728x90 AdSpace

­
Latest News
March 18, 2017

TAFAKARI YA SIKU: Dominika ya 3 ya Kwaresima Mwaka A Tarehe 19/03/2017


Masomo:

     Somo I: Kut 17:3-7

     Zab: 95:1-2, 6-7, 8-9

     Somo II: Rum 5:1-2, 5-8

     Injili: Yoh 4:5-42

Nukuu

“Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung'unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?” Mwa 17:3

“Bwana akamwambia Musa, Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako, ukaende,” Mwa 17:5

“Akapaita mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana wa Israeli, na kwa sababu walimjaribu Bwana, wakisema, Je! Bwana yu kati yetu au sivyo?” Mwa 17:7

“Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe,” Yoh 4:7

“Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele,” Yoh 4:13-14

 “Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia,” Yoh 4:19-20

“Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye,” Yoh 4:26

“Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu,” Rum 5:6

“Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi,” Rum 5:8

TAFAKARI: “Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anadhimisha Dominika ya “3” ya Kwarema ya mwaka “A” wa Kanisa. Niwaombe tuzame sote pamoja katika tafakari hii kwa maneno haya yenye kufunua kweli kuhusu Mungu: -“Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.” Tendo hili, yaani, ‘upendo huu wa Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu,’ Yoh 1:14, ni dhihirisho la mpango mzima wa Mungu na ulio huru kabisa wa kuumba ulimwenugu, Isa 45:18, kumuumba mwanadamu, Mwa 1:27, na kumkomboa mwanadamu aliyelekwisha lemewa na mzigo mzito wa dhambi, Gal 4:4-5.

Hamu hiyo, shahuku hiyo, chanzo hicho, na vuguvugu hili la upendo ni Mungu mwenyewe, kama asemavyo huyu Neno aliyefanyika mwili na kukaa kwetu, yaani, Bwana wetu Yesu Kristo; “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Yoh 15:16. Je, ndugu yangu, ulishawahi kuona ng’ombe aliyeshindwa kuibeba nundu yake hata kama inamkera?

Na huu ndio wasifu wa Kristo Yesu kama kiongozi na hasa katika fumbo hili zima la upendo wa Mungu katika historia ya wokovu wa mwanadamu, yaani, “ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii; kisha ametajwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki,” Ebr 5:8-10. Ikiwa Agano Jipya ndio utimilifu wa Agano la Kale ambalo kwalo limejificha katika Agano Jipya, upendo, na huruma ya Mungu haujawahi kukoma tangu pale Mungu alipoona inafaa na kumpendeza kuumba ulimwengu na mwanadamu hadi sasa. Kweli hii inajidhihirisha katika somo letu la kwanza kama tulivyokwisha lisikia.

Musa kama Nabii na kiongozi anashiriki sehemu hii maalumu ya historia ya wokovu wa Mwanadamu kwa upendo na upendeleo wa Mungu kwake. Hata hivyo jambo hili halikuwa rahisi sana kwake Musa. Ni rahisi kuwaswaga ng’ombe 1000 kichinjioni kuliko kumpeleka mwalifu mmoja mahabusu. Kwa huyu mmoja, yaani, mwalifu, unahitaji ulinzi wa hali ya juu, tena akiwa kafungwa pingu. Musa kama Nabii na kiongozi anapewa wajibu wa kuliongoza Taifa zima la wana wa Israeli na kulifikisha katika nchi ya ahadi. Haikuwa jambo rahisi kufanya hata kidogo kwa mwanadamu mwenye nyama na mifupa. Tuelewe watu hawa katika mazingira ya somo la leo hawakuwa na mwongozo wowote ule (leo tungezungumzia mfano wa Katiba). Amri zile za Mungu wanakuja kuzipata baadaye, Kut 20:1-26, na Mbao zile mbili za ushuhuda, Kut 31:1-18, ilhali aliowaacha chini ya mlima walishajifanyia utaratibu wao (ndama yule wa dhahabu) baada ya yeye, yaani, Musa kuchelewa kurudi kutoka mlimani, Kut 32:1-6.

