KATIKA hali ambayo siyo ya kawaida iliyowashangaza wakazi wa eneo la Ukonga Mazizini kwa Makobe, baba mmoja aliyefahamika kwa jina la Elisha Zakari amedaiwa kumpiga mwanaye wa kumzaa kipigo kama cha ng’ombe machungani na kusababishaazimie na kulazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mtoto Amani Elisha (10) aliyepigwa vibaya na baba yake mzazi hadi kuzimia kwa siku mbili.
Mtoto huyo aliyepigwa ni Amani Elisha (10) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Maarifa iliyoko Ukonga, Dar es Salaam, baada ya kipigo alizimia siku mbili.
Tukio hilo la kikatili lilitokea usiku wa Ijumaa iliyopita na sababu ya mtoto huyo kupewa kipigo inadaiwa ni kutokana na utoro shuleni na kwamba hata akienda huwa haandiki.Waandishi wetu waliponasa tukio walimtafuta mama mzazi wa mwanafunzi huyo maarufu kama mama Amani na mahojiano yakawa hivi:
ALIMPA KICHAPO KIKALI
Mwandishi: Mama ni kweli kuwa mume wako alimpiga mtoto wenu?
Mama Amani: Ni kweli baba yake Amani ndiye aliyempiga.
Mwandishi: Kwani huyu ni baba yake mzazi?
Mama Amani: Ni baba yake mzazi kweli, wakumzaa.
Mwandishi: Wakati mtoto anapigwa wewe ulikuwepo?
Mama Amani: Hapana, sikuwepo nyumbani, nilikuwa kwenye shughuli zangu, niliporudi nikakuta haya. Niliambiwa na majirani kuwa Amani kapigwa na baba yake. Hakukuwa na jinsi, tulimpeleka mtoto hospitali kutibiwa baada ya kuzimia.
Ilidaiwa kuwa baba yake aliamua kumpa adhabu mwanaye baada ya kubaini kuwa alikuwa hafiki shuleni na hata akifika alikuwa haandiki chochote na alipofuatilia, walimu walimthibitishia.
“Ni kweli huyo baba aliwahi kufika hapa shuleni akathibitishiwa kuwa mwanaye ni mtoro na hata akifika ni mvivu kwani haandiki chochote.
“Alipoambiwa hivyo alipatwa na hasira na kutaka kumchapa hapahapa shuleni lakini hatukumruhusu. Tulimuambia kama ni kumchapa akafanye hivyo nyumbani kwake,” alisema mwalimu mmoja kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa shule.
Mtoto Amani Elisha akiwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
JIRANI ASIMULIA
Jirani mmoja aliyeshuhudia kichapo hicho aliwaambia waandishi wetu kuwa Elisha au baba Amani ni jirani yao lakini walishangazwa na kichapo alichokuwa akimpa mtoto wake.
“Alimpiga kwa muda mrefu na hakuna hata jirani aliyetoa msaada, kila mtu aliamua kukaa pembeni huku tukishangaa kipigo alichompa mtoto huyo.
“Mtoto huyo alipigwa hadi kuzimia lakini baadaye alizinduka na mama yake aliporejea, kwa kushirikiana na majirani waliamua kumpeleka hospitali,” alisema shuhuda huyo.
Jirani mwingine ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini aliyeongozana na mama huyo kwenda hospitali, alisema kufuatia hali ya mtoto kuwa mbaya waliambiwa waende polisi wakachukue PF3 ndipo angetibiwa.
WATINGA POLISI
Baada ya kufika katika Kituo cha Polisi cha Stakishari, Ukonga na kutoa taarifa ya tukio hilo waliandikiwa PF3 na kumpeleka Amani Hospitali ya Amana kwa ajili ya matibabu lakini kufuatia hali yake kuwa mbaya alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
AFANYIWA UPASUAJI WA KICHWA
Gazeti hili lilimfuatilia mtoto huyo katika Hospitali ya Muhimbili na kukuta amelazwa wodi A, katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi) akiendelea na matibabu.
“Ni kweli mtoto huyo anapatiwa matibabu na amefanyiwa upasuaji wa kichwa na hali yake inaendelea vizuri,” alisema daktari mmoja ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.
BABA MBARONI
Baba wa Amani anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Stakishari, Ukonga, Dar es Salaam huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.
Gazeti hili linampa pole mtoto Amani na tunamuombea apone haraka ili arejee shuleni kuendelea na masomo pamoja na wenzake.
Source: GPL.
Like Page Yetu Hapa Kuungana Nasi Facebook.
0 blogger-facebook:
Post a Comment