728x90 AdSpace

­
Latest News
March 15, 2017

TAFAKARI YA SIKU: Alhamisi, Juma la 2 la Kwaresima Mwaka A Tarehe 16/03/2017.


Masomo:
 
    Somo: Yer 17:5-10

    Zab: 1:1 1-2, 3-4, 6

    Injili: Lk 16:19-31

Nukuu:

“Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana,” Yer 17:5

“Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake,” Yer 17:7

“Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake,” Yer 17:10

“Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu.” Lk 16:29,31

TAFAKARI: “Kuishi bila hofu ya Mungu; kutotimiza wajibu na kutokujali.”

Wapendwa wana wa Mungu, niwaalike tena kwa siku ya leo, tutafakari pamoja, “kuishi bila hofu ya Mungu; kutotimiza wajibu na kutokujali.” Somo letu la kwanza laelezea hathari za kuishi bila kuwa na hofu ya Mungu. Injili yatuelezea hathari za kutotimiza wajibu na kutokujali.

Ndugu, tuanze safari yetu kwa kutafakari kwa undani hathari za kutokuwa na hofu ya Mungu. Je, hofu ya Mungu ni nini? Mpendwa, hofu ya Mungu ni kuishi kwa kumtegemea Mungu kwa kila jambo. “Ee Bwana, Mungu wangu, umefanya kwa wingi Miujiza yako na mawazo yako kwetu; Hakuna awezaye kufananishwa nawe; Kama ningependa kuyatangaza na kuyahubiri, Ni mengi sana hayahesabiki,” Zab 40:5.

Ni kujenga mahusiano ya karibu na Mungu kiasi kwamba huwezi fanya lolote bila kumshirikisha Mungu. Ndugu yangu, “mkabidhi Bwana kazi zako, na mawazo yako yatathibitika,” Mit 16:3. Mtu anayeishi katika hofu ya Mungu, upanga na Mungu, uwaza na Mungu, ushauriana na Mungu, na uyakabidhi maisha yake mwenyewe na mipango yake yote kwa Mungu. Huku ni kuishi katika baraka kama asemavyo Nabii Yeremia, “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake,” Yer 17:7

Kuishi bila hofu ya Mungu ni kujiamini kusiko fikirika. Ni kuamini na kutegemea vitu na mali, watu na vyeo vyao. Huku ndiko tunapochuma laana kama anavyosema Nabii Yeremia, “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana,” Yer 17:5. Mtu wa mwono huu kimaisha hawezi pata baraka. Mungu hana nafasi katika maisha yake. Na hapendi kumpa Mungu nafasi.

Mtu asiye na hofu ya Mungu huishi maisha linganishi mara zote. Mtu wa mtindo huu kimaisha hawezi jipokea alivyo; na hivyo ni vigumu kufanya mabadiliko kimwili na kiroho. Mtu wa mtindo huu awezi kuwa na furaha ya kweli. Muda wote huishi maisha ya ushindani na kusahau jambo lililo la msingi katika maisha yake, yaani, Mungu hupendezwa nawe kama ulivyo. Uwepo wako ulimwenguni hapa si bahati mbaya. Maisha bila Mungu ni sawa na samaki bila maji. Hivyo ni wajibu wangu na wako kuitafuta sura ya Mungu kila siku. “Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, Niamkapo nishibishwe kwa sura yako,” Zab 17:15. Kwa nini basi itakupasa kuitafuta sura ya Mungu kila siku? Mtume Paulo anasema, “Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni,” 1Kor 15:49. Na sura ya yule wa mbinguni ni UTAKATIFU. Ndugu yangu, bila Utakatifu hakuna mbingu. Kuitafuta Sura ya Mungu ni kuutafuta Utakatifu na kuuishi huo utakatifu tungali hai kila mmoja wetu kadiri ya mazingira na wito wake.

Furaha ya kweli haipatikani kwa mali tulizonazo; bali twaipata kwa kujipokea kama tulivyo na kujua upendo wa Mungu ndani yetu. Yeye Mungu yupo tayari kutupokea na kutufanya tena wana wake tunapokiri kupotoka kwetu na kumuasi. Mungu huturudishia hadhi yetu na mastahili yetu kama watoto wake. Hii ndiyo furaha ya kweli ndani mwetu. Hakuna mamlaka yoyote au binadamu yeyote awezaye kuyafanya haya. Ni Mungu tu.

