728x90 AdSpace

­
Latest News
March 9, 2017

Tafakari ya Neno la Kwanza (1) alilotamka Yesu Akiwa Msalabani


Karibu Mpenzi Msomaji na mfuatiliaji wa Tafakari Zetu katika Blog Yetu ya Fumbuka..

Katika kipindi hiki cha Kwaresima tunapotafakari Mateso na Kifo cha Yesu Kristo Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu, leo tunakuletea Tafakari ya Maneno Saba (7) aliyoyatamka Yesu akiwa Msalabani wakati akisulubiwa.

Namba saba, kama ilivyo namba arobaini katika desturi za Kiyahudi ina maana ya utimilifu au ukamilifu. Namba saba inathibitisha kuwa kitu ni kamili au kinajitosheleza.

Karibu Tutafakari kwa pamoja maneno saba ya Yesu msalabani:

(I) “BABA UWASAMEHE, KWA KUWA HAWAJUI WATENDALO”

Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. Yesu akasema, “Baba, uwasamehe, kwa hawajui watendalo.” Wakagawana mavazi yake, wakapiga kura. -(Luka 23:33-34)

Neno la kwanza la Yesu msalabani lahusu msamaha. Msamaha ni tabia kuu ya Mungu. Ukuu wa Mungu haupo tu katika kazi kubwa na ajabu ya uumbaji, bali pia ukuu wake upo katika sifa yake ya kusamehe.

Neno hili ni habari njema ya wokovu. Inatosha neno hilo moja la msamaha kumtambua Yesu kuwa ni mkombozi. Kazi yote ya kuhubiri na kufanya miujiza ilikuwa inahusu msamaha.

Msamaha ndiyo hasa ujumbe mkuu wa mafundisho yote na miujiza yote ya Yesu. Mafundisho yote ya Yesu yalimwelekeza Mungu kuwa ni Baba mwenye huruma, mafundisho hayo yalimwelekeza mwanadamu atumie vizuri tabia hiyo kuu ya Mungu kwa kuomba msamaha.

Miujiza yote ya Yesu ilihusu msamaha wa dhambi; ndiyo maana wengi ambao aliwafanyia miujiza aliwaambia, umesamehewa dhambi zako.

Pia neno hili la kwanza la Yesu msalabani linatufundisha kuwa jambo la kwanza kabisa kwetu sisi katika kuhusiana na Mungu ni kuomba msamaha.

Mara nyingi sisi mbele ya Mungu tunaomba mambo mengine ambayo tunaamini kuwa ni mazuri na tunasahau kuomba jambo kuu kuliko yote mbele ya Mungu. Leo Yesu anatufundisha jinsi ya kuomba mbele ya Mungu.

Yesu anatuonea huruma sisi wanadamu anavyotuona tunatenda dhambi; ndiyo maana anasema hatujui tutendalo. Ni kweli kabisa! Tunapotenda dhambi hatujui tundendalo kwani sisi asili yetu ni Mungu; tuliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Tunapotenda dhambi tunaifuta sura na mfano wa Mungu ili tufanane na ibilisi.

Lakini, Yesu anatufundisha pia kuwa nasi kati yetu yatupasa kuombana msamaha. Katika mafundisho yake anasema:
Iweni na huruma kama Baba yenu wa mbinguni alivyo na huruma-(Luka 6:36)

Hata tunaposali, Yesu anatufundisha kuwa Mungu atatumia kipimo kilekile tunachotumia sisi kusameheana kati yetu:
Utusamahe makosa yetu kama na sisi tunavyowasamehe wale waliotukosea.

Yesu anatufundisha tusameheane siku zote, katika lolote na mara zote:
Kisha Petro akamwendea akamwambia, “Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe?” Hata mara saba? Yesu akamwambia, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.”-(Mathayo 18:21-22)

Amri kuu ya Mungu ni upendo. Kielelezo kikuu cha upendo ni msamaha. Yesu ametufundisha kupendana, na yeye mwenyewe anakuwa mfano mzuri kwa kutangaza msamaha pale msalabani. Mkristo asiyejua kusamehe, huyu bado hajawa mkristo. Yesu anasema;
mkipendana kati yenu, wote watajua kuwa ninyi ni wafuasi wangu.

Kwa hiyo, kitambulisho cha ukristo ni upendo; kitambulisho cha upendo ni msamaha. Tena, Yesu katika mafundisho yake, anasisitiza tuwapenda hata maadui zetu na tuwaombee ili tuweze kuwa kweli wana wa Mungu.

“Mmesikia kwamba imenenwa: Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia: Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je, nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je, nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakauwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” -(Mathayo 5:43-48)

Yesu ni mfano mzuri kwetu kwani pale msalabani anawasamehe adui zake wanaomsulibisha na anawaombea msamaha kwa Mungu. Hakika Yesu ni mwalimu halisi kwani kile alichofundisha kwa maneno, yeye mwenyewe ametekeleza kwa matendo.

Msamaha una pande mbili: kuomba msamaha na kutoa msamaha. Kati ya haya mawili ni lipi gumu zaidi?

Jiulize; wewe waweza kumsamehe mtu kwa lolote alilokufanyia?

Kumbuka: kutenda dhambi ni ubinadamu; kusamehe ni umungu.

Nakutakia Tafakari Njema.

Katika Makala Ijayo tutatafakari Neno la Pili la Yesu Akiwa Msalabani….

Ee Yesu tunakuabudu na tunakushukuru; Kwa Kuwa Umewakomboa Watu kwa Msalaba Wako Mtakatifu.
**********************************************************************
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 blogger-facebook:

Post a Comment

Item Reviewed: Tafakari ya Neno la Kwanza (1) alilotamka Yesu Akiwa Msalabani Rating: 5 Reviewed By: Unknown