Somo hili la kwanza leo linafunua sifa ya Kiongozi, yaani, pamoja na mambo yote, ‘subira na utulivu wa ndani’ wenye kupelekea maamuzi yaliyo chanya na yakinifu. Hii ndiyo busara katika uongozi. Kwa ufupi waswahili wana usemi huu kuhusu sifa hii ya kiongozi, yaani, “Kiongozi ni jalala.” Je, siyo kwenye jalala kutupwapo kila aina ya uchafu na yale yasiyofaa tena kwa matumizi? Kwa kuepuka milipuko ya magonjwa jalala uyabeba yote katika yote. Hivyo Musa anakutana na changamoto katika uongozi wake, nayo ni changamoto ya kiu. “Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung'unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?” Mwa 17:3. Watu hawa hawana maji na mazingira yale yalikuwa mazingira ya jangwani. Malalamiko ya watu kwa Musa kama kiongozi, hayarudishi kwa vijembe wala kujihami, ila anasikiliza ‘sauti ya Mungu’ ndani yake. Hivyo “Bwana akamwambia Musa, Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako, ukaende,” Mwa 17:5. Mungu anamkumbusa Musa kutumia ile fimbo aliyompatia. Leo mimi na wewe kama viongozi tunakumbushwa kutumia vyema ujuzi tulioupata kutokana na elimu tuliopitia, vipaji na karama tulizo nazo kukabiliana na sintofahamu katika uongozi wetu. Huku ndiko kupambazuka kutoka kiza kinene kwa tusichokifahamu. Ni jambo la kusikitisha na kumuhuzunisha Mungu kwamba baadhi yetu huzaliwa, uishi, na kufa wakiwa wamelala usingizi mzito licha ya elimu, vipaji na karama walizojaliwa na Mungu.

Mungu asiyeshindwa lolote kwa wale wenye kumtegemea katika kweli na haki akanena na Musa na wale wazee; “Tazama, nitasimama mbele yako huko, juu ya lile jabali katika Horebu; nawe utalipiga jabali, na maji yatatoka, watu wapate kunywa. Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli,” Mwa 17:6. Hapa tunajifunza sifa nyingine na kubwa ya kiongozi, yaani, ‘kuwa na hofu ya Mungu,’ na imaanishe kweli kwamba hofu hiyo ya Mungu imo ndani ya moyo wako kwa namna uonavyo, ufikirivyo, uamuavyo, na utendavyo. La sivyo mwisho wa uongozi wako moja ya mambo haya mawili yaweza kutokea, yaani, badala ya kuwa Mhenga kuna nafasi kubwa sana ya kuwa Lihoka, yaani, roho ile ovu isiyo na chochote cha kukumbukwa. Musa ni Mhenga wetu kwa sababu katika mapito yale, aliacha kitu cha kukumbukwa. Na ndivyo ilivyokuwa kwamba baada ya changamoto ile ya kiu, Musa “akapaita mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana wa Israeli, na kwa sababu walimjaribu Bwana, wakisema, Je! Bwana yu kati yetu au sivyo?” Mwa 17:7.

Ndugu yangu unaye safari name katika tafakari hii, Injili ya leo inafunua na kuficha nguvu halisi ya Bwana wetu Yesu Kristo kama Masiha, na kiongozi wa kufuatwa katika safari hii nzima ya wokovu wa mwanadamu, Yoh 14:6. Huu ndio wakati na utimilifu wa yote, Gal 4:4-5. Katika jambo hili, Kristo anavunja ukimya uliokuwepo kadiri ya mifumo, mitazamo, mila na desturi zetu ambazo baadhi ya hizo kama zilivyo hazina uzima ndani yake. Yesu anavunja ukimya huo kwa yale yaliyokuwa yakiendelea nje ya mila na desturi za watu wake kama Wayahudi kwa mwanamke yule Msamaria wa Sikari na kumwambia, “Nipe maji ninywe,” Yoh 4:7. Watu hawa -Wasamaria na Wayahudi- walikuwa na historia zao mbaya ambazo ziliwatenga siku baada ya siku (kwa leo nisingependa kuzama sana katika jambo hili). Kristo Yesu leo anavunja pia ukimya ndani ya Taifa lake mwenyewe kama Myahudi. Na hali ilikuwa hivi; “Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema naye?” Yoh 4:27. Ujumbe uliwafikia barabara. Kiu yako na yangu leo ni kuutafuta uso wa Mungu kwa kuishi vyema na impendezavyo Mungu, hasa upendo ule kwa jirani. Na katika kiu hii Mtakatifu Agustino wa Hippo anasema, “Mioyo yetu haitulii hadi hapo itakapo tulia kwako Ee Bwana.” Kristo Yesu ndiye kielelezo na kitoshelezo cha kiu yetu kwa sababu ni kwake tu ipo Njia, kweli, na Uzima, Yoh 14:6.

