UNAPOJIANGALIA kwenye kioo,
wewe hutazama nini?
Labda wewe hutazama nywele zako
au sehemu nyingine ya uso wako. Lakini namna gani meno yako? Je, umetambua
kwamba jinsi ambavyo wewe hutabasamu hutegemea hasa meno yako? Naam, ikiwa
unajali tabasamu yako, utatunza meno yako.
Meno ya mtu mzima yanapaswa kudumu
muda wote wa maisha yake. Yanapaswa kutunzwa vizuri. Mbali na kutafuna chakula
na kukusaidia kuzungumza kwa njia nzuri, meno yako hutegemeza midomo na mashavu
yako na hivyo kuboresha tabasamu yako na kuifanya ivutie. Kwa kweli, meno yako
ni muhimu sana!
UNAWEZA KUTUNZAJE MENO YAKO?
Meno yenye afya hutegemea chakula
unachokula. Lishe bora yenye kalisiam na vitamini A, C, na D
husaidia meno yakue tangu wakati mtu anapokuwa tumboni hadi meno yanapokomaa.
Kula chakula kinachofaa kutakusaidia uwe na meno yenye afya, lakini jihadhari
na vyakula vyenye sukari nyingi!
Vitafanya iwe rahisi zaidi meno kuoza.
Licha ya maonyo mengi yanayotolewa kuhusu jinsi vyakula vyenye sukari vinavyochangia
kuoza kwa meno, inasemekana kwamba mkaaji wa Amerika Kaskazini hula
kilo 50 hadi 60 za sukari kila mwaka!
KWA NINI SUKARI INAWEZA KUHARIBU MENO YETU?
Kuoza kwa meno husababishwa na aina
mbili za bakteria, yaani, “streptococci na lactobocilli” ambazo
hutokeza ukoga, ambao ni utando mwembamba wa bakteria na mabaki ya chakula
ambayo hukwama kwenye meno. Bakteria hizo hula sukari na kuigeuza kuwa asidi
zinazodhuru ambazo hufanya meno yaoze. Aina fulani za sukari hugeuzwa haraka
kuwa asidi au hukwama kwenye meno kwa urahisi, na hivyo kuzipa bakteria hizo
muda wa kufanya meno yaoze.Ukoga ambao hauondolewi unaweza kuwa mgumu kuzunguka
fizi.
Kudhibiti ukoga na hasa bakteria za streptococci
ni muhimu ili kuzuia meno yasioze. Kwa hiyo, ikiwa ungependa kutunza meno yako,
ni lazima usafishe kinywa chako kila siku. Chuo Kikuu cha
Upasuaji wa Meno na Kinywa huko Columbia kinasema hivi:
“Kuondoa uchafu katikati ya meno kwa kutumia uzi
mwembamba pamoja na [kupiga mswaki] ndiyo njia muhimu zaidi ya
kudumisha afya ya meno yako na
sehemu nyingine zinazoyashikilia.” Picha kwenye ukurasa huu na unaofuata
inaonyesha njia moja inayofaa ya kupiga mswaki na kuondoa
uchafu katikati ya meno. Daktari wa meno anaweza
kupendekeza vifaa na mbinu nyingine ambazo zitakusaidia kusafisha na hivyo
kutunza meno yako ifaavyo.
Jino linaposhambuliwa mara nyingi na
asidi, madini huondolewa na kunakuwa na matundu madogo sana kwenye tabaka ngumu
ya juu ya meno. Hata hivyo, kila siku madini hayo hurudishwa tena. Jinsi gani?
Imethibitishwa kwamba floraidi hutumika kuzuia kuoza kwa meno kwa kusaidia
kurudisha madini yaliyoondolewa. Kwa hiyo, ingawa kuoza kunaweza kuenea katika
sehemu nyingine za meno, jambo hilo linaweza kuzuiwa na vitu, kama vile
floraidi. Naam, meno yanaweza kujiponya!
UTAZAMIE NINI UNAPOENDA KWA DAKTARI WA
MENO?
Katika uchunguzi ambao watu waliulizwa
wao huogopa nini zaidi, woga wa kwenda kwa daktari wa meno ulichukua nafasi ya
pili baada ya woga wa kuzungumza mbele ya umati. Je, inafaa kuwa na woga huo?
Katika nchi tajiri, kekee, au mashini ndogo inayozunguka kwa kasi, na dawa za
kutia ganzi za kujipaka na za sindano huwasaidia madaktari wa meno kufanya kazi
nyingi bila kumfanya mgonjwa ahisi uchungu mwingi. Kufahamu kinachohusika
katika kila hatua ya matibabu kunaweza kupunguza woga wako.
Unapoenda kwa daktari wa meno, huenda
akasafisha au kukwangua meno yako. Anapofanya hivyo, ukoga huondolewa kwenye
sehemu zisizoweza kufikika kwa mswaki na nyuzi. Meno husafishwa na kung’arishwa
ili kuzuia ukoga na kuondoa madoa ambayo huharibu tabasamu yako.
Imegunduliwa kwamba madini ya floraidi
hupunguza hatari ya kuoza kwa meno, na katika nchi nyingi, mara nyingi
madaktari wa meno hupaka madini hayo kwenye meno ya watoto. Katika nchi nyingi
pia, madini ya floraidi hutiwa katika maji, na mara nyingi dawa za meno
huongezwa floraidi ili kuzuia meno yasioze.
