MATUMAINI ya Watanzania waishio nje ya nchi kupata uraia pacha yameota
mbawa baada ya serikali kuweka bayana kuna athari kubwa za kiusalama.
Licha ya sababu hiyo ya serikali kutotaka liwemo kwenye Katiba mpya,
suala hilo limewagawa wajumbe wengi wa Bunge Maalum kwa misingi ya
kisiasa na kiuchumi.
Mgawanyiko huo ulijitokeza zaidi katika kamati mbalimbali zilizokuwa
zikijadili Rasimu ya Katiba, kiasi cha kumfanya Mwenyekiti wa Bunge
Maalum, Samuel Sitta, kuunda kamati ya watu 10 kulishughulikia.
Sitta, pia aliagiza watalaamu wa Uhamiaji, watoe semina kwa wajumbe ambayo ilifanyika jana na kuzusha mgawanyiko mkubwa.
Katika semina hiyo, watoa mada walikuwa ni Katibu Mtendaji, Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango, Dk. Philip Mpango na mtendaji mwandamizi kutoka
Idara ya Uhamiaji, waliyopinga Watanzania wenye uraia pacha kushiriki
siasa.
Wataalamu wa uhamiaji, walisema kama Tanzania itaridhia suala hilo litaondoa uzalendo na litahatarisha amani.
Hata hivyo, katika kile kilichowashangaza wajumbe wengi, serikali
haikuwaleta wataalamu wanaohusika na uraia pacha wanaofanya kazi katika
Idara ya Uhamiaji.
Inadaiwa kuwa, hofu ya serikali ni kuwa Mtanzania atakapopewa uraia
pacha, anaweza kufanya uhalifu hapa nchini na kukimbilia nchi nyingine
aliko na uraia wake na hivyo kuweka mazingira magumu ya kumkamata.
Hofu nyingine iliyotolewa na wajumbe wengi hasa wa Zanzibar, ni kuwa
baadhi ya watu waliokimbia hapa nchini wakati wa Mapinduzi mwaka 1964,
wanaweza kurejea na kuchukua uongozi kama uraia pacha utaruhusiwa.
Hata hivyo, Mjumbe wa Bunge hilo anayewakilisha Watanzania walio nje ya
nchi, Kadari Singo, alisema suala la uraia pacha limeshakwama.
Singo, alisema kauli za Makamishna wa Uhamiaji waliotoa mada kwa
wajumbe, inaonyesha serikali haitaki Watanzania kuwa na uraia zaidi ya
nchi moja.
Alisema sababu za kuwa Watanzania walio nje ya nchi wakipewa uraia pacha
hawatakuwa na uzalendo na watahatarisha usalama wa nchi ni nyepesi.
Singo, alisema msimamo huo wa serikali ni mwiba kwa Watanzania waishio
nje ya nchi wapatao milioni moja, waliyotegemea uraia pacha utaingizwa
kwenye Katiba mpya.
Alisema serikali ilifanya hila za kuwatumia makamishna wa Uhamiaji, kwa kueleza hasara za uria pacha bila kueleza faida zake.
“Nimesikitishwa sana na dhamira ya serikali, kwani imetoa mada yenye
mlengo mmoja tu hivyo kuwanyima fursa wajumbe kujua faida za uraia
pacha,” alisema.
Alisema uraia pacha una faida kubwa na nchi nyingi zinanufaika na
utaratibu huo, ambapo fedha zinatoka nje na kuendeleza nchi husika.
Singo, alisema kutokana na hatua hiyo, Watanzania wengi watanyimwa fursa
ya kushiriki kuinua uchumi wa nchi yao kikamilifu, kutokana na
kutotambuliwa kisheria.
Alifafanua kwamba katika nchi za Kenya, Uganda na Rwanda, zinanufaika na
utaratibu huo, ambako raia wake wanaingiza fedha nyingi nchini mwao kwa
ajili ya maendeleo.
Singo, alisema uraia pacha unafungua njia kwa kurejesha rasilimali kwa wingi nchini na kulikomboa Taifa na tatizo la ajira.
Aliongeza kuwa, utafiti usio rasmi unaonyesha Watanzania walio nje wanarejesha nchini kati ya dola milioni 10 na 37 za Marekani.
Alitaja mfano wa manufaa katika nchi nyingine ni China inayonufaika na
dola bilioni 60 za Marekani kutoka nje kila mwaka, Nigeria dola bilioni
20, Kenya inavuna dola bilioni 1.7.
Hata hivyo, alikiri kuwepo utata wa takwimu za Watanzania wanaoishi nje
ya nchi kutofautiana, na kulingana na vyanzo vyake, alifafanua kwamba
Benki ya Dunia inataja wako milioni 3, mwenyewe Singo, alikadiria kati
ya milioni 1 na milioni 1.5.
Aliongeza kuwa Tanzania ni kati ya nchi nane pekee za barani Afrika
ambazo hazijaingia katika mfumo wa uraia pacha, lakini inaathirika
kupitia kuwapa uraia watu kutoka nchi nyingine zenye mfumo huo, akitoa
mfano wa Rwanda.
Alisema kama ni dhana ya uzalendo iwapo inapatikana kwenye tabia binafsi
ya mtu au mahali atokapo, akieleza imani yake ni kwamba tabia binafsi
inatathimini uzalendo na si vinginevyo.
Singo, alishauri pamoja na kuwepo mifumo mingi ya uraia pacha, Tanzania
bado inaweza kubuni mfumo unaoendana na mazingira yake ili kuwa na
unaoendana na mazingira yake.
Source: MTANZANIA
0 blogger-facebook:
Post a Comment