SOMO 1
Isa.
65:17-21
Bwana asema: Tazama, mimi naumba mbingu mpya na
nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni. Lakini
furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama,
naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha.
Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe
watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya
kuomboleza. Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku
zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi
mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa. Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake;
watapanda mizabibu, na kula matunda yake.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA
KATIKATI
Zab.
30:1, 3-5, 10-12 (K) 1
(K) Nitakutukuza, ee Bwana, kwa maana umeniinua.
Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua,
Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
Umeniinua nafsi yangu,
Ee Bwana, kutoka kuzimu.
Umenihuisha na kunitoa
Miongoni mwao washukao shimoni. (K)
Mwimbieni Bwana zaburi,
Enyi watauwa wake.
Na kufanya shukrani.
Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.
Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,
Katika radhi yake mna uhai.
Huenda kilio huja kukaa usiku,
Lakini asubuhi huwa furaha. (K)
Ee Bwana, usikie, unirehemu,
Bwana, uwe msaidizi wangu.
Uligeuza matanga yangu kuwa machezo;
Ulinivua gunia, ukanivika furaha.
Ee Bwana, mungu wangu,
Nitakushukuru milele. (K)
SHANGILIO
Eze.
33:11
Sikufurahii kufa kwake mtu mwovu, asema Bwana, bali
aiache njia yake mbaya, akaishi.
INJILI
Yn.
4:43-54
Baada ya siku mbili hizo Yesu aliondoka huko,
akaenda Galilaya. Kwa maana Yesu mwenyewe alishuhudia ya kwamba nabii hapati
heshima katika nchi yake mwenyewe. Basi alipofika Galilaya, Wagalilaya
walimpokea; kwa kuwa wameyaona mambo yote aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati
wa sikukuu; maana hao nao waliiendea sikukuu.
Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo
alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe
hawezi huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi mpaka
Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa
kufani. Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa?
Yule diwani akamwambia, Bwana, ushuke asijakufa mtoto wangu. Yesu akamwambia,
Enenda; mwanao yu hai. Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye
akashika njia. Hata alipokuwa akishuka, watumwa wake walimlaki, wakisema ya
kwamba mtoto wake yu hai. Basi akawauliza habari ya saa alipoanza kuwa hajambo;
nao wakamwambia, jana, saa saba, homa ilimwacha. Basi babaye akafahamu ya kuwa
ni saa ile ile alipoambiwa na Yesu, Mwanao yu hai. Akaamini yeye na wote wa
nyumbani mwake.
Hiyo ni ishara ya pili aliyoifanya Yesu, alipokuwa
ametoka Uyahudi kufika Galilaya.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
0 blogger-facebook:
Post a Comment