SERIKALI imesema itajitahidi kutenga fedha katika bajeti yake, ambazo
zitatumika kununua dawa za maradhi ya kisukari itakazozigawa bure kwa
wagonjwa.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano
wa pili wa ‘Pan African Diabetic Foot Study Group’ ambao ni wa siku
tatu.
Alisema licha ya dawa za ugonjwa wa kisukari kuwa za gharama kubwa,
upatikanaji wake nao umekuwa wa shida, hivyo kuwasumbua watu wenye
maradhi hayo.
Dk. Rashid, alisema serikali itajitahidi kuweka kliniki za kisukari
katika hospitali za wilaya ili wagonjwa wasihangaike kwenda mbali kupata
huduma katika hospitali za mikoa.
“Serikali imeutambua ugonjwa wa kisukari kama moja ya magonjwa yasiyo ya
kuambukiza, ambayo wagonjwa wake wanapaswa kupewa dawa bure, nia ya
dhati ipo ila fedha bado ndiyo linakuwa tatizo katika kutekeleza nia
hiyo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Pan African Diabetic Foot Study Group, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa mradi wa miguu wa ‘Step by Step’, Dk. Zulfiqarali Abbas,
alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye mzigo mkubwa wa magonjwa ya
kisukari.
“Tanzania ina mzigo mkubwa wa magonjwa yasiyoambukiza, sio tu kisukari
bali na matatizo yanayoambatana na ugonjwa huu kama vile vidonda vya
kisukari miguuni, ambalo ongezeko lake haliwezi kufumbiwa macho,”
alisema Dk. Abbas
0 blogger-facebook:
Post a Comment