Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power
Tanzania Limited (IPTL), imefungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu Kanda ya
Dar es Salaam, wakimtaka Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe awalipe fidia
ya Sh bilioni 500 kutokana na kutoa kashfa dhidi yao.
IPTL, Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Tanzania Limited (PAP)
na Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni hayo mawili, Harbinder Seth wamefungua kesi
dhidi ya Zitto, Mhariri wa gazeti la Raia Mwema, Kampuni ya Raia Mwema na
Kampuni ya Flint Graphics.
Washitakiwa wengine wameshitakiwa kwasababu makala yenye maneno ya kashfa na kuwachafua,
iliyochapishwa Agosti 13 mwaka huu katika ukurasa wa 7 na 14 wa gazeti lao,
ikiwa na kichwa cha habari cha
"Fedha za IPTL ni Mali ya Umma" na Kampuni ya Flint Graphics kwa
kuchapisha gazeti hilo.
Aidha, wanaiomba Mahakama iamuru makala hayo, yalikuwa ya
upotoshaji na kuwachafua kwa kudhamiria,
pia wadaiwa waombe radhi kwa kuchapisha habari ya kuomba msamaha kwenye
kurasa za mbele katika matoleo mawili mfululizo ya gazeti hilo.
Wadaiwa hao waliiomba Mahakama, itoe zuio kwa wadaiwa, watumishi wao,
wafanyakazi, washirika, wawakilishi au watu wengine wanaofanya kazi chini ya
wadaiwa, kuchapisha au kuandika makala
yoyote ya kuwachafua.
Wanadai makala hayo yalikuwa na maneno “kwa mara nyingine Serikali
kupitia viongozi wake akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wamedai kwamba
dola milioni 250 za Kimarekani zilizopaswa kuendelea kuwepo katika akaunti ya
“Tegeta Escrow Account’ si mali ya Serikali na hivyo si mali ya umma….
Akaunti hiyo ilifunguliwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na
Madini, Shirika la Tanesco pamoja na IPTL”.
Ilidaiwa kuwa kabla ya kusambaza habari hizo, wadaiwa walitakiwa kufanya
juhudi za kuthibitisha ukweli kutoka
kwao au kwa maofisa husika wa Serikali, ambao wangethibitisha ukweli kuwa fedha
zilizowekwa kwenye akaunti ya Escrow, zilikuwa ni dola milioni 122 za Kimarekani
na siyo dola milioni 250, kama walivyodai.
Aidha, wangejua fedha ziliwekwa katika makubaliano ya Escrow ;na siyo
kama fedha za umma, lakini ni kutokana na mgogoro wa malipo, yaliyotakiwa
kufanywa na Tanesco kwa IPTL.
Wadai hao walifungua kesi hiyo Septemba 4, mwaka huu kupitia kwa Wakili
Melchisedeck Lutema na Kay Felician Mwesiga.
KWA HABARI ZAIDI UNGANI NASI KWA KU-LIKE PAGE YETU YA FACEBOOK.. Bonyeza hapa.
0 blogger-facebook:
Post a Comment