Masomo:
Somo I: Kut 17:3-7
Zab: 95:1-2, 6-7, 8-9
Somo II: Rum 5:1-2, 5-8
Injili: Yoh 4:5-42
Nukuu
“Watu wakawa
na kiu huko; nao wakamnung'unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka
Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?” Mwa 17:3
“Bwana
akamwambia Musa, Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli
pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako,
ukaende,” Mwa 17:5
“Akapaita
mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana wa Israeli,
na kwa sababu walimjaribu Bwana, wakisema, Je! Bwana yu kati yetu au sivyo?” Mwa
17:7
“Akaja
mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe,” Yoh 4:7
“Kila anywaye
maji haya ataona kiu tena; walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa
mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake
chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele,” Yoh 4:13-14
“Yule
mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! Baba zetu waliabudu katika
mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo
kuabudia,” Yoh 4:19-20
“Yesu
akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye,” Yoh 4:26
“Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna
nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu,” Rum 5:6
“Bali Mungu aonyesha pendo lake
yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa
tungali wenye dhambi,” Rum 5:8
TAFAKARI: “Mungu
aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili
yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.”
Wapendwa wana
wa Mungu, leo Mama Kanisa anadhimisha Dominika ya “3” ya Kwarema ya mwaka “A”
wa Kanisa. Niwaombe tuzame sote pamoja katika tafakari hii kwa maneno haya
yenye kufunua kweli kuhusu Mungu: -“Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe
kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye
dhambi.” Tendo hili, yaani, ‘upendo huu wa Neno kufanyika mwili na kukaa
kwetu,’ Yoh 1:14, ni dhihirisho la mpango mzima wa Mungu na ulio huru kabisa wa
kuumba ulimwenugu, Isa 45:18, kumuumba mwanadamu, Mwa 1:27, na kumkomboa
mwanadamu aliyelekwisha lemewa na mzigo mzito wa dhambi, Gal 4:4-5.
Hamu hiyo,
shahuku hiyo, chanzo hicho, na vuguvugu hili la upendo ni Mungu mwenyewe, kama
asemavyo huyu Neno aliyefanyika mwili na kukaa kwetu, yaani, Bwana wetu Yesu
Kristo; “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami
nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo
lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Yoh 15:16. Je, ndugu yangu,
ulishawahi kuona ng’ombe aliyeshindwa kuibeba nundu yake hata kama inamkera?
Na huu ndio
wasifu wa Kristo Yesu kama kiongozi na hasa katika fumbo hili zima la upendo wa
Mungu katika historia ya wokovu wa mwanadamu, yaani, “ingawa ni Mwana, alijifunza
kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu
ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii; kisha ametajwa na Mungu kuwa
kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki,” Ebr 5:8-10. Ikiwa Agano Jipya ndio
utimilifu wa Agano la Kale ambalo kwalo limejificha katika Agano Jipya, upendo,
na huruma ya Mungu haujawahi kukoma tangu pale Mungu alipoona inafaa na
kumpendeza kuumba ulimwengu na mwanadamu hadi sasa. Kweli hii inajidhihirisha
katika somo letu la kwanza kama tulivyokwisha lisikia.
Musa kama
Nabii na kiongozi anashiriki sehemu hii maalumu ya historia ya wokovu wa
Mwanadamu kwa upendo na upendeleo wa Mungu kwake. Hata hivyo jambo hili
halikuwa rahisi sana kwake Musa. Ni rahisi kuwaswaga ng’ombe 1000 kichinjioni
kuliko kumpeleka mwalifu mmoja mahabusu. Kwa huyu mmoja, yaani, mwalifu,
unahitaji ulinzi wa hali ya juu, tena akiwa kafungwa pingu. Musa kama Nabii na
kiongozi anapewa wajibu wa kuliongoza Taifa zima la wana wa Israeli na
kulifikisha katika nchi ya ahadi. Haikuwa jambo rahisi kufanya hata kidogo kwa
mwanadamu mwenye nyama na mifupa. Tuelewe watu hawa katika mazingira ya somo la
leo hawakuwa na mwongozo wowote ule (leo tungezungumzia mfano wa Katiba). Amri
zile za Mungu wanakuja kuzipata baadaye, Kut 20:1-26, na Mbao zile mbili za
ushuhuda, Kut 31:1-18, ilhali aliowaacha chini ya mlima walishajifanyia
utaratibu wao (ndama yule wa dhahabu) baada ya yeye, yaani, Musa kuchelewa
kurudi kutoka mlimani, Kut 32:1-6.
