728x90 AdSpace

­
Latest News
August 25, 2014

KWA WANAFUNZI: Zifahamu Hatua 10 za kujiandaa na mitihani

Katika uchunguzi wetu tumebaini kuwa ni wanafunzi wachache ambao hutoka katika vyumba vya mtihani na jibu la uhakika kuwa wamefaulu au wamefeli mitihani yao, hii ikiwa na maana kuwa wengi wao huwa hawafahamu kama majibu walioandika ni sahihi au la, na hivyo kudhani kuwa wasahihishaji wanaweza kuwa na jipya zaidi ya kuwapa mavuno ya kile walichopanda.

 Kutapatapa huku kwa majibu hakuna maana nyingine zaidi ya kuutambulisha uwezo duni wa mwanafunzi husika kuwa alipoingia hadi anatoka kwenye chumba cha mtihani hakuwa anajua alichojifunza kabla, alicholetewa kwenye mtihani na alichojibu, ndiyo maana amekosa jibu la uhakika. 

 Lakini kama angefahamu alichojifunza, kilichotokea na alichojibu, moja kwa moja angeweza kuwaambia wazazi na walezi wake kuwa hakufanya vizuri mtihani wake na hivyo kutupilia mbali subira ya bahati, ambayo katika masomo haipo kwa vile apandacho mtu ndicho avunacho.

 Baada ya kusema haya ni vema sasa tukajifunza mbinu za kufanya ili mwanafunzi aweze kufanya mtihani wake vema na kufaulu kwa alama za juu. 

 Kwanza ni muda, wanafunzi wengi huwa hawafahamu matayarisho ya mitihani yanahitaji muda gani kuyakamilisha, hivyo hukurupuka wakati mitihani ikiwa karibu au kujisumbua kwa muda usiotimilifu na kujikuta wamepoteza shauku na kukata tamaa.

 Kifupi mwanzo wa mwanafunzi kufanya vibaya kwenye mitihani yake huanzia kwenye kupanga muda wake na kuutumia.
 Kwenye kipengele hiki kuna makundi matatu ambayo ni ya wale wanaouchezea muda wote, wanaoutumia kwa kuwahi na wanaoutumia kwa kuchelewa huku kiini kikubwa cha tatizo kikiwa ni kwa mwanafunzi kutokujitambua uwezo wake.

 Kujitambua uwezo ni suala muhimu, ambalo linaweza kumfanya mwanafunzi akaamua ni muda gani anaohitaji kufanya maandalizi ya mitihani wake. Hii ikiwa na maana kuwa si wanafunzi wote wanahitaji muda mwingi kujiandaa kutokana na wepesi wao wa kumbukumbu, vilevile si wote wanaohitaji muda mchache kwa maana ile ile ya uwezo wao binafsi.

 Hivyo basi, ni wajibu wa mwanafunzi kujiuliza anahitaji muda gani kukamilisha maandalizi yake kabla hajaingia kwenye chumba cha mtihani?
 Swali hili lazima liende sambamba na vitu gani ambavyo anadhani ni muhimu kuvisoma, kuvielewa kabla ya siku yake ya kutahiniwa.

 Ikiwa ni topic, lazima mwanafunzi ajiulize ni ngapi ambazo hajazielewa, na je itamchukua muda gani kuzimaliza? Ikiwa jibu atakalopata litakuwa ni miezi sita, muda huo lazima utumike kwa kukamilisha malengo ya kuzielewa topic hizo bila kukwama.
 Kama muda utamalizika bila mipango kutimizwa, kuna hatari kwa mwanafunzi kuingia kwenye chumba cha mtihani akiwa na viporo vya mada asizozifahamu, jambo ambalo ni hatari kwake endapo atakutana na maswali kutoka kwenye mada hizo.

 Mbali na hayo mwanafunzi ambaye anataka kupata alama za juu katika mtihani wake lazima awe mtu wa kujiandaa kila siku kwa kutumia dondoo zifuatazo ili kujihakikishia uwezo wa kufaulu na kuepukana na dhana ya kuishi kwa kutegemea bahati.

 KWANZA: Kama nilivyosema hapo juu jambo la kwanza ni kuzingatia muda, si vema kukurupuka na kukimbizana nao na kujinyima usingizi wakati ratiba ya mtihani ilikuwa inafahamika na muhusika alikuwa na uwezo wa kujiandaa taratibu kuelekea kwenye siku ya kutahiniwa kwake. 

