Sala mbele ya Altare:
Ee, Mkombozi wangu, ninakuja leo kufuata njia ile uliyoshika siku ya kufa sadaka yetu. Nimetubu dhambi zangu zote; ninataka kugeuza mwendo wangu; ninaomba kwako niwapatie roho za waamini marehemu waliomo toharani, rehema zote zilizotolewa na Kanisa kwa Njia ya Msalaba. Nawe MARIA Bikira Mtakatifu, uliyefuata njia ile nyuma ya mwanao YESU, uniangalie kwa wema, unitie Moyo Mkuu, nisipende dhambi tena, nikivumilia kazi na usumbufu na mateso na matukano yatakayonipata. Amina.
Wimbo:
Umekosa nini we YESU, Kushtakiwa bure kwa Pilato
Wenye kustahili hukumu, Si wewe, si wewe BWANA, ni sisi.
KITUO CHA KWANZA: -YESU ANAHUKUMIWA AFE
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Pilato anamhukumu YESU ingawa haoni kosa lake, anawaogopa Wayahudi. Anabembeleza urafiki wa Kaysari. Ee YESU usiye na kosa, hata mimi ningeweza kutenda mema mengi, lakini naogopa macho ya wenzangu, na maneno yao. Ee BWANA, uniima-rishie utashi wangu, nijitegemee katika kushika madaraka yangu.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
Wimbo:
Ole Msalaba huo mzito, Apagazwa mwana mpenzi wa MUNGU.
Mwili waenea mateso, / Alipa, alipa madhambi yetu
KITUO CHA PILI: YESU ANAPOKEA MSALABA
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
YESU anakubali kuelemewa na msalaba kwa ajili ya wokovu wa watu. Ndivyo anavyonifundisha moyo wa sadaka, moyo wa kujitolea na kujisahau kwa ajili ya wengine. Ee YESU wangu mkarimu, mimi pia ninao msalaba wangu: jirani zangu, mwenzangu wa ndoa, watoto, wazazi wangu, kazi zangu, joto, baridi, njaa, kiu, vishawishi, magonjwa na matatizo mengine ya maisha, wajibu wangu kwa MUNGU, kwa umma na kwa Kanisa. Hayo yote ni msalaba. Unipe ukarimu wako ee YESU, niyapokee bila kunung’unika, na kuyabeba vema.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
Wimbo:
Ona Muumba mbingu na nchi, Yupo chini mzigo wamwelemea,
Na mtu kiumbe chake kwa ukali, Ampiga, ampiga bila huruma.
KITUO CHA TATU: YESU ANAANGUKA MARA YA KWANZA
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
YESU amedhoofika sana, anaanguka chini, kisha anasimama, anaendelea na safari ya ukombozi. Ee YESU uliyeanguka chini ya msalaba kwa ajili ya udhaifu, ukasimama tena; usiniache katika tamaa nikianguka dhambini, bali nisimame mara moja, nikufuate.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
Wimbo:
Huko njiani we MARIA, Waonaje hali ya mwanao,
Ni damu tupu na vidonda, / Machozi, machozi yamfumba macho.
KITUO CHA NNE: YESU ANAKUTANA NA MAMA YAKE
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Wote wawili mama na mwanawe wanaumia sana moyoni kwa ajili ya dhambi zangu. Ee YESU, Mwana wa MARIA, unitilie moyoni mwangu upendo na ibada kwa Bikira MARIA; unijalie na ulinzi wake, nisitende dhambi tena.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
Wimbo:
Kwa Simoni heri ya kweli, Mimi pia YESU nisaidie,
Kuchukua mzigo wa ukombozi, Kuteswa, kuteswa pamoja nawe.