Somo hili la
kwanza leo linafunua sifa ya Kiongozi, yaani, pamoja na mambo yote, ‘subira na
utulivu wa ndani’ wenye kupelekea maamuzi yaliyo chanya na yakinifu. Hii ndiyo
busara katika uongozi. Kwa ufupi waswahili wana usemi huu kuhusu sifa hii ya
kiongozi, yaani, “Kiongozi ni jalala.” Je, siyo kwenye jalala kutupwapo kila
aina ya uchafu na yale yasiyofaa tena kwa matumizi? Kwa kuepuka milipuko ya
magonjwa jalala uyabeba yote katika yote. Hivyo Musa anakutana na changamoto
katika uongozi wake, nayo ni changamoto ya kiu. “Watu wakawa na kiu huko; nao
wakamnung'unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi
na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?” Mwa 17:3. Watu hawa hawana maji na
mazingira yale yalikuwa mazingira ya jangwani. Malalamiko ya watu kwa Musa kama
kiongozi, hayarudishi kwa vijembe wala kujihami, ila anasikiliza ‘sauti ya
Mungu’ ndani yake. Hivyo “Bwana akamwambia Musa, Pita mbele ya watu,
ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo
uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako, ukaende,” Mwa 17:5. Mungu anamkumbusa
Musa kutumia ile fimbo aliyompatia. Leo mimi na wewe kama viongozi
tunakumbushwa kutumia vyema ujuzi tulioupata kutokana na elimu tuliopitia,
vipaji na karama tulizo nazo kukabiliana na sintofahamu katika uongozi wetu.
Huku ndiko kupambazuka kutoka kiza kinene kwa tusichokifahamu. Ni jambo la
kusikitisha na kumuhuzunisha Mungu kwamba baadhi yetu huzaliwa, uishi, na kufa
wakiwa wamelala usingizi mzito licha ya elimu, vipaji na karama walizojaliwa na
Mungu.
Mungu
asiyeshindwa lolote kwa wale wenye kumtegemea katika kweli na haki akanena na
Musa na wale wazee; “Tazama, nitasimama mbele yako huko, juu ya lile jabali
katika Horebu; nawe utalipiga jabali, na maji yatatoka, watu wapate kunywa.
Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli,” Mwa 17:6. Hapa tunajifunza sifa
nyingine na kubwa ya kiongozi, yaani, ‘kuwa na hofu ya Mungu,’ na imaanishe
kweli kwamba hofu hiyo ya Mungu imo ndani ya moyo wako kwa namna uonavyo,
ufikirivyo, uamuavyo, na utendavyo. La sivyo mwisho wa uongozi wako moja ya
mambo haya mawili yaweza kutokea, yaani, badala ya kuwa Mhenga kuna nafasi
kubwa sana ya kuwa Lihoka, yaani, roho ile ovu isiyo na chochote cha
kukumbukwa. Musa ni Mhenga wetu kwa sababu katika mapito yale, aliacha kitu cha
kukumbukwa. Na ndivyo ilivyokuwa kwamba baada ya changamoto ile ya kiu, Musa
“akapaita mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana
wa Israeli, na kwa sababu walimjaribu Bwana, wakisema, Je! Bwana yu kati yetu
au sivyo?” Mwa 17:7.
