728x90 AdSpace

­
Latest News
March 18, 2017

MASOMO YA MISA : Jumamosi, Juma la 2 la Kwaresima Mwaka A Tarehe 18/03/2017


SOMO 1
Mik. 7:14-15, 18-20

Walishe watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako, wakaao peke yao, mwituni katikati ya Karmeli; na walishe katika Bashani na Gileadi, kama siku za kale. Kama katika siku zile za kutoka kwako katika nchi ya Misri nitamwonyesha mambo ya ajabu.
Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema. Atarejea na kutuhurumia; atayakanyaga maovu yetu; nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi yva bahari. Wewe utamtimilizia Yakobo kweli yako, na Ibrahimu rehema zako, ulizowaapia baba zetu tangu siku za kale.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 103:1-4, 9-12 (K) 8

(K) Bwana amejaa huruma na neema.

Ee nafsi yangu umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote. (K)

Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema. (K)

Yeye hatateta sikuzote,
Wala hatashika hasira yake milele.
Hakututenda sawa na hatia zetu,
Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. (K)

Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. (K)

SHANGILIO
Yn. 6:64, 69

Maneno yako, Ee Bwana, ni roho, tena ni uzima; Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.

INJILI
Lk. 15:1-3, 11-32

Watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia Yesu wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung’unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao. Akawaambia mfano huu, akisema,
Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati.
Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye.
Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteeni ndama yule aliyenona mkamchinje nje; nasi tule na kufurahi; kw akuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia.
Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na lipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima. Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema. Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wowote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona.
Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami siku zote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuw ahuyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 blogger-facebook:

Post a Comment

Item Reviewed: MASOMO YA MISA : Jumamosi, Juma la 2 la Kwaresima Mwaka A Tarehe 18/03/2017 Rating: 5 Reviewed By: Unknown