Waziri Mkuu, mizengo Pinda akizungumza na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (kulia) Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Africa Mashariki (EADB), Vivianne Yeda (kushoto) na Mjumbe wa Bodi ya EADB,Khadija Simba baada ya kufungua Semina ya Wanasheria wa Serikali wa nchi za Afrika ya Mashariki ya kuwajengea uwezo wanasheria hao katika kuchambua na kufikia mamuzi ya mikataba ya uvunaji maliasili za mataifa hayo,. Semina hiyo ilifanyika kwenye hoteli ya White sands jijini Dar es salaam Septemba 9, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewataka wanasheria kutoka nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki waweke mbele maslahi ya wananchi wa kawaida wakati
wanapoingia mikataba na wawekezaji kwenye sekta ya madini.
Ametoa
wito huo leo mchana (Jumanne, Septemba 9, 2014) wakati akifungua semina
ya siku tano juuya mafunzo ya kuingia makubaliano na mikataba kwenye
sekta ya madini kwa wanasheria wa sekta ya umma kutoka nchi wanachama wa
Jumuiya hiyo ulioanza leo kwenye hoteli ya Whitesands jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza
na washirki wa mkutano huo kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na
Tanzania, Waziri Mkuu Pinda alisema wanapaswa wawajali sana wananchi
walio maskini kwa sababu wao hawana fursa ya kuingia kwenye vikao kama
vyao na kutoa sauti juu ya kile wanachokitaka.
“Muwapo
ofisini kwenu au kwenye miji yenu mikuu, mnapojadiliana na wawekezaji
na kufikia makubaliano kuhusu rasilmali za nchi, siku zote muwafikirie
hawa watu wa chini, walio maskini ambao ni wengi na wako nje ya majengo
yenu.”
“Wao
ndiyo wadau wakuu lakini hawana uwezo wa kuingia kwenye vikao kama
hivi, sote tunatambua kwamba wameishi na hizo rasilmali kwa vizazi vingi
tu. Licha ya umaskini wao, wanaishi juu ya ardhi ambayo chini yake kuna
utajiri tele wa madini na rasilmali nyingine. Ninawasihi sana
muwafikirie watu hawa kabla ya kufanya maamuzi yoyote,” alisisitiza
Waziri Mkuu.
Alisema
ili jambo hilo liweze kufanikiwa ni lazima, wanasheria kama wadau wa
mwanzo kabisa, wakubali kukataa pokea fedha chafu na vishawishi kutoka
kwa wawekezaji na siku zote waweke uzalendo mbele kwa maslahi ya nchi
zao.
“Rasilmali
za bara la Afrika hazijaleta maendeleo kwa wakazi wakazi wa bara hili
kwa sababu wanaofaidika ni makampuni makubwa kutoka nje na watu wachache
sana wenye nafasi huku walio wengi wakiambulia patupu. Ni theluthi moja
tu ya mikataba ya uchimbaji madini inayolifaidisha bara zima la Afrika
ikilinganishwa na faida ambayo bara la Amerika Kusini inanufaika nalo.”
Ili
kuepukana na hali hiyo, Waziri Mkuu alisema umefika wakati wa kukataa
kutoa misamaha ya kodi kwa makampuni ya kimataifa na kuhakikisha kuwa
makampuni hayo yanalipa kodi katika kila nchi husika ya Afrika
Mashariki. “Natumaini hii semina itasaidia kutufungua macho katika
maeneo ambayo mikataba yetu na sheria zetu zilikuwa zinalegalega, ili
kuanzia sasa tuweze kunufaika na rasilmali zetu,” alisema.
Alisema
umefika wakati wa kuhakikisha Serikali za nchi husika zinaweka sera
madhubuti na miongozo ya kisheria itakayohakikisha mikataba
inayoandaliwa kwa ajili ya utafutaji na uendelezaji wa madini na
rasilmali zake inazinufaisha nchi kwanza.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu
alisema semina hiyo ni muhimu kwa sababu wanaolengwa ni wanasheria
kutoka Afrika Mashariki na Afrika ndilo eneo pekee lenye rasilmali
ambazo bado hazijaendelezwa.
“Semina
hii imelenga kuwafunua macho wanasheria wetu ili rasilmali zetu ziweze
kuwanufaisha wananchi… ndani ya mikataba tunayoingia kuna mapungufu
makubwa kwa maana ya kuwanufaisha wananchi.”
“Inawataka
watambue kwamba mfanyabiashara yeyote akija ni lazima anatafuta faida.
Na ukilala tu, yeye anapata faida kubwa sana. Wakienda kusaini mikataba
hawa wanasheria wanapaswa kuangalia sheria za nchi husika lakini pia
wanapaswa kuweka uzalendo mbele na kuacha tamaa. Wanatakiwa wafanye
maamuzi kwa niaba ya wananchi,” alisema.
Mapema,
akimkaribisha Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba
alisema sekta ya madini ni mojawapo ya sekta zinazokua kwa haraka sana
hapa nchini lakini inachangia chini ya asilimia moja ya ajira zote
nchini.
KWA HABARI ZAIDI UNGANI NASI KWA KU-LIKE PAGE YETU YA FACEBOOK.. Bonyeza hapa.
0 blogger-facebook:
Post a Comment