Ndugu yangu
unaye safari name katika tafakari hii, Injili ya leo inafunua na kuficha nguvu
halisi ya Bwana wetu Yesu Kristo kama Masiha, na kiongozi wa kufuatwa katika
safari hii nzima ya wokovu wa mwanadamu, Yoh 14:6. Huu ndio wakati na utimilifu
wa yote, Gal 4:4-5. Katika jambo hili, Kristo anavunja ukimya uliokuwepo kadiri
ya mifumo, mitazamo, mila na desturi zetu ambazo baadhi ya hizo kama zilivyo
hazina uzima ndani yake. Yesu anavunja ukimya huo kwa yale yaliyokuwa
yakiendelea nje ya mila na desturi za watu wake kama Wayahudi kwa mwanamke yule
Msamaria wa Sikari na kumwambia, “Nipe maji ninywe,” Yoh 4:7. Watu hawa
-Wasamaria na Wayahudi- walikuwa na historia zao mbaya ambazo ziliwatenga siku
baada ya siku (kwa leo nisingependa kuzama sana katika jambo hili). Kristo Yesu
leo anavunja pia ukimya ndani ya Taifa lake mwenyewe kama Myahudi. Na hali
ilikuwa hivi; “Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa
akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema
naye?” Yoh 4:27. Ujumbe uliwafikia barabara. Kiu yako na yangu leo ni kuutafuta
uso wa Mungu kwa kuishi vyema na impendezavyo Mungu, hasa upendo ule kwa
jirani. Na katika kiu hii Mtakatifu Agustino wa Hippo anasema, “Mioyo yetu
haitulii hadi hapo itakapo tulia kwako Ee Bwana.” Kristo Yesu ndiye kielelezo
na kitoshelezo cha kiu yetu kwa sababu ni kwake tu ipo Njia, kweli, na Uzima,
Yoh 14:6.
Kristo Yesu
kama mwalimu wetu, anachukuwa nafasi hii kutoa mafundisho/katekesi ya kweli juu
yake mwenyewe, na juu ya ufalme ule wa mbinguni ambao kwa upendo wa Mungu Baba
na kwa wale wote waliouridhia u urithi wao. Tendo hili la Yesu kuomba maji kwa
mwanamke huyu Msamaria ndio mlango wa ufahamu wote kwa yale atakayoyazungumza
juu ya kweli kuhusu Yeye mwenyewe na kila alichokijia kama Masiha. Hata hivyo
kutokkana na mahusiano yasiyo afya kati ya Wasamaria na Wayahudi, kitendo kile
cha Yesu kuomba maji kinamshangaza sana mwanamke yule Msamaria. Naye anahoji,
“Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana
Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.),” Yoh 4:9. Yesu anaanza kuvunja kuta
zile za hofu na ukimya ule wa muda mrefu na kusema, “Kama ungaliijua karama ya
Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye
angalikupa maji yaliyo hai,” Yoh 4:10. Yesu anaondoa hali ile ya kufa na kuleta
uzima. Hii ni moja ya changamoto kubwa leo kuhusu uinjilishaji mpya na katekesi
ya kina kuhusu imani yetu. Hakuna usalama wowote kuendelea kujenga kuta za
utengano. Usalama upo pale tunapozivunja kuta hizo na kujenga mahusiano katika
kweli, uhuru na haki.
Pamoja na
kujifunua kwake Yesu kwa mara ya kwanza kama Masiha, bado somo hili -nipe maji
ninywe- linabaki katika hali ya nadharia kwa mwanamke huyu. Naye anamjibu Yesu
hivi, “Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi
hayo maji yaliyo hai? Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa
kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake?”
Yoh 4:11-12. Ndugu yangu, kila mmoja wetu huwa kile alacho katika maana ya
kwamba, kile ulicho ni tokea la historia yako (mila na desturi ulizokulia).
