728x90 AdSpace

­
Latest News
March 13, 2017

TAFAKARI YA SIKU: Jumatatu, Juma la 2 la Kwaresima Mwaka A Tarehe 13/03/2017


Masomo:-

     Somo: Dan 9:4-10

     Zab: 79:8, 9, 11, 13

     Injili: Lk 6:36-38

Nukuu:

“Rehema na msamaha ni kwa Bwana wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake manabii,” Dan 9:9-10.

“Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa,” Lk 6:36-37.

TAFAKARI: “Huruma na Msamaha wa Mungu; kwa kuacha dhambi na kuongoka.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, leo tutafakari juu ya “huruma na msamaha wa Mungu; kwa kuacha dhambi na kuongoka.” Ndugu yangu, ni ukweli kabisa kwamba hakuna asiye na dhambi. Wate tuishio katika dunia hii twaitaji neema na huruma ya Mungu kila wakati. Kuishi katika ukweli huu, yaitaji unyenyekevu mkubwa. Kishawishi kikubwa cha mwanadamu ni kule kutaka kuwa sawa na Mungu muda wote. Kiburi hiki ni sababu la anguko la wazazi wetu wa kwanza. Ila kwa neema ya Bwana wetu Yesu Kristu, sote tumepata uwezekano wa kumrudia Mungu.

Mpendwa, “tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo wetu,” 1Yoh 1:8. Kuna njia moja tu ya kumrudia Mungu. Njia hii ni kukiri makosa yako bila kujibakiza. Ndugu yangu, “tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote,” 1Yoh 1:9. Jambo hili linawezekana kwa Mungu kwa sababu yeye ni mwaminifu na “rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi,” Dan 9:9.

Kiburi chetu na kukosa unyenyekevu ndicho Nabii Danieli anatupa angalizo. Nyakati za Nabii Danieli, watu wote walimwasi Mungu. Kiburi hiki kilikuwa kwa wakuu na wafalme mbele ya uso wa Mungu. Nabii Danieli kwa niaba ya watu wake anasimama na kusema,  “Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi.” Dan 9:8. Wapendwa, mahangaiko ya watu na uovu kuendelea katika jamii yetu leo kwa kiasi kikubwa yanatokana na dhambi za kila mmoja wetu kadiri azitendavyo, na dhambi ya kijamii-“social sin,” ambayo kwa kiasi kikubwa hutendwa na watawala wetu kwa nafasi walizokuwa nayo. Jambo hili lilitokea pia wakati wa Nabii Danieli.

Asiposimama mmoja kati yetu na kuomba huruma hiyo ya Mungu, kamwe tusitegemee huruma na msamaha wa Mungu. Tazama taifa letu leo mambo yanavyokwenda. Je, ni mara ngapi, na tena kwa uwazi kabisa viongozi wetu wanapuuza sauti za waliowaweka madarakani? Tuelewe kabisa kwamba, sauti ya watu ni sauti ya Mungu. Kwa ukweli wa jambo hili, embu turejee mchakato mzima wa pendekezo la Katiba mpya kwenye Bunge la katiba. Je, Mungu kupitia sauti ya watu alisikilizwa na wale tuliowachagua kufanya kazi hiyo? Cha kushangaza bado tunapambana na Mungu kwa kufanya kila tuwezacho ili mawazo yetu na tamaa zetu zishinde nguvu ya Mungu. Jambo hili lina hatari kubwa sana kwa maisha yetu ya usoni.

Nachelea kujiita Nabii, ila kadiri nionavyo, hatujampa Mungu nafasi ya kutosha hasa kwa jambo hili muhimu si tu kwa sisi, bali kwa kizazi kijacho. Mungu hata kaa kimya kamwe kuona Taifa lake linateketea. Watumishi wa Mungu leo hawasikilizwi hata kama wakikemea uovu huu. Nyakati za Nabii Danieli kadiri ya somo letu la leo hawakusikilizwa kabisa. Kwa sauti ya unyonge, Nabii Danieli anasema, “tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi,” Dan 9:5-6. Hakika tunaitaji mtu, au nguvu ya kutuvusha hapa tulipo kama Taifa. Lolote tutakalo tenda kwa sasa bila kusikiliza sauti ya Mungu, hakutakuwa na baraka yoyote.

Injili yaeleza kwa undani huruma ya Mungu. Yesu anasema, “Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma,” Lk 6:36. Huruma anayotutaka Bwana wetu Yesu Kristo tuwe nayo, ni huruma katika kutenda tukiwa na hofu ya Mungu. Muda tuliokuwa nao sasa baada ya kutenda dhambi, na wote tukiwa tunaitaji huruma ya Mungu, si muda wa kulaumiana na kuhukumiana. Yesu anatupa angalizo; “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa,” Lk 6:36. Angalizo hili la Yesu halina maana ya kutowajibika au kutowajibishwa kwa makosa tunayotenda hasa kwa dhambi ya kijamii-“social sin,” la hasha! Wote wanaohujumu Taifa hili yawapasa kuona ni kosa na kuchukua hatua. Wasipofanya hivyo, Mungu mwenyewe atatoa hukumu kwa wakati wake kwa sababu tayari anaona mateso ya watu wake.

Dhambi ya kijamii ni kupigana na kushindana na Mungu moja kwa moja kwa kile ulicho, nafasi uliyo nayo, na mbaya zaidi kama kiongozi. Umekuwa kama ulivyo kwa tokeo la tendo la Mungu. Ni Mungu aliyekuweka kuwa hivyo kwa niaba yake uwatumikie watu wake. Kwani, “sauti ya watu ambao wamekuweka madarakani ni sauti ya Mungu.” Wengi wetu jambo hili hatulijui kiundani, na kama tunalijua tunalichukulia kimzaha mzaha tu bila umakini na umahiri.

Tendo hili la kupigana na Mungu kwa uwazi huu, na tena bila kujali na kujirudi, ni kumkufuru Roho Mtakatifu. Dhambi hii hakuna wa kusamehe. “Bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele,” Mk 3:29.

Sasa tufanye nini ndugu zangu? Wapendwa, bila Yesu na kwa msaada wake, hatuwezi kuvuka bonde hili. Tunamwitaji Yesu sasa zaidi ya kitu kingine unachoweza kufikiri. Kwa sababu, “Mtu huyu Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi,” Mdo 5:31. Hakuna njia yeyote tuwezayo kupita isipokuwa kwa njia ya Yesu Kristo. Hili amelisema mwenyewe Yesu Kristo na siyo mimi wapendwa. “Yesu akawaambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” Yoh 14:6. Ni katika Yesu Kristo, “ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi,” Kol 1:14

Ndugu yangu uliyefuatana nami katika tafakari hii, ni kazi yako kama mbatizwa na mfuasi hai, wa kweli na mwakilishi wa kristo pale ulipo, tunaposhika na kufuata ushauri huu wa Mtume Paulo, "uwafubue macho yao, na kuwagueza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.” Mdo 26:18. Hii ndiyo maana ya kuimarishwa katika sakramenti ya Kipaimara.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa,” Lk 6:36-37.


Tusali:-Ee Yesu, tujalie ujasiri wa kuiishi Imani yetu na kusimama katika kweli yako siku zote za maisha yetu. Amina
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 blogger-facebook:

Post a Comment

Item Reviewed: TAFAKARI YA SIKU: Jumatatu, Juma la 2 la Kwaresima Mwaka A Tarehe 13/03/2017 Rating: 5 Reviewed By: Unknown