Somo la Injili la tupa kisa cha tajiri na maskini Lazaro. Tajiri anajulikana kwa mwono wake, na maisha yake ya anasa. Lazaro anajulikana kwa jina lake, umaskini wake na unyonge wake. Kosa kubwa la tajiri huyu ni dhambi ya kutotimiza wajibu. Ndugu yangu, kabla ya kuendelea na tafakari hii nikuombe usali kwanza sala ya “NAKUUNGAMIA.” Dhambi ya kutotimiza wajibu, ni kosa la nne tunalokiri katika sala hii ya “nakuungamia Mungu mwenyezi.” Lazaro tunaambiwa mara zote alikaa kwenye mlango, ikimaanisha kwamba kwa vyovyote vile tajiri huyu alimwona Lazaro katika dhiki yake na ilimpasa tajiri huyu afanye kitu. Kutotimiza wajibu, ni kosa la kutokufanya kitu wakati ulitakiwa kufanya kitu. Tajiri huyu anahukumiwa kwa kutokujali na kutokufanya chochote.

Ndugu yangu, tazama mazingira unayoishi, Je, akina Lazaro hawapo? Wale Mungu aliotubariki kuwa na Magari binafsi, Je, unapofunguliwa geti hujamwona Lazaro pembeni akisubiri wema na upendo wako? Wale ambao hula vizuri kila siku na asubuhi kumwaga viporo vya wali na vipande ya samaki, Je, huwaoni akina Lazaro wakilichungulia shimo taka kwa masikitiko? Wewe ambaye kila siku huingia ofisini na mkoba wako, Je, humuoni Lazaro kwenye ‘benchi’ akisubiri wema na huruma yako?

Ukweli ni kwamba, wote tutakufa na kujongea kiti cha ukumu. Tunapoishi hapa duniani, tunaaswa na mzaburi, “usiogope mtu atakapopata utajiri, na fahari ya nyumba yake itakapozidi. Maana atakapokufa hatachukua cho chote; utukufu wake hautashuka ukimfuata,” Zab 49:16-17. Mambo yote yatupayo ufahari ipo siku tutayaacha. Je mbele ya Mungu tutafika na jambo gani kama utambulisho wetu?

Ndugu yangu, ijumaa ijayo, nakualika wakati wa njia ya msalaba utafakari kituo cha tisa; Yesu anaanguka mara ya tatu. Njia ya msalaba kwa kutumia misale ya waamini, kuna maneno haya katika kituo hiki cha tisa; “Mara nyingi mno ninajibovusha kwa kupenda mno starehe, anasa na tafrija. Ee Yesu mwema, nisaidie kuufuata mfano wa Mtakatifu Paulo, niutese mwili wangu na kuutumikisha, ili nipate siku moja tuzo mbinguni.” Katika kujibovusha huko, hujakutana na akina Lazaro?

Tunapojitesa na kuwajali wengine, hakika tutapata tuzo mbinguni. Mateso aliyoyapata Tajiri, alitamani na kuomba taarifa zile ziwafikie ndugu zake ili wasije patwa na mateso yale. Ibrahimu anamjibu, “wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu.” Lk 16:29,31. Ndugu yangu, hapa Musa anawakilisha Sheri za Mungu na Amri zake. Manabii hapa ni wale wahudumu wa neno la Mungu. Kwa maana nyingine tungesema, sisi kama wafuasi wa Kristo tunajua taratibu zitupasazo kuishi, ikiwa ni pamoja na Amri za Mungu. Na Amri kuu kupita zote ni Amri ya upendo. “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii,” Mt 22:37-40 Pili, tumepewa wachungani, na wapo muda wote kwa kutuhudumia hasa kiroho. Tunaonywa na kufundishwa kupitia mahubiri yao. Kwa kuyashika haya mawili na kuyaishi, basi tuzo tutalipata. Nje ya hapo tutegemee mateso makali.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake,” Yer 17:7

Tusali:-Ee Yesu, tuepushe na dhambi ya kutokujali na kutotimiza wajibu wetu. Amina
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 blogger-facebook:

Post a Comment

Item Reviewed: TAFAKARI YA SIKU: Alhamisi, Juma la 2 la Kwaresima Mwaka A Tarehe 16/03/2017. Rating: 5 Reviewed By: Unknown