Masomo:-
Somo: Dan 9:4-10
Zab: 79:8, 9, 11, 13
Injili: Lk 6:36-38
Nukuu:
“Rehema na msamaha ni kwa Bwana
wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda
katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake
manabii,” Dan 9:9-10.
“Basi, iweni na huruma, kama Baba
yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi
hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa,” Lk 6:36-37.
TAFAKARI: “Huruma na Msamaha wa Mungu; kwa kuacha
dhambi na kuongoka.”
Wapendwa wana wa Taifa la Mungu,
leo tutafakari juu ya “huruma na msamaha wa Mungu; kwa kuacha dhambi na
kuongoka.” Ndugu yangu, ni ukweli kabisa kwamba hakuna asiye na dhambi. Wate
tuishio katika dunia hii twaitaji neema na huruma ya Mungu kila wakati. Kuishi
katika ukweli huu, yaitaji unyenyekevu mkubwa. Kishawishi kikubwa cha mwanadamu
ni kule kutaka kuwa sawa na Mungu muda wote. Kiburi hiki ni sababu la anguko la
wazazi wetu wa kwanza. Ila kwa neema ya Bwana wetu Yesu Kristu, sote tumepata
uwezekano wa kumrudia Mungu.
Mpendwa, “tukisema kwamba hatuna
dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo wetu,” 1Yoh 1:8. Kuna njia moja
tu ya kumrudia Mungu. Njia hii ni kukiri makosa yako bila kujibakiza. Ndugu
yangu, “tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee
dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote,” 1Yoh 1:9. Jambo hili
linawezekana kwa Mungu kwa sababu yeye ni mwaminifu na “rehema na msamaha ni
kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi,” Dan 9:9.
Kiburi chetu na kukosa unyenyekevu
ndicho Nabii Danieli anatupa angalizo. Nyakati za Nabii Danieli, watu wote
walimwasi Mungu. Kiburi hiki kilikuwa kwa wakuu na wafalme mbele ya uso wa
Mungu. Nabii Danieli kwa niaba ya watu wake anasimama na kusema, “Ee
Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba
zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi.” Dan 9:8. Wapendwa, mahangaiko ya watu na
uovu kuendelea katika jamii yetu leo kwa kiasi kikubwa yanatokana na dhambi za
kila mmoja wetu kadiri azitendavyo, na dhambi ya kijamii-“social sin,” ambayo
kwa kiasi kikubwa hutendwa na watawala wetu kwa nafasi walizokuwa nayo. Jambo
hili lilitokea pia wakati wa Nabii Danieli.
Asiposimama mmoja kati yetu na
kuomba huruma hiyo ya Mungu, kamwe tusitegemee huruma na msamaha wa Mungu.
Tazama taifa letu leo mambo yanavyokwenda. Je, ni mara ngapi, na tena kwa uwazi
kabisa viongozi wetu wanapuuza sauti za waliowaweka madarakani? Tuelewe kabisa
kwamba, sauti ya watu ni sauti ya Mungu. Kwa ukweli wa jambo hili, embu turejee
mchakato mzima wa pendekezo la Katiba mpya kwenye Bunge la katiba. Je, Mungu
kupitia sauti ya watu alisikilizwa na wale tuliowachagua kufanya kazi hiyo? Cha
kushangaza bado tunapambana na Mungu kwa kufanya kila tuwezacho ili mawazo yetu
na tamaa zetu zishinde nguvu ya Mungu. Jambo hili lina hatari kubwa sana kwa
maisha yetu ya usoni.
