua historia fupi ya
Marehemu. Huko mbinguni hakuna kazi tena zaidi ya kuishi umilele tulioandaliwa,
au kuteseka katika umilele tuliojiandalia kwa kuishi ndivyo sivyo. Vyeti vyako,
na historia yako kitaaluma ikuwezeshe kuupata utakatifu huo kwa kutumika vyema.
Kielelezo chetu kama wafuasi wa Kristo, ni Kristo Yesu Mwenyewe.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na
awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika,
na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Mt 20:27-28
Tusali:-Ee Yesu, nipe ufahamu wa kuelewa
vyema sababu ya yale yote unayonikirimia katika maisha na wito ninaoishi, nami
nitumike vyema kwa ajili ya wengine. Amina
0 blogger-facebook:
Post a Comment