728x90 AdSpace

­
Latest News
March 2, 2017

MAKALA: Mambo ya Msingi ya kuzingatia kabla ya kusoma Biblia


Na. James Waibina
Mpendwa msomaji wa Jarida letu la Fumbuka, Nichukue fursa hii ya pekee kukukaribisha katika makala hii ya Biblia ni Jibu, makala ambayo hukuletea mafundisho mbalimbali yahusuyo Biblia tangu kuumbwa kwa Mwanadamu, Historia ya Ukombozi na Maisha mapya baada ya hapa duniani kupitia katika kitabu cha Ufunuo, lakini pia kupitia makala hii utapata majibu ya maswali mbalimbali yahusuyo imani kwa misingi ya Biblia kama jina lenyewe lisemavyo “Biblia ni Jibu”
Leo katika Makala hii ninakuletea Maandalizi ya Msingi yapaswayo kufanyika kabla ya Kusoma Biblia ili utakapoisoma uielewe na kuweza kuiishi. Usisome Biblia kimazoea jipange kwanza kwa kuzingatia yafuatayo;-
1.    Mwamini Yesu Kristo
Msomaji wa Neno la Mungu ni lazima amwamini Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wake, mtu asiyemwamini Yesu hawezi kukubali wala kuamini Neno la Mungu (1 Wakorintho 2:14). Kwa hiyo, Wokovu ni kwa njia ya Imani peke yake katika Kristo (Waefeso 2:8-9). Roho wa Mungu huwawezesha wasomaji wa neno wapate kuelewa vitu vya Rohoni.

2.    Kubali Kwamba Biblia Ina Pumzi Ya Mungu.
Neno la Mungu linajisema lenyewe kwamba lina pumzi ya Mungu (2 Timotheo 3:16-17). Kusoma neno la Mungu ni lazima uanze kwa kushukuru ukweli wa neno. Haihitajiki imani kubwa sana bali ni kukubali ukweli kwamba Biblia ni kweli na haina mapungufu.

3.    Mwombe Mungu
Maombi ni muhimu katika kuyaelewa maandiko. Neno la Mungu linatuelekeza kwamba ikiwa mmoja wenu atapungukiwa na hekima na aombe dua kwa Mungu awapaye wote kwa ukarimu wala hakemei naye atapewa. (Yakobo 1:5). Pia Katika Yohana twasoma “na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atusikia” (1 Yohana 5:14).Pia twasoma Mathayo 7:7-8.

4.    Jifunze Kwa Juhudi Na Uvumilivu
Kwa kuwa kurasa nyingi za maneno ya Mungu wakati mwingine hazieleweki unaposoma, jitihada na uvumilivu vinahitajika katika kujifunza neno la Mungu (2Tim 2:15), Kwa kuwa sisi ni wanadamu wenye ufahamu mfupi, maandiko yanasema; jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari ukilitumia kwa halali neno la Kweli.

5.    Jipatanishe na Mungu
Ni vizuri kuungama dhambi zako kila wakati ili umruhusu Mungu asafishe maisha yako, ili kwamba ushirika wako na Mungu udumu (1Yohana 1:6-10). Tunapotambua kukiri dhambi zetu na kuziungama inatufanya sisi kuwa waangalifu na kila namna ya dhambi katika kufikiri, kunena au katika kutenda na hivyo tunashinda.

6.    Ishi Kwa Kufuata Mapenzi Ya Mungu
Bwana Yesu alisema “Mtu akipenda kuyatenda mapenzi ya Mungu yake atajua habari ya yale mafunzo kwamba yatoka kwa Mungu au kwamba mimi nanena kwa nafsi yangu tu. Ujuzi huleta majivuno bali upendo hujenga. (1Kor 8:1).

Mpendwa Msomaji, Neno la Mungu ni chakula cha Roho zetu hivyo kulisoma na kuliishi hutufanya tuimarike kiroho, hayo yatawezekana tu kwa kujipanga na kufuata hiyo misingi niliyoielezea hapo juu. Tusikubali kusoma biblia kimazoea.

Twasoma:

"Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza"
_ (Luka 14:28-30)

Imetayarishwa na:   James Waibina

Kwa Maoni /Ushauri: Tuwasiliane kupitia

0713515059- (WhatsApp) au  jameswaibina@fumbuka.co.tz

*************************************MBARIKIWE******************************
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 blogger-facebook:

Post a Comment

Item Reviewed: MAKALA: Mambo ya Msingi ya kuzingatia kabla ya kusoma Biblia Rating: 5 Reviewed By: Unknown