Mitume wa Yesu walipigwa na bumbuwazi baada ya kuambiwa kwamba wanapaswa kusamehe na kusahau, hali iliyowafanya kumwomba Yesu ili aweze kuwaongezea imani. Ili kuweza kudumu katika imani ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, waamini hawana budi kuiishi, kukua na kudumu katika imani hata mwisho kwa kuirutubisha kwa Neno la Mungu na Sala, daima wakimwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaongezea, ili iweze kutenda kazi kwa upendo na kuzidi kuwa na matumaini kwa kukita mizizi yake katika imani ya Kanisa. Ukuaji wa imani katika maisha ya Padre ndiyo tema iliyoongoza tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Wakleri wa Jimbo kuu la Roma, tarehe 2 Machi 2017 iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano.
Katika tafakari yake, Baba Mtakatifu amekazia mambo makuu matatu: kumbukumbu ambayo inajikita katika imani ya Mababa wa Kanisa na Kanisa katika ujumla wake. Hii ni imani inayotenda na kushuhudiwa katika upendo. Matumaini yanamkumbusha Padre kwamba, Mwenyezi Mungu amemwezesha kuwa katika safari inayofumbatwa katika matumaini ambayo ni dira na mwongozo wa maisha. Mang’amuzi ya nyakati ni maamuzi ambayo Padre anapaswa kuyafanya ili kutekeleza tendo jema kadiri ya mapenzi ya Mungu, kwa kuwa na kumbu kumbu ya neema na baraka ambazo Mwenyezi Mungu amemkiria kwa nyakati mbali mbali; kwani kuna watu waliofariki dunia wakiwa na imani; huu ni umati mkubwa wa mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake.
Matumaini yanamwezesha Padre kuwa na imani na mshangao wa matendo ya Mungu katika maisha yake, kama anavyoshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Msalaba linalowavuta wote kwake, baada ya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maondoleo ya dhambi, ushuhuda wa kweli una mvuto na mashiko anasema Baba Mtakatifu Francisko! Mang’amuzi sahihi na thabiti yanamwilishwa katika upendo, ili kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha, kwani Mungu anaangalia yale yaliyofichika sirini. Huu ni muda wa toba na wongofu wa ndani, kwa kukumbuka upendo wa Mungu unaofumbatwa kwenye Fumbo la Msalaba, ili kumwachia Mwenyezi Mungu, aweze kuongoza maisha ya Padre wake.
Baba Mtakatifu anasema, kukua katika imani kunakwenda sanjari na ukuaji wa upendo, mshikamano, ufahamu wa Neno la Mungu na kufundisha yote ambayo Kristo Yesu amewaamuru mitume wake, kwani utangazaji wa awali kabisa wa Injili unapaswa kufumbatwa kwa namna ya pekee katika majiundo makini na ukomavu katika imani, Mafundisho tanzu ya Kanisa; kwa kukutana na Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha, ili hatimaye, kukuza ari na mwamko wa kuwa ni mtume mmissionari. Msalaba wa Kristo ni kielelezo makini cha imani na ni chimbuko la utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu; yaani Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kuna umati mkubwa wa mashuhuda wa Fumbo la Pasaka, mwaliko wa kuendelea kutembea katika matumaini, kwa kuwa makini kwa vishawishi dhidi ya imani.
Baba Mtakatifu anasema, katika Waraka wake wa Furaha ya Injili amefafanua kwa kina na mapana umuhimu wa kumbu kumbu kama sehemu ya imani kama ilivyokuwa kwa Waisraeli katika Agano la Kale, kwani furaha ya kuinjilisha daima inachipuka kutoka kwenye kumbu kumbu ya shukrani, neema ambayo waamini wanapaswa kuiomba daima. Kuna mashuhuda wa imani ambao kweli wameacha chapa ya kudumu katika maisha ya watu; hawa pengine ni watu wa kawaida lakini ushuhuda wao umekuwa na mashiko katika imani ya watu! Kimsingi kabisa, mtu anayeamini ni mtu anayekumbuka!
