Na. James J. Waibina
Mpendwa msomaji wa Jarida letu
la Fumbuka na BLOG yetu ya Fumbuka kupitia fumbukasasa.blogspot.com, Nichukue
fursa hii ya pekee kukukaribisha kwa mara nyingine katika makala hii ya KIJANA
AMKA.
Baada ya kuangalia Maana ya
Kukata tamaa katika Makala iliyopita, leo tutaangalia dalili za ndani za
mtu aliyekata tamaa hivyo karibu uwe nami ili uweze kujifunza mengi yamkini
nawe umekata tamaa ila hujijui.
Hizi ni dalili ambazo watu
wengine nje ya mhusika hawawezi kuzitambua kiurahisi, ni muhusika tu ndiye
anaweza kuzitambua au kuhisi, Sasa tuziangalie dalili hizi angalau kwa
undani zaidi.
1. Kukosa msukumo kimawazo.
Kwakua kila jambo linaanzia
kwenye mawazo, ili mtu afanikiwe anahitaji msukumo na ushawishi wa mawazo yake.
Maana mawazo anayokuwanayo mtu
kwa muda mrefu, huwa yanajitokeza katika maneno yake na hatimaye katika matendo
yake.
Hivyo basi ukiona msukumo wa
mawazo yako ya mwanzo umepungua, basi ujue kuwa hiyo ni dalili mojawapo ya
kukata tamaa.
2. Kuhisi kuchoshwa kimawazo
Ukiona mawazo yako yamechoshwa
kwa kuliwazia jambo fulani ambalo mwanzoni ulikuwa umelipanga vizuri, nayo ni
dalili ya kukata tamaa.
3. Mawazo ya kushindwa (Hasi)
Haya ni mawazo ambayo siku zote
hayana ushawishi wa kukusaidia kufanya jambo lolote, badala yake huleta woga
kufanya jambo kwa kuhofia kushindwa au kukosa uhakika wa kufikia malengo.
4. Kukosa ubunifu wa njia mbadala
Ukiona jambo linashindikana kwa
njia moja na huku unakosa ubunifu wa njia mbadala jinsi ya kulifanikisha jambo
hilo, nayo inaweza ikawa ni dalili ya kukata tamaa. Kila mtu ana uwezo mkubwa
sana wa ubunifu, tofauti zetu zinajitokeza pale ambapo wengine wanashughulisha
sana sehemu ya ubongo zinazo husika na ubunifu, wakati wengine wamezilemaza.
5. Kupoteza furaha /hamu ya
jambo husika.
Jambo ambalo ulikuwa
unalifurahia na kuliona nzuri, huku ukifikiria kufikia mafanikio, ghafla
unaanza kupoteza furaha au hamu ya jambo hilo, nayo ni moja ya dalili ya kukata
tamaa.
6. Kutofurahia ushauri
Ukiona unaanza kuchukia ushauri
hasa unaokwenda kinyume na mawazo yako au ushauri unaokushawishi kuendelea
kufanya jambo ambalo umeamua kuliacha. Hii inaweza kuwa dalili ya kukata tamaa.
7. Kufanya maamuzi ya haraka
Mawazo yako yanapoamua kufanya
maamuzi yanayohatarisha maafanikio yako, au kuhatarisha maisha yako kama
kujiua, ni dalili tosha ya kukata tamaa.
8. Kupoteza taswira ya mafanikio
Taswira ya mafanikio ndio
msukumo halisi wa kufikia mafanikio. Kupoteza taswira ya mafanikio akilini
mwako, ni dalili ya kukata tamaa.
9. Kupoteza ujasiri
Akili yako inapopoteza ujasiri
juu ya jambo ambalo hapo mwanzo ulikuwa na ujasiri mkubwa wa kulitenda au
kukabiliana nalo, hapo moja kwa moja utakuwa umefikia hatua ya kukata tamaa.
10. Kujihurumia
Hili nalo ni tatizo la ndani ya
mtu, unapoanza kuona akili yako inajihurumia nakuona kama watu au jambo lina
kukosesha furaha ni dalili ya kukata tamaa.
11. Kujihisi hufai kabisa
Unahisi maisha yako hayana jambo
lolote la maaana la kuchangia na hayafai kabisa. Huenda ukahisi unahatia
nyingi. Hii pia ni dalili ya kukata tamaa.
12. Kutamani kufa
Baadhi ya watu hutamani kufa
kuliko kuishi kwasababu ya mambo ya hapa duniani yaliyowaumiza mioyo. Wengine
hutamani kujiua na wengine hufikia hatua ya kumwomba Mungu awachukue kama vile
nabii Elia katika biblia alivyoomba (1wafalme 19:4).
Kwa leo tuishie hapo,
katika Makala ijayo tutazungumzia Dalili za nje za mtu aliyekata tamaa.
******************************************
ITAENDELEA ........
Kwa Maoni /Ushauri: Tuwasiliane
kupitia
0713515059 -(WhatsApp)
au jameswaibina@fumbuka.co.tz
0 blogger-facebook:
Post a Comment