728x90 AdSpace

­
Latest News
March 1, 2017

KWARESIMA: Siku 40 za kutembea katika Jangwa la maisha ya kiroho!

Wakati umetimia na ufalme wa Mungu umekaribia, tubuni na kuiamini Injili, (Mk 1:15), haya ndiyo maneno  ya kwanza ya Yesu  ambayo kadri ya Mwinjili Marko  yanafungua kazi ya hadhara ya Yesu, kwa maana hiyo kazi ya  Yesu inaanza  kwa kuwaandaa watu katika toba  ili hatimaye, wapate kuukaribia au kuingia katika ufalme wa Mungu. Na wakati ndiyo sasa. Wakati ni sasa , Yesu anatuhubiria  na Kwaresima imewadia, na ndiyo maana siku ya Jumatano ya majivu,  kwa kuitikia mwito wa maneno ya Yesu kanisa linatualika kuingia katika kipindi cha Kwaresma, ambacho ni kipindi cha kujikusanya, kujitayarisha, kijitengeneza na kujikarabati   hasa kwa toba, kufunga, kusali na kujitoa sadaka zaidi mambo yanayorutubishwa kwa tafakari ya kina ya Neno la Mungu.
Kwaresima ni kipindi  cha siku arobaini  ambacho ni mwaliko wa kusafiri kiroho na Kristo Mwokozi wetu, kama walivyofanya Waisraeli jangwani kwa muda wa miaka arobaini. Katika safari ya Kwaresima, Kanisa  linatuongoza kwa tafakari na mazoezi  yatakayotusaidia kukua zaidi  kiroho na zaidi kukutana  na Kristo mfufuka aliye Jiwe kuu la msingi la Ufalme wa Mungu. Katika Agano la Kale, ilichukuwa taifa la Israel miaka arobaini  kuingia katika Nchi ya ahadi,  hiki kilikuwa ni kipindi kirefu ambacho pamoja na kutawaliwa na matendo makuu ya Mungu, kilitawaliwa pia na vishawishi kiasi hata cha kuwafanya Waisraeli wajisikie mara kadhaa kuiacha safari iliyokuwa inawaelekeza  mbele kwenye nchi ya ahadi.
Pia kilikuwa ni kipindi cha kuterereka na kukataa tamaa hasa pale Waisraeli walipopata shida (kut 14:10-12), mbali na hayo kilikuwa pia ni kipindi kilicho jaa huruma ya Mungu. Katika Agano Jipya, ilimchukuwa Yesu  siku arobaini za kufunga ambamo  ndani yake Yesu anashiriki hali yetu dhaifu akitufundisha na kutuonyesha  njia ya kuvishinda vishawishi, dhambi na nafasi zake. Safari hii ya Yesu ya siku arobaini  ilikuwa ni kielelezo cha kipindi  cha maisha yetu, maisha yaliyojaa raha na karaha, yakidai kupokea hayo yote kwa jicho na uradhi wa moyo  unaongozwa na Imani katika matendo! Hivyo basi, ni matumaini kuwa  pamoja na vikwazo na changamoto  nyingi  tunazozipitia katika safari ya imani, kipindi cha Kwaresma  kinatupatia fursa  ya mazoezi  ya kiroho na tafakari zitakazo saidia kukutana na Kristu mfufuka.
Ikumbukwe kuwa, kuna mambo manne, ambayo yaweza kufanya imani yetu kubakia imara hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima  na wakati wote wa maisha yetu. Nayo ni sala, kufunga, matendo ya huruma na tafakari ya kina ya Neno la Mungu; mambo yote haya huenda sanjari! Kufunga ni roho ya sala, matendo ya huruma ni damu ya kufunga, hivyo sasa kama ukisali, funga na kama ukifunga, onyesha huruma  na kama ukitaka maombi yako yasikilizwe sikiliza maombi ya  wengine, na ndiyo kusema   asiyefunga masikio  yake kwa  wengine, anajifungulia masikio ya Mungu kwake mwenyewe. Ukifunga angalia mfungo wa wengine  pia, na ukitaka Mungu ajue kuwa una njaa basi  nawe tambua kama mwingine au mwenzako ana njaa, na ukitaka huruma onyesha huruma. Hivyo, Kipindi hiki kitupe fursa ya kumjua Mungu zaidi, na hivyo tumwendee Mungu kwa  sala, toba, tafakari ya kina ya Neno la Mungu, matendo ya huruma, kufunga, kuwajali wenzetu na hasa wale wanaoteseka  na wanahitaji.
Chanzo: Radio Vatican.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 blogger-facebook:

Post a Comment

Item Reviewed: KWARESIMA: Siku 40 za kutembea katika Jangwa la maisha ya kiroho! Rating: 5 Reviewed By: Unknown