Yesu anamtoa
mwanamke huyu Msamaria kwenye nadharia na kumpeleka kwenye tendo halisi kuhusu
-“nipe maji ninywe.” Na kweli ya akisemacho Yesu juu ya “nipe maji ninywe ni
hiki:-“Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; walakini ye yote atakayekunywa
maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa
yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele,” Yoh
4:13-14. Kweli ya hiki akisemacho Yesu kinafunua kile alicho, yaani, Masiha, na
kile alichokijia, yaani, Mkombozi wetu. Uwepo wa Yesu kwako na kwangu ni
kuufikia uzima wa milele, na ule ukamilifu wa Mungu, Mt 5:48, ambao bila huo
hatuwezi kumwona Mungu. Ukamilifu huu ni Mtakatifu wako kama cheo chako. Yesu anasema
wazi wazi kile alichokijia. “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi
nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele,” Yoh 10:10.
Mara somo
linaanza kueleweka katika hatua hii ya “tendo”-nipe maji ninywe ingawa
chembechembe za nadharia bado zinamsonga mwanamke huyu. “Yule mwanamke
akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka,” Yoh
4:15. Hata hivyo Yesu anataka kujua kweli iliyopo ndani ya nafsi yetu, kwa
sababu kama kweli hiyo ipo ndani yetu basi tu huru, Yoh 8:32. Hivyo “Yesu
akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa,” Yoh 4:16. Basi “Yule mwanamke
akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume; kwa
maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo
umesema kweli,” Yoh 4:17-18. Mguso wa maneno haya ya kweli juu ya maisha ya
mwanamke huyu Msamaria yanafunua ndani ya moyo wake kile alicho Kristo Yesu.
“Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! Baba zetu waliabudu
katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo
kuabudia,” Yoh 4:19-20.
Ndugu yangu,
hadi hapa Yesu kesha yafanya yote mawili, yaani, kweli ya kile alicho, na kile
alichokijia. Kilicho baki sana ni Yesu kumwonyesha njia ya kufuata ili afike
pale ambapo kila mmoja wetu kwa kuumbwa kwa sura na mfano wake Mungu siyo jambo
la mabati mbaya. Tumeumbwa tuishi milele. “Yesu akamwambia, Mama, unisadiki,
saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.
Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka
kwa Wayahudi. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi
watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao
wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho
na kweli,” Yoh 4:21-24. Kumwabudu Mungu katika roho na kweli ni kujisalimisha
kwa Mungu pasipo kuwa na viambata. Viambata katika imani ni ile michanganyo
isiyoendana na kile alicho Mungu. Ili kupata uhakika wa kile akifanyacho, “Yule
mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye
atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote,” Yoh 4:25. Na Yesu akamaliza
katekesi yake kwa hitimisho hili lenye utoshelevu wote: “Mimi ninayesema nawe,
ndiye,” Yoh 4:26. Ndugu yangu, achia viambata vyako na ambatana na Kristo Yesu.
Kwake upo uzima wa milele.
Ndugu yangu,
furaha ni kama kikohozi huwezi kuizuia. Mara baada ya kupata kitoshelevu cha
kiu yake kwa muda mrefu, “yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake
mjini, akawaambia watu, Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote
niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?” Yoh 4:28-29. Kwa tendo
hili la mwanamke huyu Msamaria tunakumbushwa kushirikishana mambo yale makuu
aliyotutendea Mungu. Wokovu wako uwe faida pia kwa wengine. Na kwa tendo hilo
nawe unakuwa Kristo mwingine pale ulipo.
