Mwamini mwana wa Mungu Tumsifu Yesu Kristo.... Tunakuleteni tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 21 mwaka A tukiongozwa na Nabii Isaya, Mtume Paulo na Mwinjili Matayo, ambao wanatuambia kuwa imani thabiti katika Yesu Kristo Mwana wa Mungu ni msingi wa wokovu wetu.
Nabii Isaya katika somo la kwanza anatoa mafundisho yake wakati wa utawala wa Hezekia, yaani wakati wa utawala huu aliyekuwa mtunza mfuko anatumia vibaya mali aliyokabidhiwa yaani hajali shida za watu. Anajitazama yeye binafsi, anajiimarisha katika utajiri binafsi na anakuza jina lake.
Ni kwa shida hii Nabii Isaya anafundisha kinyume na madhulumu yanayofanywa na wenye madaraka. Anawaambia kuwa watanyanganywa funguo na watakabidhiwa wengine wenye kushika sheria ya Bwana. Funguo ni alama ya madaraka, ni alama ya utawala na hivi nabii anawaambia kuwa madaraka yenu yatapokonywa na Mungu. Mpendwa msikilizaji, ndiyo kusema hivi leo kuna wenye mamlaka wengi ambao wamejiimarisha katika mali, katika ubaya, kiasi kwamba wanapopita mitaani petu wanajionesha katika sura hiyo! Wanatoa harufu ya dhuluma.
Nabii anawaonya kuacha mali hizo na kumrudia Bwana. Hata hivyo tukumbuke kuwa Mungu hachukizwi na mali bali na tunaweza kuwa na mali na madaraka halali kama vitu hivi vinatupatia nafasi ya kuwaongoza wengine vema tukiwajalia haki na ustawi wa maisha yao.
Mtume Paulo anatualika kutambua mara na kuacha ubaya tukiongozwa na hekima ya Mungu ambayo inapita ufahamu wa kibinadamu. Kwa jinsi hiyo hatuna budi kuitafuta na kuipokea hekima ya Mungu ili itusaidie katika kutawala taifa la Mungu na mali tulizokabidhiwa na Mungu mwenyewe. Mtakatifu Paulo anazidi kutuambia jinsi hekima ya Mungu ilivyo ya ajabu ya kwamba katika ubaya wa Wayahudi yaani wanapomkataa Masiha, mara moja milango inafunguka kwa ajili ya mataifa ndiyo sisi! Hakika hekima yake haichunguziki, hatuna uwezo wa kuielewa vema kumbe yafaa kusadiki na kujiweka katika maongozi ya Mungu. Ndiyo kusema katika udhaifu wetu Mungu aweza kuibua jambo la ajabu kwa ajili ya wokovu wetu.
Mwinjili Mathayo anatuletea Kristu aliye katika harakati za uchungaji, yuko Kaisaria Filipi, yuko katika kutekeleza utume wake uliomleta duniani. Huko anataka kuhakiki kama watu na mitume wanamfahamu kina au bado. Anaweka swali mbele ya mitume, Je watu wasema mimi ni nani? Na ninyi mwasema mimi ni nani? Jibu toka jumuiya ya watu ni kwamba Yesu ni mmojawapo wa manabii, ni Ni nabii Eliya, ni Yohane Mbatizaji na mwishoni jibu la Mitume linatolewa na Mtakatifu Petro akisema “wewe ndiye Kristo, mwana wa Mungu aliye hai” Jibu hili la Mtakatifu Petro ndilo linabeba kiini cha injili, ni ufunuo wa Masiya mpakwa mafuta wa Bwana.
Kwa njia ya jibu hili mwinjili Mathayo anataka watu wote wamjue Kristo kama masiya na hakuna tena mfalme mwingine zaidi yake. Watu walitoa jibu kuwa ni nabii lakini sasa mwinjili anatuambia wakati wa manabii umekwisha na hivi ni Kristo pekee mwana wa Mungu aliye hai. Mpendwa hivi leo ukiulizwa Yesu ni nani utasema nini? Kwangu mimi Kristu ni mkombozi wa maisha yangu anayenipenda katika udhaifu wangu, anayeniita kila siku kutubu na kumrudia yeye kwa njia ya kitubio. Ni yule anayewapenda wote bila ubaguzi maskini kwa matajiri.
Tupige hatua kidogo mbele katika tafakari yetu tuone je jibu la Mt Petro linaishia pale tu au lina matunda? Jibu la Mtakatifu Petro lina matokeo makubwa mno, Mtakatifu Petro atakuwa mwamba ambapo Kanisa la Kristu litajengwa. Na si mwamba tu bali ni mwamba wa kujengea, ni mwamba wa imani. Makatifut Petro amekiri imani ambayo lazima ikue na izae matunda. Mwamba huu ni imara na hivi hata nguvu za kuzimu haziwezi kuubomoa. Anakabidhiwa funguo ambazo tulisikia Nabii Isaya akizungumzia kwamba mtunza hazina atanyanganywa na Bwana. Tunarudia tena kusema kuwa funguo ni alama ya madaraka, uwezo juu ya taifa la Mungu.
Oneni mpendwa, ni mamlaka gani Mtakatifu Petro amepewa ili ailinde imani! Asimamie Kanisa, afundishe, aonye na zaidi aimarishe imani ya waamini wote wa taifa la Mungu. Leo hii wajibu huu anao Baba Mtakatifu, Khalifa wa Mtakatifu Petro, Askofu wa Roma na mchungaji mkuu wa Kanisa lote la ulimwengu. Tunao wajibu wa kumwombea ili imani yake ibaki imara na abaki katika kuhudumu na kusimamia taifa takatifu la Mungu akijiimarisha katika imani na umisionari.
Tumsifu Yesu Kristo.
TAFADHALI MUWE MNAANDIKA NA MISTARI YA VITABU KWA AJILI YA REJEA (REFERENCE)
ReplyDelete