 PILI: Jindae mwenyewe kwa kutafuta na kufanya mitihani iliyopita, huku ukinakili maswali ambayo watunzi wamekuwa wakiyarudia rudia kila mwaka.
 Njia hii itakuwezesha kujiandaa kwa kuzingatia shabaha na mahitaji halisi ya maswali yatokayo mara nyingi kwenye mitihani.  Hakikisha unapata mitihani ya nyuma ya ngazi uliyopo isiyopungua kumi au zaidi na uifanye huku ukihakikisha hakuna swali hata moja ambalo linakushinda.
 Pamoja na ukweli kwamba ubahatishaji wa vitu si njia sahihi sana, lakini umeonekana kuwasaidia wale ambao ubahatishaji wao huambatana na umakini, hivyo mwanafunzi anatakiwa kuwa na tabia ya kubahatisha maswali ambayo anadhani mwalimu wake anaweza kuyatoa kutoka kwenye daftari lake na hivyo kujiandaa.
 Ubahatishaji huu, lazima uambane na kile nilichosema awali, yaani  kuwa na kumbukumbu ya mitihani iliyopita. Wanasema watalaamu kuwa ulimwengu una tabia ya kurudia matukio, hivyo hata kwenye maswali kuna tabia hii ya kujirudia rudia.

 TATU: Orodhesha maeneo yote ambayo huyaelewi kwenye mtihani hiyo ya nyuma na uyafanyie mazoezi kwa kupata ushauri kwa waalimu wako. Kama kuna mada ambazo hujazielewa kwenye daftari lako hakikisha muda uliojiwekea utatosha kuzielewa.

 NNE: Hakikisha unajizoeza kufanya mitihani ya majaribio  mara kwa mara, ambayo utaifanya kwa kuzingatia muda na masharti yote ambayo hutolewa siku ya kufanya mtihani halisi. Haifai mwanafunzi kukimbia majaribio yanayotolewa darasani na mwalimu wake, kwani hayo ndiyo yatamuwezesha kufahamu kama amekamilika kwa kutahiniwa au bado kuna eneo linamtatiza.

  TANO: Hakikisha kuwa kumbukumbu zako kichwani zinaongezeka kadiri unavyojifunza, usiwe mtu wa kusahau sahau uliyojifunza na ikiwezekana eneo ambalo unaonekana kulisahau ndilo ulipe kipaumbele cha kujikumbusha, ikibidi hata kila siku.

 SITA: Angalia kwa makini alama zako za mitihani ya majaribio, ikiwa unapata alama za chini ujue kuna mahali panahitaji nguvu za ziada, shauriana na mwalimu wako maeneo yote unayokosa au yanayokusumbua kabla ya siku ya mtihani.

 SABA: Ili mwanafunzi awe na uhakika wa kufanya vema mtihani wake anatakiwa kuzingatia dondoo zote zilizotolewa kwenye kipengele cha kuimarisha kumbukumbu kichwani, ambazo zimo ndani ya kitabu hiki.

   NANE: Wakati mwingine ni vema ukausikiliza mwili, si vema kuulazimisha kusoma hata kama unaona kuna udhaifu, baadhi ya wanafunzi hukesha wiki mbili mfululizo wakisoma, matokeo yake mwili na akili huchoka na kushindwa kupokea masomo vizuri. Muda wa kupumzika unahitajika.

 TISA: Kabla mwanafunzi hajaingia katika chumba cha mtihani anatakiwa kujiamini kwa kushinda hofu. Eneo hili ni muhimu sana kwani kuna wanafunzi hufeli si kwa sababu hawakujiandaa, bali hukumbwa na hofu muda mfupi kabla ya kuanza mtihani. Hivyo ni muhimu mwanafunzi akaandaliwa kisaikolojia na waalimu pamoja na wazazi wake jinsi atakavyoweza kufanya mtihani bila hofu.

 KUMI: Imani ni hitimisho la mafanikio ya mwanafunzi, haifai kuingia katika chumba cha mtihani ukiwa na mawazo hasi. Kinachotakiwa ni ari ya ushindi au kwa lugha nyingine ni mawazo chanya. “LAZIMA NIFAULU MTIHANI HUU” Imani hii inaweza kujengwa na mtu kupitia kujiamini mwenyewe au kuamini kwa msaada wa nguvu za imani yake ya dini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 blogger-facebook:

Post a Comment

Item Reviewed: KWA WANAFUNZI: Zifahamu Hatua 10 za kujiandaa na mitihani Rating: 5 Reviewed By: Unknown