Kwa upande wa wanafunzi
wa Yesu wanabaki na maswali mengi kichwani mwao. Kwa vile muda ulishakwenda,
wanamsihi Mwalimu wao ale kile walichokwenda kuhemea mjini. Naye “Akawaambia,
Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi. Chakula changu ndicho hiki, niyatende
mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake,” Yoh 4:32, 34. Kwa jibu hili
la Yesu tunajifunza kwamba kiu na furaha ya Mungu ni kukupata wewe na mimi bila
kujipoteza katika haya ya leo na kesho tu. Kuondoa ile sintofahamu kwa
wanafunzi wake na hasa kwa tukio lile la mazungumzo baina yake Yesu na yule
mwanamke Msamaria, Yesu anawaambia upendeleo waliokuwa nao mbele ya Mungu kama
wahudumu, Yoh 4:35-41. Upendeleo huo unao wewe na mimi pia kwa sakramenti ya
ubatizo na kipaimara (uimarisho). Atimaye Yesu anawapata wote, Wasamaria
waliodharaulika na Wayahudi, na Wayahudi walio waliojitenga na Wasamaria kadiri
ya misimamo yao kiimani. Na huu ndio ushuhuda wa Wasamaria juu ya Kristo Yesu:
-“Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako
tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi
wa ulimwengu,” Yoh 4:42.
Wapendwa wana
wa Mungu, somo letu la pili latufundisha kwamba, wewe na mimi leo tunauishi
Utatu huu Mtakatifu na umoja usiogawanyika tunapoambatana pasipo kujipoteza
katika malimwengu tukiwa ndani ya Utatu huu kila mmoja kadiri alivyoitwa
kutumika hapa duniani kama viumbe shirikishwa katika uumbaji wa pili na
Mungu-“co-creators of God.” Hivyo wito na maisha yako unayoyaishi kwa uaminifu
ni kwa namna hiyo hiyo unashiriki fumbo hili Takatifu katika (kuumba, kukomboa,
na kutakatifuza malimwengu). Hapa ndipo twawezwa kuhesabiwa haki katika imani
hiyo. Hivyo “Basi
tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa
njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani
kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la
utukufu wa Mungu,” Rum 5:1-2. Na kuishi Imani hii katika kweli, tumaini na
haki, tunawezeshwa na Roho Mtakatifu tuliyepewa. “Na kazi ya uthabiti wa moyo
ni tumaini;na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha
kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi,” Rum 5:4b-5. Je,
ninalo la kujivunia au kuona fahari juu ya kufunuliwa siri na fumbo hili la
Utatu Mtakatifu na umoja usiogawanyika? Sina!
Ndugu yangu,
lazima uelewe jambo hili, kwamba, “Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati
ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu,” Rum 5:6. Je, mimi nimekamilika?
Kama nimekamilika, je, mazingira yangu na kutenda kwangu kwa watu kuna akisi
upendo huu alionifia Kristo? Ukweli ni kwamba, “Mungu aonyesha pendo lake yeye
mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali
wenye dhambi,” Rum 5:8. Sadaka yangu kila siku ni kuwa mwaminifu pale nilipo,
na kuvuja damu kila siku kwa kujitoa vilivyo kwa kile nikifanyacho kama moja ya
huduma na kuwajibika kwangu. Kutafuta huruma mbele za watu ili kuonekana mwema
ni kupoteza muda na neema ya Mungu ndani yako. Huu ndio mchezo haramu na
usiopendeza mbele ya Mungu unaofanywa na viongozi wetu, hasa wa kisiasa kucheza
na hisia zetu.
Basi nielewa
kwamba pale nilipo na kwa kila mmoja kadiri ya wito na nafasi yake ni kielezo
cha mwanga kama mshumaa. Unapowaka mshumaa na kutoa kile kilicho kama mshumaa
-“kuliondoa giza”- mshumaa haubaki kama ulivyo. Hii ndiyo sadaka ya kila mmoja
wetu anapoishi kila alicho katika kweli na haki. Nilete uhai, furaha,
matumaini, upendo, na amani pale nilipo kama Kristo afanyavyo daima.
Tusifu Yesu
Kristo!
“Mimi
ninayesema nawe, ndiye,” Yoh 4:26.
Tusali:-Ee Yesu
Mwema na Mwalimu wetu, tuondolee woga pasipo woga ili tuweze kuabudu katika
roho na kweli. Amina
0 blogger-facebook:
Post a Comment