SERIKALI imekamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza wa nyumba 6,064 za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) zenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 300.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Josephat Musira, alisema kuwa lengo la ujenzi wa nyumba hizo ni kupunguza tatizo la uhaba wa nyumba kwa wanajeshi na watumishi wa wizara hiyo.
Alisema katika fedha hizo, dola milioni 285 ni mkopo wa ujenzi wa nyumba kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia Benki ya Exim.
Meja Musira alisema kiasi kilichobaki cha dola milioni 15 zimetolewa na serikali ili kufanikisha mpango huo.
“Tayari tumekamilisha ujenzi wa nyumba 6,064 katika mikoa tisa hapa nchini, lengo ni kupunguza uhaba wa nyumba kwa wanajeshi,” alisema Meja Musira.
Aliitaja mikoa ambayo tayari nyumba hizo zimekamilika ni Dar es Salaam (2,288), Pwani (840), Arusha (792), Tanga (312), Pemba (320), Morogoro (616), Dodoma (592), Kagera (144) na Kigoma (160).
Alisema nyumba hizo zimejengwa na Kampuni ya Shanghai Construction (Group) General kutoka nchini China.
Meja Musira alisema mkakati ni kujenga nyumba 10,000 katika maeneo tofauti, hali ambayo wanaamini inaweza kupunguza ukubwa wa tatizo la nyumba za wafanyakazi hao.
“Kwa upande wa Dar es Salaam nyumba zimejengwa katika maeneo ya Lugalo, Gongo la Mboto, Ukonga, Kigamboni-Navy, Ubungo Kibangu, Kunduchi KTC, Mbweni JKT na Kimbiji.
“Ni nyumba za kisasa, zimejengwa katika mandhari nzuri, zina kila kitu hadi viwanja vya michezo na barabara, hivyo tunaamini wahusika watazingatia suala la usafi,” alisema.
Alisema uzinduzi wa nyumba hizo unatarajiwa kufanyika wakati wowote kuanzia hivi sasa katika eneo la Gongo la Mboto ambako kuna ghorofa 50 zilizokamilika ambapo Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
KWA HABARI ZAIDI UNGANA NASI KWA KU-LIKE PAGE YETU YA FACEBOOK.. Bonyeza hapa.
0 blogger-facebook:
Post a Comment