KITUO CHA TANO - SIMONI WA KIRENE ANAMSAIDIA YESU
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Nausifu ukarimu wa Simoni wa Kirene. Ee BWANA unijalie ukarimu kama huo, niitikie nami wito wa kukusaidia kuchukua msalaba. Nitoe zaka na michango yote ya uenezaji wa dini; nijitolee mimi mwenyewe katika kazi ya maendeleo ya dini. Uwajalie vijana wengi wito wa Upadre, waweze kuchukua msalaba pamoja nawe kwa ajili ya wokovu wa dunia. Uwaimarishe viongozi wa dini. Ustawishe moyoni mwa waamini wote mwamko wa utume.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
Wimbo:
Uso wa YESU Malaika, Betlehemu walikuabudu,
Bahati yake Veronika, Kupangusa, kupangusa Mfalme wa Mbingu.
KITUO CHA SITA: VERONIKA ANAPANGUSA USO WA YESU
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Mama huyu ni kinyume kabisa cha Pilato. Veronika anajua analopaswa kutenda, na analitenda bila kujali macho na maneno ya makundi ya watu waovu. Ee YESU, uliyemtuza Veronika zawadi ya picha ya uso wako juu ya kitambaa, unijalie ushupavu na ujasiri wake wa kutenda mema, ili roho yangu ipambwe kwa chapa ya uungwana na utakatifu wako.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
Wimbo:
Wakimvuta huku na huku, Wauaji wanamchokesha bure,
Chini wanamtupa bado kwa nguvu, Aibu, aibu yao milele.
KITUO CHA VII: YESU ANAANGUKA MARA YA PILI
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Ee YESU uliyelegea mno kwa mateso makali, unapoanguka mara ya pili kwa ajili ya udhaifu wa mwili, wanionya kwamba hata mimi naweza kurudi dhambini kwa udhaifu wa moyo. Nipe basi neema ya kuepuka nafasi za dhambi na visa vyenye kunikwaza na kunirudisha dhambini.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
Wimbo:
Wanawake wa Israeli, Msilie kwa sababu hiyo,
Muwalilie hao kwa dhambi, Upanga, upanga ni juu yao.
KITUO CHA VIII: AKINA MAMA WANAMLILIA YESU
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Asanteni sana akina mama kwa moyo wenu wa huruma. Ee YESU uliyetulizwa na wanawake, unipe moyo wa kuwaheshimu akina mama wote. Uwaite na wasichana wengi waingie utawa, ili watulize moyo wako Mtakatifu kwa sala na sadaka zao.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
Wimbo:
Mwokozi sasa ni ya tatu, Waanguka chini ya msalaba,
Katika dhambi za uregevu, Nijue, nijue kutubu hima.
KITUO CHA IX: YESU ANAANGUKA MARA YA TATU
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Ee YESU unayezidi kudhoofika kwa mateso unaanguka mara ya tatu, upate kunistahilia neema ya kuutiisha mwili wangu na kuusulibisha, licha ya kuepuka nafasi za dhambi. Mara nyingi mno ninajibovusha kwa kupenda mno starehe, anasa na tafrija. Ee YESU mwema, nisaidie kuufuata mfano wa Mtakatifu Paulo, niutese mwili wangu na kuutumikisha, ili nipate siku moja tuzo mbinguni.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
Wimbo:
Muje Malaika wa Mbingu, Funikeni mwiliwe kwa huruma,
Vidonda vyake na utupu, Askari, askari wamemvua.
KITUO CHA X: YESU ANAVULIWA NGUO
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Askari wanamvua kwa nguvu nguo yake, iliyogandamana na madonda yake; wanayaamsha mara moja mateso yote aliyoteswa tangu mwanzo. Ee YESU, unayavumilia mateso makali haya, upate kunifundisha kuuvua kwa nguvu moyoni mwangu urafiki mbaya, au kitu kingine chochote kile kinachoharibu urafiki wa MUNGU, hata ikipasa kutoa sadaka kubwa.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
Wimbo:
Hapo MKRISTO ushike moyo, BWANA wako alazwa msalabani,
Mara miguu na mikono, Yafungwa, yafungwa kwa misumari
KITUO CHA XI: YESU ANASULIBIWA MSALABANI
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Ee YESU uliyepigiliwa misumari msalabani, nakutolea akili na utashi wangu, vifungwe pamoja na miguu yako, nipate kuwaza, kusema na kutenda siku zote yale tu yanayolingana na utukufu wa msalaba wako Mtakatifu. Ee YESU, mimi ni mfungwa wako. Nisaidie kuimarisha kifungo hicho kwa sala, Sakramenti na fadhila za KiKRISTO.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
Wimbo:
YESU mpenzi nakuabudu, Msalabani unapohangaika,
Nchi yatetemeka kwa hofu, Na jua, na jua linafifia.