Kristo Yesu kama mwalimu wetu, anachukuwa nafasi hii kutoa mafundisho/katekesi ya kweli juu yake mwenyewe, na juu ya ufalme ule wa mbinguni ambao kwa upendo wa Mungu Baba na kwa wale wote waliouridhia u urithi wao. Tendo hili la Yesu kuomba maji kwa mwanamke huyu Msamaria ndio mlango wa ufahamu wote kwa yale atakayoyazungumza juu ya kweli kuhusu Yeye mwenyewe na kila alichokijia kama Masiha. Hata hivyo kutokkana na mahusiano yasiyo afya kati ya Wasamaria na Wayahudi, kitendo kile cha Yesu kuomba maji kinamshangaza sana mwanamke yule Msamaria. Naye anahoji, “Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.),” Yoh 4:9. Yesu anaanza kuvunja kuta zile za hofu na ukimya ule wa muda mrefu na kusema, “Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai,” Yoh 4:10. Yesu anaondoa hali ile ya kufa na kuleta uzima. Hii ni moja ya changamoto kubwa leo kuhusu uinjilishaji mpya na katekesi ya kina kuhusu imani yetu. Hakuna usalama wowote kuendelea kujenga kuta za utengano. Usalama upo pale tunapozivunja kuta hizo na kujenga mahusiano katika kweli, uhuru na haki.

Pamoja na kujifunua kwake Yesu kwa mara ya kwanza kama Masiha, bado somo hili -nipe maji ninywe- linabaki katika hali ya nadharia kwa mwanamke huyu. Naye anamjibu Yesu hivi, “Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai? Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake?” Yoh 4:11-12. Ndugu yangu, kila mmoja wetu huwa kile alacho katika maana ya kwamba, kile ulicho ni tokea la historia yako (mila na desturi ulizokulia).

Yesu anamtoa mwanamke huyu Msamaria kwenye nadharia na kumpeleka kwenye tendo halisi kuhusu -“nipe maji ninywe.” Na kweli ya akisemacho Yesu juu ya “nipe maji ninywe ni hiki:-“Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele,” Yoh 4:13-14. Kweli ya hiki akisemacho Yesu kinafunua kile alicho, yaani, Masiha, na kile alichokijia, yaani, Mkombozi wetu. Uwepo wa Yesu kwako na kwangu ni kuufikia uzima wa milele, na ule ukamilifu wa Mungu, Mt 5:48, ambao bila huo hatuwezi kumwona Mungu. Ukamilifu huu ni Mtakatifu wako kama cheo chako. Yesu anasema wazi wazi kile alichokijia. “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele,” Yoh 10:10.

Mara somo linaanza kueleweka katika hatua hii ya “tendo”-nipe maji ninywe ingawa chembechembe za nadharia bado zinamsonga mwanamke huyu. “Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka,” Yoh 4:15. Hata hivyo Yesu anataka kujua kweli iliyopo ndani ya nafsi yetu, kwa sababu kama kweli hiyo ipo ndani yetu basi tu huru, Yoh 8:32. Hivyo “Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa,” Yoh 4:16. Basi “Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume; kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli,” Yoh 4:17-18. Mguso wa maneno haya ya kweli juu ya maisha ya mwanamke huyu Msamaria yanafunua ndani ya moyo wake kile alicho Kristo Yesu. “Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia,” Yoh 4:19-20.

Ndugu yangu, hadi hapa Yesu kesha yafanya yote mawili, yaani, kweli ya kile alicho, na kile alichokijia. Kilicho baki sana ni Yesu kumwonyesha njia ya kufuata ili afike pale ambapo kila mmoja wetu kwa kuumbwa kwa sura na mfano wake Mungu siyo jambo la mabati mbaya. Tumeumbwa tuishi milele. “Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli,” Yoh 4:21-24. Kumwabudu Mungu katika roho na kweli ni kujisalimisha kwa Mungu pasipo kuwa na viambata. Viambata katika imani ni ile michanganyo isiyoendana na kile alicho Mungu. Ili kupata uhakika wa kile akifanyacho, “Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote,” Yoh 4:25. Na Yesu akamaliza katekesi yake kwa hitimisho hili lenye utoshelevu wote: “Mimi ninayesema nawe, ndiye,” Yoh 4:26. Ndugu yangu, achia viambata vyako na ambatana na Kristo Yesu. Kwake upo uzima wa milele.