DAKTARI WA MENO ANAWEZA KUFANYA NINI?
Madaktari wa meno wanazidi kuzoezwa
mbinu za kuzuia kuharibika kwa meno madini yanapoondolewa. Mara nyingi kuoza
kwa meno kunaweza kuzuiwa kwa kuziba matundu yanapokuwa bado madogo sana. Kwa
hiyo, unapoenda kwa daktari wa meno mapema, unaweza kufurahia matibabu ya meno.
Hata hivyo, asidi inayotokezwa na ukoga
ikibaki kwenye meno, meno huanza kuoza. Meno hayo yasipotibiwa, huenda yakawa
na matundu. Jino lililo na tundu litahitaji kutibiwa. Ikiwa halijaoza hadi
sehemu zenye neva, basi kwa kawaida sehemu iliyooza huondolewa na tundu
kuzibwa.
Daktari hutumia kekee kuondoa sehemu
iliyooza na kusafisha tundu hilo kisha huliziba. Mchanganyiko wa madini ya
zebaki, fedha, na bati unaotumiwa kuziba matundu ya meno huwa mgumu haraka na
hushindiliwa ili uenee kwenye tundu lote. Michanganyiko mingine hufanywa iwe
migumu kwa kutumia mashini ndogo inayotoa nuru ya buluu. Matundu yasipotibiwa
na sehemu zenye neva zianze kuoza, huenda mizizi ikahitaji kuondolewa au hata
jino kung’olewa. Kuondolewa kwa mizizi kunaweza kuzuia jino lising’olewe, kwani
matibabu hayo huhusisha kujaza na kuziba sehemu ya ndani ya jino. Sehemu ya juu
ya meno yaliyoharibika sana hufunikwa kwa vifuniko, au meno bandia yanaweza
kutumiwa jino linapong’olewa.
KWA NINI INAFAA KUMWONA DAKTARI WA
MENO?
Labda bado unaogopa kumwona daktari wa
meno. Ikiwa ndivyo, mweleze daktari wa meno wasiwasi wako. Kabla ya matibabu
kuanza, kubalianeni ishara utakayotoa (kama vile kuinua mkono) unapohisi
uchungu. Mwombe akueleze kinachohusika katika kila hatua ya matibabu.
Unaweza
kumsaidia mtoto wako awe na meno yenye afya kwa kuwasifu madaktari wa meno na
anapokosea, usitishe kumwadhibu kwa kumpeleka kwa daktari wa meno.
Dakt. Daniel Kandelman, profesa wa
Idara ya Afya ya
Kinywa katika Chuo Kikuu cha Montreal, anasema hivi:
“Siku hizi inawezekana kufikia mradi huu wa afya ya meno: tunza meno yako ya asili,
utakuwa na tabasamu yenye kuvutia maisha yako yote.” Kufanya hivyo kuna
manufaa!
Jino lililokomaa kabisa huonyesha
chakula ambacho mama alikuwa akila alipokuwa mjamzito na wakati mtoto alipokuwa
mchanga meno yakikua ndani ya fizi. Hatua ya ukuzi hukoma mtoto anapokuwa
tineja au anapofikia umri wa miaka ishirini na kitu.
Wataalamu wa meno wamegundua kwamba
sukari ya asili inayoitwa xylitol, imesaidia kudhibiti ukoga unaofanya
meno yaoze. Chingamu fulani zina sukari hiyo ya xylitol.
JINSI YA KUPIGA MSWAKI
Kuna njia mbalimbali za
kupiga mswaki lakini uwe mwangalifu, tumia tu kiasi kidogo cha dawa ya meno.
Dawa ya meno hukwaruza na inaweza kuwa “ngumu mara nyingi zaidi kuliko jino.”
1. Pinda mswaki kidogo
kutoka kwenye mwisho wa fizi. Kwa utaratibu, piga mswaki kutoka kwenye fizi
kwenda chini. Hakikisha kwamba umepiga mswaki sehemu zote za
meno, ndani na nje.
2. Piga mswaki polepole
kwenye sehemu za meno za kutafunia.
3. Ili usafishe sehemu ya
ndani ya meno ya mbele, shikilia mswaki wima. Piga mswaki kutoka kwenye fizi
hadi kwenye sehemu ya kutafunia.
4. Piga ulimi mswaki na
sehemu ya juu ya kinywa.
KUTOA UCHAFU KATIKATI YA MENO KWA
UZI MWEMBAMBA
Madaktari wa meno
hupendekeza kwamba mtu atoe uchafu katikati ya meno kwa kutumia uzi kila siku
na apige mswaki kila baada ya kula.
1. Zungusha uzi kwenye
kidole cha katikati cha kila mkono, na uache sehemu ndogo ya uzi katikati ya
vidole hivyo.
2. Kwa kutumia kidole cha
gumba cha mkono mmoja na kidole cha shahada cha mkono ule mwingine, shikilia
uzi kwa nguvu. Fanya ni kana kwamba unausugua uzi huo katikati ya meno ili
uweze kupita.
3. Pinda uzi huo katika
umbo la C, na kuuvuta juu na chini ili usafishe pande za kila jino.
Pitisha uzi taratibu chini ya fizi, lakini usifinye uzi wenyewe kwenye fizi
wala usiuvute karibu na fizi.
Chanzo:
The Columbia University
School of Dental and Oral Surgery’s Guide
to Family Dental Care
0 blogger-facebook:
Post a Comment