KITUO CHA XII: YESU ANAKUFA MSALABANI
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Ee YESU uliyekufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu, unijalie niichukie dhambi, nisiishi kamwe katika dhambi. Nifahamu kwamba nilipobatizwa kwa jina lako, nilibatizwa katika mauti yako ili utu wangu wa kale usulibishwe nawe, mwili wa dhambi uangamizwe nisitumikie tena dhambi.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
Wimbo:
Mama MARIA mtakatifu, Upokee maiti ya Mwanao,
Tumemwua kwa dhambi zetu, Twatubu kwake na kwako.
KITUO CHA XIII: YESU ANASHUSHWA MSALABANI
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Ee YESU uliyeshushwa msalabani baada ya kufa, unijalie nidumu katika maisha ya kujitoa sadaka mpaka siku ya kufa kwangu. Nielewe na kukubali kwamba baada tu ya kufa ndio mwisho wa vita na mashindano ya KiKRISTO.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
Wimbo:
Pamoja nawe kaburini, Zika dhambi na ubaya wa moyo,
YESU tuwe Wakristo kweli, Twakupa twakupa sasa mapendo
.
KITUO CHA XIV : YESU ANAZIKWA KABURINI
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Ee YESU, ulizikwa kaburini, ukafufuka siku ya tatu. Mimi pia nilizikwa pamoja nawe kwa njia ya ubatizo katika mauti yako. Kwa vile wewe ulifufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa BABA, unijalie nami nifufuke, yaani nishike mwenendo mpya, mwenendo wa uzima wa milele.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
Wimbo:
Katika roho yangu BWANA, Chora mateso niliyokutesa,
Nisiyasahau madeni, Na kazi, na kazi ya kuokoka.
(Hiari yako - Mbele ya Altare)
KITUO CHA XV: YESU AMEFUFUKA
K. Ee YESU tunakuabudu, tunakushukuru.
W. Kwa kuwa umewakomboa watu kwa Msalaba wako Mtakatifu.
Habari njema aliyotuletea YESU ni kwamba baada ya kila Ijumaa Kuu huja sikukuu ya Pasaka; kwamba punje ya ngano isipoanguka ikafa, hukaa hali hiyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa maozo mengi. Twakushukuru, ee YESU, kwa mateso yako, lakini twakushukuru hasa kwa ufufuko wako, kwa kuwa huo ndio unaotupa hakika ya kuwa hatukuzaliwa kwa ajili ya mateso na maumivu, bali kwa ajili ya heri ya milele.
= BABA yetu…= Salamu MARIA… = Atukuzwe BABA…
K. Ee BWANA, Utuhurumie.
W. Utuhurumie.
Roho za waamini wapate rehema kwa MUNGU, wapumzike kwa amani. Amina.
***
SALA YA MWISHO:
YESU wangu, kwa uchungu wote ulioona juu ya msalaba, na kwa kuzimia kwako kwa ukali wa mateso, unijalie nguvu ya kuvumilia kwa moyo taabu zote sasa na saa ya kuzimia kwangu. Nawe MARIA Mamangu, kwa uchungu wote ambao moyo wako umejaa ulipomwona mwanao mpenzi kuinama kichwa na kuzimia, unifadhili nife kifo chema. Amina.
© Fumbuka BLOG.
© Fumbuka BLOG.
0 blogger-facebook:
Post a Comment