SOMO 1
Dan. 3:25, 34-43
Ndipo Azaria akasimama akasali hivi,
akifumbua kinywa chake katikati ya moto na kusema:
Usituache kabisa, kwa ajili ya jina
lako, wala usilitangue agano lako na kutuondolea rehema zako, kwa ajili ya
Ibrahimu umpendaye, na kwa ajili ya Isaka mtumishi wako, na Israeli mtakatifu
wako kama nyota za mbinguni na kama mchanga wao pwani. Maana sisi, Ee Bwana,
tumekuwa duni kuliko mataifa yote, na kudhulumiwa leo katika ulimwengu wote kwa
sababu ya dhambi zetu. Sasa hakuna mfalme wala nabii wala kiongozi; hakuna
dhabihu wala kafara wala sadaka wala uvumba; wala mahali pa kukutolea dhabihu
na kuona rehema.
Lakini kwa moyo uliovunjika na kwa roho
nyenyekevu tukubaliwe nawe, na sadaka yetu iwe machoni pako leo kama dhabihu za
kondoo waume na ng’ombe, na kama kondoo wanono elfu kumi. Nasi tukufuate kwa
unyofu, maana wanaokutumaini Wewe hawataaibika.
Na sasa tunakufuata kwa moyo wote;
tunakucha na kuutafuta uso wako. Usitufedheheshe, bali ututendee kwa kadiri ya
fadhili zako, sawasawa na wingi wa huruma zako. Utuokoe kwa kadiri ya maajabu
yako, na kulitukuza jina lako, Ee Bwana.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 25:4-9 (K) 6
(K) Ee Bwana, kumbuka rehema zako na
fadhili zako.
Ee Bwana unijulishe njia yako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha. (K)
Ee Bwana kumbuka rehema zako na fadhili
zako,
Maana zimekuwako tokea zamani.
Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu,
Wala maasi yangu.
Ee Bwana, kwa ajili ya wema wako. (K)
Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi
njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake.
(K)
SHANGILIO
Yn. 11:25, 26
Mimi ndimi ufufuo na uzima, asema
Bwana; Yeye aniaminiye mimi, hatakufa kabisa na milele.
INJILI
Mt. 18:21-35
Petro alimwendea Yesu akamwambia, Bwana,
ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia,
Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.
Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni
umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza
kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha
kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote
alivyo navyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia
akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule
akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni.
Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa
wajoli wake, aliyemwia dinari mia; akamkamata, akamshika koo, akisema, Nilipe
uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi akisema, Nivumilie,
nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata
atakapoilipa ile deni.
Basi wajoli wake walipoyaona
yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote
yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu,
nimekusamehe wewe deni ile yoe, uliponisihi; nawe pia haikukupasa kumrehemu
mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika,
akampeleka kwa watesaji, hata atakapolipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu
wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehekwa mioyo yenu kila mtu ndugu
yake.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
0 blogger-facebook:
Post a Comment