728x90 AdSpace

­
Latest News
March 13, 2017

TAFAKARI YA SIKU: Jumamosi, Juma la 1 la Kwaresima Mwaka A Tarehe 11/03/2017


Masomo:

      Somo 1: Kumb 26:16-19

      Zab: 119:1-2, 4-5, 7-8

       Injili: Mt 5:43-48

Nukuu:

“Umemwungama Bwana leo, kuwa ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake na maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake,” Kumb 26:17

“Lakini mimi nawaambia: Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki,” Mt 5:44-45

Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48

TAFAKARI: “Kuishi ahadi zetu za ubatizo: Kuwapenda Maadui zetu na kuwa wapatanishi.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo tuyatafakari makuu ya Mungu kwa “kuishi ahadi zetu za ubatizo; kuwapenda maadui zetu na kuwa wapatanishi.” Somo letu la wana wa Israeli wanamuungama Mungu kwa kuzishika amri zake. “Umemwungama Bwana leo, kuwa ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake na maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake,” Kumb 26:17. Nasi leo kama wafuasi wake Kristo somo hili latukumbusha ahadi za ubatizo wetu. Ubatizo wetu ni kumwungama Kristo kwa fumbo la mateso, kifo na ufufuko wake. Fumbo hili linatufanya kuzaliwa upya kwa Roho Mtakatifu. Kuzaliwa huku ni kule Yesu anapomtaka Nikodemo azaliwe upya. “Yesu akamwambia, Amin, Amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu,” Yoh 3:3.

Kuishi ahadi zetu za ubatizo ni kutembea katika njia za Bwana wetu Yesu Kristo. Tu wakristo kwa sababu tu wafuasi wa Kristo. Na kama tu wafuasi wa Kristo, yatupasa kutembea katika njia zake. Tomaso alitaka kujua njia impasayo kuifuata kama mfuasi wa Kristo. “Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia? Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:5-6.

Mpendwa katika Kristo, njia yetu wabatizwa na wafuasi wa Kristo ni Yesu mwenyewe. Na njia aliyochagua ni njia ya Msalaba. Hatuwezi kuukwepa Msalaba kama tu wafuasi wa Kristo. Msalaba ni utukufu wetu na ushindi wetu. Ukweli wake ni yale anayotufundisha, nayo ni habari njema ya Wokovu. Habari hii ya wokovu ni uhai na umilele ambao yeye mwenyewe anasema, “ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo, huku, au, kule kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu,” Lk 17:20b-21. Mfano mzuri ni pale ufanyapo mtihani. Mwalimu anapokupa mtihani, 100% unayo wewe mwenyewe. Yakupasa kumwonyesha mwalimu asilimia hiyo 100. Maana yake kufaulu kwa mtihani kupo kwako na ni juu yako.

Uzima katika Kristo tunaupata tunaposhiriki masakramenti yake, na hasa sakramenti ya Ekaristi Takatifu tukiwa na mioyo safi. “Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe,” Yoh 6:35.

Tunaishi ahadi zetu za ubatizo kwa kuzishika amri zake na kufuata maagizo yake. Ni kuwa na hofu ya Mungu ndani mwetu. Na amri iliyo kuu ni ya upendo. “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo,” Yoh 13:34. Amri hii ya upendo na nyinginezo zatupasa kuzishika si kinadharia tu bali kwa matendo yetu na yenye kumpendeza Mungu. Huku ni kudhihirisha tunampenda Yesu Kristo na yule aliye mpeleka. “Yeye aliye na mri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21. Tendo hili la kuzishika amri za Mungu ni kukaa katika pendo la Mungu. Huku ni kumuishi Kristo aliyekaa katika pendo la Mungu kwa kushika amri zake. “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10.

