Masomo:-
Somo: Isa 1:10, 16-20
Zab: 50: 8-9, 16bc-17, 21, 23
Injili: Mt 23:1-12
Nukuu:
“Jiosheni, jitakaseni; ondoeni
uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;
jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni
yatima haki yake; mteeni mjane,” Isa 1:16-17
“Bali ninyi msiitwe Rabi, maana
mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu,” Mt 23:8
TAFAKARI: “Utayari wa Mungu kusamehe; Yesu Kristo
Mpatanishi wetu na Mungu na mwenye mamlaka ya kusamehe dhambi.”
Wapendwa wana wa Taifa la Mungu,
leo tutafakari kwa pamoja “Utayari wa Mungu kusamehe; Yesu Kristo Mpatanishi
wetu na Mungu na mwenye mamlaka ya kusamehe dhambi.” Ndugu yangu, mwito wa
Nabii Isaya kwa watu wa Sodoma na Gomora, ni kuacha njia mbaya na kumrudia
Mungu. Mungu yupo tayari muda wote kusamehe kwa sababu MSAMAHA ni moja ya
uhasili wake.
Mungu daima ni, “mwenye kuwaonea
huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye
kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa
baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha nne,” Kut 34:7.
Tendo la kuwapatiliza watoto uovu
wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha nne, ni matokeo ya laana.
Laana ni kinyume cha baraka. Kwa upande mwingine, laani huenda hadi kizazi cha
nne. Kwa mantiki hiyo, yapo mambo fulani watu huteseka bila kujua, na chanzo
chake yawezekana watu fulani, wakati fulani, hawakuenenda katika njia ya Bwana.
Kuepuka tatizo hilo, Nabii Isaya
anawatahabarisha watu wa Sodoma na Gomora na kusema kwamba, “Jiosheni,
jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni
kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni
walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteeni mjane,” Isa 1:16-17
Ndugu yangu, upendo wa Mungu
kwetu na utayari wake wa kusamehe hauna mfano. Kinachotokea kwa upende watu, ni
kukubali kufa na tai shingoni, ni kwa sababu ya kiburi chetu. Chapa tulioyonayo
ya sura na mfano wake Mungu, Mwa 1:27, ndiyo mvuto mkubwa wa hurama yake kwetu.
Mungu wetu hapendi kuona tunaangamia bure. Anasema hata kama tungekuwa na dhambi
nyekundu kama bendera, yupo tayari kusameha na kuzifanya nyeupe kama sufu, Isa
1:18.
Mpendwa, kwa nini unakubali
kuumwa na mbwa aliyefungwa na kamba kwenye mti? Dhambi, ni kujipeleka ukijua
kabisaaa! Wokovu ni kumrudia Muumba wako ukijua uzuri na wema wake. Hata hivyo,
pamoja na madhaifu yetu, Mungu bado hajakata tamaa nasi.
Pamoja na watu kutokutambua wema
wa Mungu, “ila wakakataa kutii, wala hawakuyakumbuka maajabu yako, uliyoyafanya
kati yao; lakini wakafanya shingo zao kuwa ngumu, na katika kuasi kwao wakaweka
jemadari, ili wairudie hali ya utumwa; lakini wewe u Mungu, uliye tayari
kusamehe, mwenye neema, mwenye huruma nyingi, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa
rehema, basi hukuwaacha,” Neh 9:17.
Ndugu yangu, watu wengi
hujihukumu wenyewe na kujifungia neema za kupatanishwa na Mungu. Ni kosa kubwa
kuishi katika hatia fulani. “Na kama mtu akifanya dhambi, na kutenda mambo hayo
mojawapo ambayo Bwana alizuilia yasifanywe, ajapokuwa hakuyajua, ni mwenye
hatia vivyo, naye atachukua uovu wake,” Wal 5:17. Lakini Mungu wetu hakai na
hasira yake milele. Kufanya hivyo ni kinyume cha uhalisia wake. Yeye hufurahia
rehema. “Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia
kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana
yeye hufurahia rehema,” Mik 7:18.
Katika Injili yetu ya leo, Yesu
anatoa angalizo kwa wanafunzi wake akisema wawe macho juu ya waandishi na
mafarisayo kwa kujihesabia haki na kukaa katika kiti cha Musa. Wapendwa, Musa
anawakilisha sheria. Mafarisayo na waandishi kukaa katika kitu cha Musa ni kuwa
juu ya Sheria za Mungu. Wanajichukulia mamlaka yasiyo yao, na kuwabebesha watu
mizigo mizito isiyo bebeka.
Ushauri wa Yesu kwetu kuhusu
Mafarisayo na Waandishi, ni kutenda na kuisha wasemayo, ila kwa mfano wa
matendo yao tusitende. Yesu Kristo anaona kasoro ya watu hawa na anawakemea kwa
kusema, “ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu
ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi
waingie,” Mt 23:13. Wanausema na kuusifia utakatifu bila kuuishi.
Badala yake, Yesu anatutaka
kufanya hili, “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi
nyote ni ndugu,” Mt 23:8. Mwalimu wetu ni Yesu Kristo, na katika Yeye sote kwa
kupitia sakramenti ya Ubatizo tumerudishiwa urithi wetu na kuwa wana wa Mungu.
Kwa tukio hili la kupatanishwa na Mungu Baba kupitia mwanaye Mpenzi Yesu
Kristo, sisi sote leo ni ndugu. Kwa upatanisho huo, Yesu Kristo anayo mamlaka
ya kusamehe dhambi. “Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri
duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Ondoka, ujitwike
kitanda chako, uende nyumbani kwako,” Mt 9:6
Ndugu yangu, nani aliye tabibu
zaidi ya Bwana wetu Yesu Kristo? Ni kwa Yesu Kristo tunaweza kuponywa na kuwa
huru tukiwa na haja hiyo. “Na makutano walipojua walimfuata; akawakaribisha,
akawa akisema nao habari za ufalme wa Mungu, akawaponya wale wenye haja ya
kuponywa,” Lk 9:11. Je, mwenzangu humuitaji Yesu? Kuponywa huku na Yesu ni
matokeo ya kuziungama dhambi na kuomba uponyaji huo. Tendo hili linatupelekea
kuwa na haja ya kuponywa. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana,
mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii,” Yak
5:16. Amina
Tumsifu Yesu Kristo!
“Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni
mmoja, nanyi nyote ni ndugu,” Mt 23:8
Tusali:-Ee Yesu, usituache waja wako
tunapoitaji uponyaji wako. Amina
0 blogger-facebook:
Post a Comment