Nachelea kujiita Nabii, ila
kadiri nionavyo, hatujampa Mungu nafasi ya kutosha hasa kwa jambo hili muhimu
si tu kwa sisi, bali kwa kizazi kijacho. Mungu hata kaa kimya kamwe kuona Taifa
lake linateketea. Watumishi wa Mungu leo hawasikilizwi hata kama wakikemea uovu
huu. Nyakati za Nabii Danieli kadiri ya somo letu la leo hawakusikilizwa
kabisa. Kwa sauti ya unyonge, Nabii Danieli anasema, “tumefanya dhambi,
tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo
yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa
jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na baba zetu,
na watu wote wa nchi,” Dan 9:5-6. Hakika tunaitaji mtu, au nguvu ya kutuvusha
hapa tulipo kama Taifa. Lolote tutakalo tenda kwa sasa bila kusikiliza sauti ya
Mungu, hakutakuwa na baraka yoyote.
Injili yaeleza kwa undani huruma
ya Mungu. Yesu anasema, “Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na
huruma,” Lk 6:36. Huruma anayotutaka Bwana wetu Yesu Kristo tuwe nayo, ni
huruma katika kutenda tukiwa na hofu ya Mungu. Muda tuliokuwa nao sasa baada ya
kutenda dhambi, na wote tukiwa tunaitaji huruma ya Mungu, si muda wa kulaumiana
na kuhukumiana. Yesu anatupa angalizo; “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa;
msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa,” Lk 6:36. Angalizo
hili la Yesu halina maana ya kutowajibika au kutowajibishwa kwa makosa
tunayotenda hasa kwa dhambi ya kijamii-“social sin,” la hasha! Wote wanaohujumu
Taifa hili yawapasa kuona ni kosa na kuchukua hatua. Wasipofanya hivyo, Mungu
mwenyewe atatoa hukumu kwa wakati wake kwa sababu tayari anaona mateso ya watu
wake.
Dhambi ya kijamii ni kupigana na
kushindana na Mungu moja kwa moja kwa kile ulicho, nafasi uliyo nayo, na
mbaya zaidi kama kiongozi. Umekuwa kama ulivyo kwa tokeo la tendo la Mungu. Ni
Mungu aliyekuweka kuwa hivyo kwa niaba yake uwatumikie watu wake. Kwani, “sauti
ya watu ambao wamekuweka madarakani ni sauti ya Mungu.” Wengi wetu jambo hili
hatulijui kiundani, na kama tunalijua tunalichukulia kimzaha mzaha tu bila
umakini na umahiri.
Tendo hili la kupigana na Mungu kwa
uwazi huu, na tena bila kujali na kujirudi, ni kumkufuru Roho Mtakatifu. Dhambi
hii hakuna wa kusamehe. “Bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha
hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele,” Mk 3:29.
Sasa tufanye nini ndugu zangu? Wapendwa,
bila Yesu na kwa msaada wake, hatuwezi kuvuka bonde hili. Tunamwitaji Yesu sasa
zaidi ya kitu kingine unachoweza kufikiri. Kwa sababu, “Mtu huyu Mungu
amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba
na msamaha wa dhambi,” Mdo 5:31. Hakuna njia yeyote tuwezayo kupita isipokuwa
kwa njia ya Yesu Kristo. Hili amelisema mwenyewe Yesu Kristo na siyo mimi
wapendwa. “Yesu akawaambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa
Baba, ila kwa njia ya mimi.” Yoh 14:6. Ni katika Yesu Kristo, “ambaye katika
yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi,” Kol 1:14
Ndugu yangu uliyefuatana nami
katika tafakari hii, ni kazi yako kama mbatizwa na mfuasi hai, wa kweli na
mwakilishi wa kristo pale ulipo, tunaposhika na kufuata ushauri huu wa Mtume
Paulo, "uwafubue macho yao, na kuwagueza waiache giza na kuielekea nuru,
waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa
dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.” Mdo
26:18. Hii ndiyo maana ya kuimarishwa katika sakramenti ya Kipaimara.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na
huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa;
achilieni, nanyi mtaachiliwa,” Lk 6:36-37.
Tusali:-Ee Yesu, tujalie ujasiri wa kuiishi Imani yetu na
kusimama katika kweli yako siku zote za maisha yetu. Amina
0 blogger-facebook:
Post a Comment