Karibu Mpenzi Msomaji na mfuatiliaji wa Tafakari Zetu katika Blog Yetu ya Fumbuka..
Katika kipindi
hiki cha Kwaresima tunapotafakari Mateso na Kifo cha Yesu Kristo Msalabani kwa
ajili ya ukombozi wa mwanadamu, leo tunakuletea Tafakari ya Maneno Saba (7)
aliyoyatamka Yesu akiwa Msalabani wakati akisulubiwa.
Namba saba, kama ilivyo namba arobaini katika desturi za Kiyahudi ina
maana ya utimilifu au ukamilifu. Namba saba inathibitisha kuwa kitu ni kamili
au kinajitosheleza.
Karibu Tutafakari kwa pamoja maneno saba ya Yesu msalabani:
(I) “BABA UWASAMEHE, KWA KUWA HAWAJUI WATENDALO”
Na
walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale
wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. Yesu akasema,
“Baba, uwasamehe, kwa hawajui watendalo.” Wakagawana mavazi yake, wakapiga
kura.
-(Luka
23:33-34)
Neno la kwanza la Yesu msalabani lahusu msamaha. Msamaha ni tabia kuu ya
Mungu. Ukuu wa Mungu haupo tu katika kazi kubwa na ajabu ya uumbaji, bali pia
ukuu wake upo katika sifa yake ya kusamehe.
Neno hili ni habari njema ya wokovu. Inatosha neno hilo moja la msamaha
kumtambua Yesu kuwa ni mkombozi. Kazi yote ya kuhubiri na kufanya miujiza
ilikuwa inahusu msamaha.
Msamaha ndiyo hasa ujumbe mkuu wa mafundisho yote na miujiza yote ya
Yesu. Mafundisho yote ya Yesu yalimwelekeza Mungu kuwa ni Baba mwenye huruma,
mafundisho hayo yalimwelekeza mwanadamu atumie vizuri tabia hiyo kuu ya Mungu
kwa kuomba msamaha.
Miujiza yote ya Yesu ilihusu msamaha wa dhambi; ndiyo maana wengi ambao
aliwafanyia miujiza aliwaambia, umesamehewa dhambi zako.
Pia neno hili la kwanza la Yesu msalabani linatufundisha kuwa jambo la
kwanza kabisa kwetu sisi katika kuhusiana na Mungu ni kuomba msamaha.
Mara nyingi sisi mbele ya Mungu tunaomba mambo mengine ambayo tunaamini
kuwa ni mazuri na tunasahau kuomba jambo kuu kuliko yote mbele ya Mungu. Leo
Yesu anatufundisha jinsi ya kuomba mbele ya Mungu.
Yesu anatuonea huruma sisi wanadamu anavyotuona tunatenda dhambi; ndiyo
maana anasema hatujui tutendalo. Ni kweli kabisa! Tunapotenda dhambi hatujui
tundendalo kwani sisi asili yetu ni Mungu; tuliumbwa kwa sura na mfano wa
Mungu. Tunapotenda dhambi tunaifuta sura na mfano wa Mungu ili tufanane na
ibilisi.
Lakini, Yesu anatufundisha pia kuwa nasi kati yetu yatupasa kuombana
msamaha. Katika mafundisho yake anasema:
Iweni na
huruma kama Baba yenu wa mbinguni alivyo na huruma-(Luka 6:36)
Hata tunaposali, Yesu anatufundisha kuwa Mungu atatumia kipimo kilekile
tunachotumia sisi kusameheana kati yetu:
Utusamahe makosa yetu kama na sisi
tunavyowasamehe wale waliotukosea.
Yesu anatufundisha tusameheane siku zote, katika lolote na mara zote:
Kisha Petro
akamwendea akamwambia, “Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe?”
Hata mara saba? Yesu akamwambia, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara
sabini.”-(Mathayo 18:21-22)
Amri kuu ya Mungu ni upendo. Kielelezo kikuu cha upendo ni msamaha. Yesu
ametufundisha kupendana, na yeye mwenyewe anakuwa mfano mzuri kwa kutangaza
msamaha pale msalabani. Mkristo asiyejua kusamehe, huyu bado hajawa mkristo.
Yesu anasema;
mkipendana kati yenu, wote watajua kuwa
ninyi ni wafuasi wangu.
Kwa hiyo, kitambulisho cha ukristo ni upendo; kitambulisho cha upendo ni
msamaha. Tena, Yesu katika mafundisho yake, anasisitiza tuwapenda hata maadui
zetu na tuwaombee ili tuweze kuwa kweli wana wa Mungu.
“Mmesikia
kwamba imenenwa: Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi
nawaambia: Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa
Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema,
huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi
mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je, nao hawafanyi yayo hayo? Tena
mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa,
je, nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakauwa wakamilifu, kama Baba yenu wa
mbinguni alivyo mkamilifu.” -(Mathayo 5:43-48)
Yesu ni mfano mzuri kwetu kwani pale msalabani anawasamehe adui zake
wanaomsulibisha na anawaombea msamaha kwa Mungu. Hakika Yesu ni mwalimu halisi
kwani kile alichofundisha kwa maneno, yeye mwenyewe ametekeleza kwa matendo.
Msamaha una pande mbili: kuomba msamaha na kutoa msamaha. Kati ya haya
mawili ni lipi gumu zaidi?
Jiulize; wewe waweza kumsamehe mtu kwa lolote alilokufanyia?
Kumbuka: kutenda dhambi ni ubinadamu; kusamehe ni umungu.
Nakutakia Tafakari Njema.
Katika Makala Ijayo
tutatafakari Neno la Pili la Yesu Akiwa Msalabani….
Ee Yesu tunakuabudu na tunakushukuru; Kwa Kuwa Umewakomboa
Watu kwa Msalaba Wako Mtakatifu.
**********************************************************************
0 blogger-facebook:
Post a Comment