728x90 AdSpace

­
Latest News
March 18, 2017

TAFAKARI YA SIKU: Jumamosi, Juma la 2 la Kwaresima Mwaka A Tarehe 18/03/2017


Masomo:

    Somo: Mik 7:14-15; 18-20

    Zab: 103:1-2, 3-4, 9-10, 11-12

    Injili: Lk 15:1-3; 11-32

Nukuu:

“Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema,” Mik 7:18

“Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako,” Lk 15:18-19

TAFAKARI: “Toba ya kweli; Upendo na Msamaha wa Mungu.”

Wapendwa wana wana Mungu, kwa pamoja tutafakari kwa undani “toba ya kweli; Upendo na Msamaha wa Mungu.” Somo la kwanza linatuelezea uhalisia wa Mungu. Mungu kwa asili ni Upendo, Huruma, na Msamaha. Ni Mungu anayetutakia mema muda wote sisi viumbe na wana wake. Ni Mungu anayejifunua kwetu kwa njia mbali mbali, ikiwa ni kwa njia ya historia na vile alivyoviumba. Ni Mungu ambaye yupo na alikuwepo nyakati zote hata kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu. Tulikuwa daima ndani ya mawazo yake.

Kwa upande wetu,  tuna kazi moja tu, yaani, kumtafuta kwa maana anapatika. Nabii Isaya anatuambia hivi, “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu baribu; Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki aache mawazo yake; na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa.” Isa 55:6-7.

Ndugu yangu, kumwasi Mungu ni tendo ambalo lipo chini ya uwezo wetu. Kumrudia Mungu ni tendo la toba na kufanya maamuzi sahihi na ya msingi. Tunapofanya maamuzi haya ni wazi kabisa kwamba yatupasa kuachilia mengi ambayo kwayo yalitupa furaha na hata kujulikana na kujikweza. Ila tukitambua umuhimu wa umilele wa maisha yetu, hatuna budi kuachilia yote haya ambayo ni ya kupita na ya muda mfupi.

Tunapofanya toba ya kweli na kumrudia Mungu, hutupokea kama tulivyo. Mungu katika mapokezi haya hatazamani historia yetu. Mungu huanza mradi mpya nasi na kutufanya wapya tena katika yale mazuri anayotufikiria. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho,” Yer 29:11. Ndugu yangu, kwa nini hubadiliki? Waitaji malaika washuke na kukuambia jambo hili? Kwa nini unakuwa kero kwa ndugu na jirani zako? Kwa nini unakuwa kero kwa wanajumuiya zako na viongozi wako? Je, unapenda kuishi hivyo hadi lini?

Injili yetu ya leo inatupa kisa na simulizi la mwana mpotevu. Wahusika wakuu katika kisa hiki ni Baba mzazi, Mwana mpotevu, na Kaka ya mwana mpotevu. Wengine ni watumishi au watumwa wa Baba mzazi wa Mwana mpotevu, na marafiki wa mwana mpotevu. Mwana mpotevu, tena aliye mdogo katika familia hii, anafanya kitu ambacho si cha kawaida katika jamii na hasa mila na desturi kama zilivyokuwa. Kitendo cha kuomba urithi au sehemu ya mali yake kabla ya kifo cha baba yake, kulimaanisha kumtakia baba yake mabaya. Ni kutokumtambua baba yake. Ni kumchukulia baba yake kama marehemu.

Kwa upande wa baba yake, na kutokana na upendo aliokuwa nao kwa wana wake na familia, anakubali aibu hiyo, na kufanya kadiri ya matakwa ya mwanaye. Baba anampa sehemu ya urithi wake. Yaliyompata kijana huyu wote tunafahamu simulizi hili. Ndugu yangu, kutenda makosa ni hali yetu sote wanadamu. Ila tofauti ipo hapa; unapotambua umefanya kosa na kuchukua hatua kwa uliyoyafanya ndiko kunapoturejeshea hadhi na heshima yetu tena. Mwana mpotevu analiona kosa lake na anakiri kwa matendo na maneno, “Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako,” Lk 15:18-19. Ndugu yangu, haya ndiyo majuto ya kweli. Tunachoangalia si aibu tutakayopata, bali huruma, neema, na stahili tunayoyapata kwa kufanya toba ya kweli.

Ndugu yangu, unapodondoka kwa sababu ya dhambi, usione aibu kuamka na kuomba msamaha kwa muumba wako. Yeye Mungu anasema, “mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.” Ufu 1:8. Je, kuna mwingine wa kumkimbilia zaidi ya Mungu wetu? Mungu aliye Upendo hana mipaka wala masharti ya pekee unapomrudia. Mungu anasema, “nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii wataniona,” Mit 8:17.

Upendo wa Baba hauna mfano. Katika simulizi hili la mwana mpotevu, Baba huyu anapomwona mtoto wake, hapendi na wala haitaji kujua historia ya yale maovu aliyofanya. Furaha yake ni kumwona mwanaye kama alivyo, na anajua kurudi kwake ni toba ya kweli. Anachofanya Baba ni kumrudishia stahili yake kama mwana na mmoja wa familia. Ni kumwesabia haki tena kama mwana familia. Lakini jambo la kushangaza ni kwamba tendo hili la Baba, linakuwa sononeko la Kaka ya mwana mpotevu. Haoni maana ya furaha hii na sababu ya kuwa hai mdogo wake. Ndugu yangu, katika safari ya wokovu, tusipende kujitazama wenyewe. Wokovu ni kwa wote na nifuraha ya Mungu. Katika mfano huu, Yesu anawakemea Waisraeli na hasa Mafarisayo ambao wanahuzunika kwa yale anayofanya Yesu ambao ndio upendo wa Mungu Baba.

Yatupasa mimi na wewe kutiana moyo na kufurahia pale mwenzetu au wenzetu wanapomwongokea Mungu na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu. Mara nyingi hatuachi kuwasema vibaya wale wanaojitahidi kuishi njia impendezayo Mungu. Tunawapachika majina mengi, na kuwakatisha tamaa kabisa. Kwa upande wetu, mwenzetu anapojitahidi kuishi vizuri, basi iwe changamoto ya sisi kufanya vizuri.

Ndugu yangu, wakati ndiyo sasa! Kaa na tafakari namna utendavyo. Je, unafanya kadiri ya mapenzi ya Mungu? Urithi wako ni fursa uliyonayo sasa katika utendaji. Je, unatumia fursa hiyo vizuri kwa Sifa na Utukufu wa Mungu? Je, baada ya kuishi ovyo kwa muda wote huo, upo tayari kufanya toba ya kweli na kuacha njia hiyo mbaya? Basi nielewe nafasi niliyo nayo ni leo na sasa tu. Ni vyema nikachukua hatua sasa na kuutafuta uso wa Bwana. “Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya Bwana,” Sef 2:3

Tumsifu Yesu Kristu!

“Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako,” Lk 15:18-19

Tusali:-Ee Yesu, niongoze katika kweli yako. Amina
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 blogger-facebook:

Post a Comment

Item Reviewed: TAFAKARI YA SIKU: Jumamosi, Juma la 2 la Kwaresima Mwaka A Tarehe 18/03/2017 Rating: 5 Reviewed By: Unknown