SOMO 1
Yer. 7:23-28
Naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni sauti yangu,
nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile
yote nitakayowaamuru, mpate kufanikiwa. Lakini hawakusikiliza, wala kutega
sikio lao, bali walikwenda kw amashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa mioyo
yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele. Tokea siku ile baba zenu walipotoka
katika nchi ya Misri hata leo, nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu
ninyi, nikiamka mapema kila siku na kuwatuma. Lakini hawakunisikiliza, wala
kutega sikio lao; bali walifanya shingo yao kuwa ngumu; walitenda mabaya kuliko
baba zao. Nawe utawaambia maneno hayo yote; lakini hawatakusikiliza; nawe
utawaita; lakini hawatakuitikia. Nawe utawaambia, Taifa hili ndilo
lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu
umepotea, umekatiliwa mbali vinywa vyao.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 95:1-2, 6-9 (K) 7
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu
mioyo yenu.
Njoni, tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi. (K)
Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)
Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba,
Kama siku ya Masa jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)
SHANGILIO
Zab. 51:10, 12
Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Unirudishie furaha ya wokovu
wako.
INJILI
Lk. 11:14-23
Yesu alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule
bubu akanena, makutano wakastaajabu. Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa
Beelzebuli, mkuu wa pepo. Wengine walimjaribu, wakitaka ishara itokayo
mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe
kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa
Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa
ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa
nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo
kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye
nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama;
lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya
silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake.
Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu
asiyekusanya pamoja nami hutapanya.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
0 blogger-facebook:
Post a Comment