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, somo la Injili latualika pia kutafakari juu ya upendo wetu na maadui zetu, ambao tunda lake ni upatanishi. Si jambo rahisi kibinadamu kumpenda adui yako, hasa pale unapoyakumbuka mabaya aliyokutendea. Ila tusipo enda zaidi ya kuwapenda wale tu ambao wanatupenda, ukristo na ufuasi wetu bado haujakomaa, na imani yetu bado changa. “Lakini mimi nawaambia: Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki,” Mt 5:44-45. Huku ndiko kwenda zaidi ya yale yaonekanayo kwa mtazamo wa kibinadamu ambayo kwayo hutupatia haki ya leo na sasa, na kukosa neema ya huruma ya Mungu. Hivyo kwa kuyapata hayo tu huyafanya Maisha yetu ya kiroho kuwa na ulakini.

Tunakuwa wana wa Mungu tu kwa kuwapenda maadui zetu na kuwaombea. Kwa dhambi zetu tulikuwa maadui na Mungu. Ila kwa kupitia mwanaye Yesu Kristo kwa mateso, kifo na ufufuko wake tumepatanishwa na Mungu. Kristo ni kielelezo cha UPANANISHO HAI NA WA KWELI. Nasi kwa kumfuata Kristo tunafanya kazi hiyo ya upatanisho kwa kuwaombea watesi wetu kwa Mungu awabadili mienendo yao mibaya. “Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?” Mt 5:46-47. Wapendwa inasikitisha sana kuona miongoni mwetu kadiri ya wito na utume wetu, tumekuwa wakristo wazuri sana wa jumapili, twakiri kuwa askari imara wa Kristo, na ifikapo jumatatu tunatoroka kambini na kufanya kinyume kabisa na utambulisho wetu kwa kutowapenda na kutokuwa tayari kuwasamehe watesi wetu. Kwa kweli haya ni zaidi ya maigizo.

Ndugu yangu, hatuwaombei mabaya maadui zetu. Tukumbuke nao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, Mwa 1:27. Mungu tu ndiye anayeweza kuwabadili kwa sababu ndani yao ipo chapa yake-sura na mfano wake. Kwa upendo alio nao Mungu wetu kwa wema na waovu, hata kaa kimya aache chapa yake ipotee bure. Kwa msaada wa sala zetu, Mungu yupo tayari kuwabadili kwa tendo hili la sala na majuto. Tunakuwa pia wana wa Mungu kwa kuwa wapatanishi. “Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu,” Mt 5:9.

Upatanisho ni tendo la ibada na ukombozi. Misa Takatifu kama ibada ya neno na Ekaristi Takatifu ni tendo la upatanisho. Tunapatanishwa nafsi zetu, wenzetu (wema na waovu), na Mungu. Huku ndiko kumwilishwa kwa neno (Mwana wa Mungu), kuwa mwili. Ni tendo la upendo mkubwa wa Mungu Baba kwetu wanadamu. Ni ufupisho wa historia yote ya wokovu wetu.

Hivyo basi, kama mfuasi mwaminifu na mwenye hofu ya Mungu, wewe na mimi yatupasa kufurahi na kushangilia pale tunaposhutumiwa kwa ajili ya haki, tunapoudhiwa na kunenewa kila neno baya kwa uongo kwa ajili ya Kristo. Hii ndiyo maana halisi na mapaswa ya kuwa mkristo wa kweli na mfuasi wa Kristo. Yesu anasema, “heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12.

Ndugu yangu, hii ndiyo changamoto ya kweli ya ishi yetu kama wakristo. Kuishi huku kunakuhitaji kuziishi ahadi zako za ubatizo kuwapenda maadui zako, na kuwa wakili wa Kristo, yaani mpatanishi. Ahadi hizi za ubatizo ndicho alichokifanya Yesu Kristo katika safari nzima ya wokovu wetu. Je, upo tayari kuvivaa viatu vya Yesu?

Tumsifu Yesu Kristu!

Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48

Tusali:- Ee Yesu, uliye Njia, Ukweli, na Uzima, kamwe usituache katika fumbo hili la wokovu wetu, yaani kuziishi ahadi zetu za ubatizo na kuwa mawakili wako, yaani Wapatanishi. Amina
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 blogger-facebook:

Post a Comment

Item Reviewed: TAFAKARI YA SIKU: Jumamosi, Juma la 1 la Kwaresima Mwaka A Tarehe 11/03/2017 Rating: 5 Reviewed By: Unknown