728x90 AdSpace

­
Latest News
March 13, 2017

Tafakari ya Neno la Pili (2) alilotamka Yesu Akiwa Msalabani


Baada ya kutafakari Neno la Kwanza katika Makala iliyopita, mpendwa msomaji na mfuatiliaji wa Tafakari katika Blog yetu ya Fumbuka, karibu tena leo tutafakari neno la pili alilotamka Yesu akiwa Msalabani:


(II) “AMIN, NAKUAMBIA, LEO HIVI UTAKUWA PAMOJA NAMI MBINGUNI”

Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, “Je, wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.” Lakini yule wa pili akamjibu, akamkemea, akisema, “Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lolote lisilofaa.” Kisha akasema, “EeYesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.” Yesu akamwambia, “Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami mbinguni.” (Luka 23:39-43)

Neno la pili la Yesu msalabani lathibitisha kuwa msamaha una nguvu kuliko dhambi. Yesu amefundisha juu ya msamaha kwa kuwaombea msamaha watesi wake. Yesu ameonesha kuwa yeye ni Mungu kwa kutumia tabia kuu ya Mungu ya kusamehe. Yule mhalifu ametambua kosa lake na amemtambua Yesu kuwa ni Mungu na akaomba msamaha; Yesu mara moja akamsamehe kwa kumpa nafasi mbinguni.

Leo hii utakuwa pamoja nami mbinguni: Neno hili ni habari njema ambayo kila mmoja wetu angefurahi kuambiwa na Yesu. Hapa Yesu anatufundisha kuwa, Mungu humpa msamaha papo kwa papo mtu yeyote anayeomba msamaha bila kujali amekosa nini.

Ni dhambi kubwa kuishi na dhambi bila kuomba msamaha. Kutoomba msamaha kwa Mungu ni dharau kubwa. Yule mhalifu mwingine alimdharau Mungu na kumtaka amshushe msalabani; kumbe huyu mwingine alimwogopa Mungu na kuomba msamaha.

Katika neno la kwanza Yesu alifundisha kuwa jambo la kwanza mbele ya Mungu ni kuomba msamaha. Mhalifu wa kwanza hakuelewa mafundisho hayo, ndiyo maana badala ya kuomba msamaha akaomba muujiza wa kushushwa msalabani. Muujiza huo hakuupata kamwe. Kumbe yule mhalifu wa pili alielewa vema mafundisho ya Yesu pale Msalabani; akaomba msamaha. Huyu alipata alichokiomba palepale bila kupewa ahadi; Leo hii utakuwa pamoja nami mbinguni.

Ukombozi ni msamaha wa dhambi zetu na kuingizwa mbinguni. Ukombozi ni tendo au jambo la leo na sio kesho. Ukombozi hautafutwi kesho na wala hauombwi kesho. Ukombozi daima ni leo; ndiyo maana Yesu anasema: Leo utakuwa pamoja nami mbinguni. Yesu hakusema, Ngoja kwanza nifufuke siku ya tatu nitakukaribisha mbinguni.

Neno LEO katika Injili ya Luka lina maana ya kufuta yaliyopita na kumwingiza mtu katika maisha mapya. 

Yesu alipozaliwa malaika waliwaambia wachungaji: LEO katika mji wa Daudi, kwa ajili yenu amezaliwa mwokozi ndiye Kristo Bwana.

Yesu alipoanza kuhubiri nyumbani kwao Nazareth aliwaambia: LEO Maandiko haya yametimia masikioni mwenu.

Yesu alipokutana na mtu mwenye dhambi aitwaye Zakayo alimwambia: Zakayo shuka upesi, kwa kuwa LEO imenipasa kushinda nyumbani mwako. Na alipoenda nyumbani kwa Zakayo alimwambia: LEO wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.

Na mwisho Yesu alimwambia yule mhalifu aliyeomba msamaha: LEO hii utakuwa pamoja nami mbinguni.

Kwa hiyo, neno LEO lina maana ya kufuta historia ya zamani ya dhambi na kumwingiza mtu katika historia mpya ya neema, yaani uwepo wa Mungu rohoni mwetu. Yesu anatualika mimi na wewe tuingie leo hii katika historia mpya. Katika ukombozi hakuna neno kesho; ukombozi ni leo. 

Anza leo hii kuomba msamaha kwa Mungu. Anza leo kuomba msamaha kwa wote uliowakosea. Anza leo kuwasamehe wote waliokukusea. Leo hii, utakuwa mwana wa Mungu na mbinguni ndiko kutakuwa nyumbani kwako milele.

Tunajifunza nini kutoka kwa mwalifu wa Kwanza: Wengi wetu tunaomba Miujiza kwa Mungu pasipo kujipatanisha kwanza na Mungu, Sala ya kweli ni ile inayotanguliwa na Toba.

Tunajifunza nini kutoka kwa Mwalifu wa Pili: Tujinyenyekeze kwa Mungu na kumkimbilia yeye, Maana maandiko matakatifu yanasema “Ni Mwingi wa Huruma si mwepesi wa hasira”.

Katika Makala Ijayo tutatafakari Neno la Tatu la Yesu Akiwa Msalabani….

Ee Yesu tunakuabudu na tunakushukuru; Kwa Kuwa Umewakomboa Watu kwa Msalaba Wako Mtakatifu.
**********************************************************************
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 blogger-facebook:

Post a Comment

Item Reviewed: Tafakari ya Neno la Pili (2) alilotamka Yesu Akiwa Msalabani Rating: 5 Reviewed By: Unknown