Baada ya kutafakari Neno la Kwanza katika Makala iliyopita, mpendwa
msomaji na mfuatiliaji wa Tafakari katika Blog yetu ya Fumbuka, karibu tena leo
tutafakari neno la pili alilotamka Yesu akiwa Msalabani:
(II) “AMIN, NAKUAMBIA,
LEO HIVI UTAKUWA PAMOJA NAMI MBINGUNI”
Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, “Je, wewe
si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.” Lakini yule wa pili akamjibu, akamkemea,
akisema, “Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni
haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali
huyu hakutenda lolote lisilofaa.” Kisha akasema, “EeYesu, nikumbuke
utakapoingia katika ufalme wako.” Yesu akamwambia, “Amin, nakuambia, leo hivi
utakuwa pamoja nami mbinguni.” (Luka
23:39-43)
Neno la pili la Yesu msalabani lathibitisha kuwa
msamaha una nguvu kuliko dhambi. Yesu amefundisha juu ya msamaha kwa kuwaombea
msamaha watesi wake. Yesu ameonesha kuwa yeye ni Mungu kwa kutumia tabia kuu ya
Mungu ya kusamehe. Yule mhalifu ametambua kosa lake na amemtambua Yesu kuwa ni
Mungu na akaomba msamaha; Yesu mara moja akamsamehe kwa kumpa nafasi mbinguni.
Leo hii
utakuwa pamoja nami mbinguni: Neno hili
ni habari njema ambayo kila mmoja wetu angefurahi kuambiwa na Yesu. Hapa Yesu
anatufundisha kuwa, Mungu humpa msamaha papo kwa papo mtu yeyote anayeomba
msamaha bila kujali amekosa nini.
Ni dhambi kubwa kuishi na dhambi bila kuomba
msamaha. Kutoomba msamaha kwa Mungu ni dharau kubwa. Yule mhalifu mwingine
alimdharau Mungu na kumtaka amshushe msalabani; kumbe huyu mwingine alimwogopa
Mungu na kuomba msamaha.
Katika neno la kwanza Yesu alifundisha kuwa
jambo la kwanza mbele ya Mungu ni kuomba msamaha. Mhalifu wa kwanza hakuelewa
mafundisho hayo, ndiyo maana badala ya kuomba msamaha akaomba muujiza wa
kushushwa msalabani. Muujiza huo hakuupata kamwe. Kumbe yule mhalifu wa pili
alielewa vema mafundisho ya Yesu pale Msalabani; akaomba msamaha. Huyu alipata
alichokiomba palepale bila kupewa ahadi; Leo
hii utakuwa pamoja nami mbinguni.
Ukombozi ni msamaha wa dhambi zetu na kuingizwa
mbinguni. Ukombozi ni tendo au jambo la leo na sio kesho. Ukombozi hautafutwi
kesho na wala hauombwi kesho. Ukombozi daima ni leo; ndiyo maana Yesu anasema:
Leo utakuwa pamoja nami mbinguni. Yesu hakusema, Ngoja kwanza nifufuke siku ya
tatu nitakukaribisha mbinguni.
Neno LEO katika Injili ya Luka lina maana ya
kufuta yaliyopita na kumwingiza mtu katika maisha mapya.
Yesu alipozaliwa malaika waliwaambia
wachungaji: LEO katika mji wa Daudi, kwa ajili yenu amezaliwa mwokozi ndiye
Kristo Bwana.
Yesu alipoanza kuhubiri nyumbani kwao Nazareth aliwaambia: LEO Maandiko haya
yametimia masikioni mwenu.
Yesu alipokutana na mtu mwenye dhambi aitwaye Zakayo alimwambia: Zakayo shuka
upesi, kwa kuwa LEO imenipasa kushinda nyumbani mwako. Na alipoenda nyumbani
kwa Zakayo alimwambia: LEO wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye
ni mwana wa Ibrahimu.
Na mwisho Yesu alimwambia yule mhalifu aliyeomba msamaha: LEO hii utakuwa
pamoja nami mbinguni.
Kwa hiyo, neno LEO lina maana ya kufuta historia
ya zamani ya dhambi na kumwingiza mtu katika historia mpya ya neema, yaani
uwepo wa Mungu rohoni mwetu. Yesu anatualika mimi na wewe tuingie leo hii
katika historia mpya. Katika ukombozi hakuna neno kesho; ukombozi ni leo.
Anza leo hii kuomba msamaha kwa Mungu. Anza leo
kuomba msamaha kwa wote uliowakosea. Anza leo kuwasamehe wote waliokukusea. Leo
hii, utakuwa mwana wa Mungu na mbinguni ndiko kutakuwa nyumbani kwako milele.
Tunajifunza nini kutoka kwa mwalifu wa Kwanza: Wengi wetu tunaomba Miujiza kwa Mungu pasipo kujipatanisha kwanza na
Mungu, Sala ya kweli ni ile inayotanguliwa na Toba.
Tunajifunza nini kutoka kwa Mwalifu wa Pili: Tujinyenyekeze kwa Mungu na kumkimbilia yeye, Maana maandiko
matakatifu yanasema “Ni Mwingi wa Huruma si mwepesi wa hasira”.
Katika Makala Ijayo
tutatafakari Neno la Tatu la Yesu Akiwa Msalabani….
Ee Yesu tunakuabudu na tunakushukuru; Kwa Kuwa Umewakomboa
Watu kwa Msalaba Wako Mtakatifu.
**********************************************************************
0 blogger-facebook:
Post a Comment