Imani inarutubishwa kwa kumbu kumbu inayozamisha mizizi yake katika historia iliyopita, iliyopo, ili kuweza kuwa na mwelekeo mpana kwa siku za usoni. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kumbu kumbu endelevu ya imani, msingi wa wokovu wa binadamu unaofumbatwa katika: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu, mhimili wa imani ya Kanisa. Ibada ya Misa Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni ushuhuda wa upendo usiokuwa na kikomo, mwaliko ni toba na wongofu wa ndani, ili kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, imani inarutubishwa kwa matumaini yanayofanya rejea katika kumbu kumbu kwa uwepo endelevu wa Mwenyezi Mungu; kwa kufiriki na kutenda ili kumwilisha upendo na huruma ya Mungu kwa maskini na wahitaji zaidi. Imani inashuhudiwa katika matendo yanayofumbatwa katika matumaini na huduma makini. Mapadre wajitahidi kuondokana na vishawishi vinavyoweza kudumaza ujasiri na ari katika imani, licha ya kutambua udhaifu wao kwani wanaimarishwa kwa neema na nguvu ya Mungu, kwani ushindi wa Kristo ni Msalaba ambao pia ni bendera ya ushindi.
Moyo wa kimissionari unatambua mipaka hii, lakini unapiga moyo konde kwa kuwa dhaifu miongoni mwa watu dhaifu, kwa kuendelea kujifunza Injili ya Kristo na kujiweka chini ya Roho Mtakatifu na kwa njia hii, mwamini ataweza kujisadaka kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kama alivyofanya Zakayo Mtoza ushuru. Mtume Petro ni kielelezo cha ushuhuda wa imani iliyoguswa na kutikiswa katika msingi wake, lakini ikaimarishwa kwa sala na uwepo wa Kristo Yesu baada ya toba na wongofu wa ndani, ili aweze kuwaimarisha ndugu zake Kristo katika imani.
Mtume Petro ni mtu mwenye imani thabiti kiasi cha kukiri kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu aliye hai! Akaonesha imani haba kama kiatu cha raba alipomkana Yesu mara tatu na pale alipojitia umwamba wa kutaka kutembea katika juu ya maji! Lakini, Petro ni mwamba ambao Kristo amejenga Kanisa lake juu yake. Daima Mtakatifu Petro ameendelea kuwa ni mvuvi na mdhambi, lakini daima kwa kumwambata Kristo Yesu kuwa ni kiini cha maisha na utume wake! Petro alimtumainia Yesu kwani alikuwa na maneno ya uzima!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu alimwombea Mtakatifu Petro ili asitumbukie katika kishawishi na kashfa ya Msalaba, ili hatimaye, aweze kuwaimarisha ndugu zake katika imani, changamoto kwa waamini kumkimbilia Mungu ili asiwatie kishawishini, bali awaokoe na yule mwovu! Hii inatokana na ukweli kwamba, binadanu ni dhaifu! Waamini wamkimbilie daima Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaimarishia imani. Mapadre wajifunze kutoka kwa Mtume Petro umuhimu wa kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kama alivyofanya Kristo Yesu, Alhamisi kuu, kwa kuwaosha Mitume wake miguu; waendelee kujizatiti kuwaimarisha ndugu zake katika imani, kwa njia ya ushuhuda wa sala ya Kristo kwa mitume wake.
Hii yote ni mifano hai ya jinsi ambavyo Mitume wa Yesu walivyoteseka katika kukuza na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Yesu daima anawaonesha huruma, upendo na msamaha, lakini wafuasi wa Kristo wanakumbushwa kwamba, ubaya na dhambi havikufungwa katika udhaifu wa binadamu, ndiyo maana Neno wa Mungu alifanyika Mwili, akazaliwa na kutunzwa kwenye Familia Takatifu ya Nazareti. Ubaya na dhambi ni matokeo ya kiburi cha mwanadamu anayetaka kujifananisha na Mungu. Yesu alitambua udhaifu wa Petro na wala havikumtisha, lakini alikuwa na hofu kubwa pale Mitume walipokuwa wanalumbana kuhusu madaraka!
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Mwenyezi Mungu anayeruhusu vishawishi vinawasaidia waja wake kukuza imani na kwamba, daima anakuwepo ili kuwategemeza, anataka kuendeleza urafiki na uaminifu wake. Yesu alimkaripia Petro alipohoji uhusiano wake na Yohane, mwanafunzi ambaye alipendwa zaidi na Yesu! Ukweli, umoja, upendo na mshikamano ni mambo yanayoweza kuimarisha imani kwa Kristo na Kanisa lake. Yesu alifahamu nyakati za kumwinua Mtakatifu Petro na nyakati za kumfundisha ukomavu wa imani. Petro alionesha ukomavu katika maisha yake kwa kusema na kutenda kutoka katika sakafu ya moyo wake! Yesu akampenda, akamhurumia, akamsamehe na kumwiimarisha katika imani, ili awaimarishe pia ndugu zake katika Kristo Yesu!
Chanzo: Radio Vatican.
0 blogger-facebook:
Post a Comment