Ndugu yangu, furaha ni kama kikohozi huwezi kuizuia. Mara baada ya kupata kitoshelevu cha kiu yake kwa muda mrefu, “yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu, Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?” Yoh 4:28-29. Kwa tendo hili la mwanamke huyu Msamaria tunakumbushwa kushirikishana mambo yale makuu aliyotutendea Mungu. Wokovu wako uwe faida pia kwa wengine. Na kwa tendo hilo nawe unakuwa Kristo mwingine pale ulipo.

Kwa upande wa wanafunzi wa Yesu wanabaki na maswali mengi kichwani mwao. Kwa vile muda ulishakwenda, wanamsihi Mwalimu wao ale kile walichokwenda kuhemea mjini. Naye “Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi. Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake,” Yoh 4:32, 34. Kwa jibu hili la Yesu tunajifunza kwamba kiu na furaha ya Mungu ni kukupata wewe na mimi bila kujipoteza katika haya ya leo na kesho tu. Kuondoa ile sintofahamu kwa wanafunzi wake na hasa kwa tukio lile la mazungumzo baina yake Yesu na yule mwanamke Msamaria, Yesu anawaambia upendeleo waliokuwa nao mbele ya Mungu kama wahudumu, Yoh 4:35-41. Upendeleo huo unao wewe na mimi pia kwa sakramenti ya ubatizo na kipaimara (uimarisho). Atimaye Yesu anawapata wote, Wasamaria waliodharaulika na Wayahudi, na Wayahudi walio waliojitenga na Wasamaria kadiri ya misimamo yao kiimani. Na huu ndio ushuhuda wa Wasamaria juu ya Kristo Yesu: -“Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu,” Yoh 4:42.

Wapendwa wana wa Mungu, somo letu la pili latufundisha kwamba, wewe na mimi leo tunauishi Utatu huu Mtakatifu na umoja usiogawanyika tunapoambatana pasipo kujipoteza katika malimwengu tukiwa ndani ya Utatu huu kila mmoja kadiri alivyoitwa kutumika hapa duniani kama viumbe shirikishwa katika uumbaji wa pili na Mungu-“co-creators of God.” Hivyo wito na maisha yako unayoyaishi kwa uaminifu ni kwa namna hiyo hiyo unashiriki fumbo hili Takatifu katika (kuumba, kukomboa, na kutakatifuza malimwengu). Hapa ndipo twawezwa kuhesabiwa haki katika imani hiyo. Hivyo “Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu,” Rum 5:1-2. Na kuishi Imani hii katika kweli, tumaini na haki, tunawezeshwa na Roho Mtakatifu tuliyepewa. “Na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini;na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi,” Rum 5:4b-5. Je, ninalo la kujivunia au kuona fahari juu ya kufunuliwa siri na fumbo hili la Utatu Mtakatifu na umoja usiogawanyika? Sina!

Ndugu yangu, lazima uelewe jambo hili, kwamba, “Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu,” Rum 5:6. Je, mimi nimekamilika? Kama nimekamilika, je, mazingira yangu na kutenda kwangu kwa watu kuna akisi upendo huu alionifia Kristo? Ukweli ni kwamba, “Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi,” Rum 5:8. Sadaka yangu kila siku ni kuwa mwaminifu pale nilipo, na kuvuja damu kila siku kwa kujitoa vilivyo kwa kile nikifanyacho kama moja ya huduma na kuwajibika kwangu. Kutafuta huruma mbele za watu ili kuonekana mwema ni kupoteza muda na neema ya Mungu ndani yako. Huu ndio mchezo haramu na usiopendeza mbele ya Mungu unaofanywa na viongozi wetu, hasa wa kisiasa kucheza na hisia zetu.

Basi nielewa kwamba pale nilipo na kwa kila mmoja kadiri ya wito na nafasi yake ni kielezo cha mwanga kama mshumaa. Unapowaka mshumaa na kutoa kile kilicho kama mshumaa -“kuliondoa giza”- mshumaa haubaki kama ulivyo. Hii ndiyo sadaka ya kila mmoja wetu anapoishi kila alicho katika kweli na haki. Nilete uhai, furaha, matumaini, upendo, na amani pale nilipo kama Kristo afanyavyo daima.

Tusifu Yesu Kristo!

“Mimi ninayesema nawe, ndiye,” Yoh 4:26.


Tusali:-Ee Yesu Mwema na Mwalimu wetu, tuondolee woga pasipo woga ili tuweze kuabudu katika roho na kweli. Amina
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 blogger-facebook:

Post a Comment

Item Reviewed: TAFAKARI YA SIKU: Dominika ya 3 ya Kwaresima Mwaka A Tarehe 19/03/2017 Rating: 5 Reviewed By: Unknown