Na. James Waibina
Mpendwa msomaji wa Jarida letu la Fumbuka, Nichukue fursa hii ya
pekee kukukaribisha katika makala hii ya Biblia ni Jibu, makala ambayo
hukuletea mafundisho mbalimbali yahusuyo Biblia tangu kuumbwa kwa Mwanadamu,
Historia ya Ukombozi na Maisha mapya baada ya hapa duniani kupitia katika
kitabu cha Ufunuo, lakini pia kupitia makala hii utapata majibu ya maswali
mbalimbali yahusuyo imani kwa misingi ya Biblia kama jina lenyewe lisemavyo “Biblia ni Jibu”
Leo katika Makala hii ninakuletea Maandalizi ya Msingi yapaswayo
kufanyika kabla ya Kusoma Biblia ili utakapoisoma uielewe na kuweza kuiishi.
Usisome Biblia kimazoea jipange kwanza kwa kuzingatia yafuatayo;-
1.
Mwamini Yesu Kristo
Msomaji wa Neno la Mungu ni lazima amwamini Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi
wake, mtu asiyemwamini Yesu hawezi kukubali wala kuamini Neno la Mungu (1
Wakorintho 2:14). Kwa hiyo, Wokovu ni kwa njia ya Imani peke yake katika Kristo
(Waefeso 2:8-9). Roho wa Mungu huwawezesha wasomaji wa neno wapate kuelewa vitu
vya Rohoni.
2.
Kubali Kwamba Biblia Ina
Pumzi Ya Mungu.
Neno la Mungu linajisema lenyewe kwamba lina pumzi ya Mungu (2 Timotheo
3:16-17). Kusoma neno la Mungu ni lazima uanze kwa kushukuru ukweli wa neno.
Haihitajiki imani kubwa sana bali ni kukubali ukweli kwamba Biblia ni kweli na
haina mapungufu.
3.
Mwombe Mungu
Maombi ni muhimu katika kuyaelewa maandiko. Neno la Mungu linatuelekeza
kwamba ikiwa mmoja wenu atapungukiwa na hekima na aombe dua kwa Mungu awapaye
wote kwa ukarimu wala hakemei naye atapewa. (Yakobo 1:5). Pia Katika Yohana
twasoma “na huu ndio ujasiri tulionao
kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atusikia” (1 Yohana
5:14).Pia twasoma Mathayo 7:7-8.
4.
Jifunze Kwa Juhudi Na
Uvumilivu
Kwa kuwa kurasa nyingi za maneno ya Mungu wakati mwingine hazieleweki
unaposoma, jitihada na uvumilivu vinahitajika katika kujifunza neno la Mungu
(2Tim 2:15), Kwa kuwa sisi ni wanadamu wenye ufahamu mfupi, maandiko yanasema;
jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu mtenda kazi asiye na sababu ya
kutahayari ukilitumia kwa halali neno la Kweli.
5.
Jipatanishe na Mungu
Ni vizuri kuungama dhambi zako kila wakati ili umruhusu Mungu asafishe
maisha yako, ili kwamba ushirika wako na Mungu udumu (1Yohana 1:6-10). Tunapotambua
kukiri dhambi zetu na kuziungama inatufanya sisi kuwa waangalifu na kila namna
ya dhambi katika kufikiri, kunena au katika kutenda na hivyo tunashinda.
6.
Ishi Kwa Kufuata Mapenzi Ya Mungu
Bwana Yesu alisema “Mtu akipenda kuyatenda mapenzi ya Mungu yake atajua
habari ya yale mafunzo kwamba yatoka kwa Mungu au kwamba mimi nanena kwa nafsi
yangu tu. Ujuzi huleta majivuno bali upendo hujenga. (1Kor 8:1).
Mpendwa Msomaji, Neno la Mungu ni chakula cha Roho zetu hivyo kulisoma na kuliishi hutufanya tuimarike kiroho, hayo yatawezekana tu kwa kujipanga na kufuata hiyo misingi niliyoielezea hapo juu. Tusikubali kusoma biblia kimazoea.
Twasoma:
"Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza"
_ (Luka 14:28-30)
Imetayarishwa na: James Waibina
Kwa Maoni /Ushauri: Tuwasiliane kupitia
0713515059- (WhatsApp) au jameswaibina@fumbuka.co.tz
*************************************MBARIKIWE******************************
0 blogger-facebook:
Post a Comment