Jumuiya ya
Kikristo Tanzania (CCT) imetoa tamko zito ikieleza kushangazwa na kauli ya Rais
Jakaya Kikwete ya kupinga mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba
iliyotokana na maoni ya Watanzania na kusema kitendo hicho kimeishusha hadhi
Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyoiteua.
Tamko hilo
la CCT ni mwendelezo wa lawama ambazo Rais Kikwete amekuwa akitupiwa na taasisi
na watu mbalimbali kutokana na mchakato wa kuandika Katiba Mpya kwenda mrama
baada ya Mkuu huyo wa nchi kueleza maoni yake dhidi ya mapendekezo ya muundo wa
Serikali ya Muungano wakati akilihutubia Bunge la Katiba.
Miongoni mwa
watu waliojitokeza kuzungumzia kauli hiyo katika siku za karibuni ni aliyekuwa
Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, Maaskofu wa Kanisa Katoliki, katibu Mkuu
wa Chadema, Dk Willbrod Slaa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif
Sharrif Hamad.
Jana(Julai 14,2014),
CCT iligongelea msumari juu ya lawama hizo ikifananisha kauli ya kiongozi huyo
aliyoitoa Machi 21,2014, wakati akifungua Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma
na Mama anayeamua kubeba mimba na kujifungua kwa uchungu, kisha kumtelekeza
mtoto, badala ya kumfurahia.
Pia katika
tamko lake ,Jumuiya hiyo imewataka wajumbe wa Bunge hilo kuheshimu maoni ya
Watanzania yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kuacha kujadili maoni ya vyama
vyao vya siasa.
“Inashangaza
jinsi chama kimoja cha siasa kinavyolazimisha wabunge na wanachama wake
kukubaliana na mapendekezo yake ambayo yanapingana wazi na yaliyomo katika
rasimu ya Katiba,” linaeleza tamko hilo lililotolewa baada ya Mkutano wa 48 wa
Halmashauri Kuu ya Jumuiya hiyo uliofanyika Julai 2 na 3 mjini Dodoma.
Tamko hilo
pia limetaja mambo mengine saba yanayolikabili Taifa.
Kabla ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba kutoa
rasimu ya pili ya Katiba Desemba 30,2013, CCM ilisambaza waraka kuwaarifu
wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka CCM kuwa msimamo wa chama hicho tawala ni
Muungano wa serikali mbili, tofauti na mapendekezo ya wananchi yaliyo kwenye
rasimu hiyo ambayo yanataka serikali tatu.
Licha ya
mara kadhaa Jaji Warioba kutetea kile kilichopendekezwa na Tume yake, wajumbe
hao kutoka CCM wameyapinga maoni hayo na kusisitiza kuwa yanaweza kubadilishwa
kadri Bunge la Katiba litakavyoona inafaa.
Kitendo
hicho kilisababisha wajumbe kutoka vyama vingine kuunda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA), ambao Aprili 16,2014, uliamua kususia vikao vya Bunge hilo
ukitoa masharti kuwa utarejea Bungeni kama chombo hicho cha kuandika Katiba
kitajikita kujadili mapendekezo ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya
Jaji Warioba.
Bunge hilo
litaendelea na vikao vyake Agosti 5,2014 na mwenyekiti wake, Samuel Sitta
anahaha kushawishi UKAWA walegeze msimamo wao.
Katika
hotuba yake ya kufungua Bunge la Katiba, Rais Kikwete aligusia mambo kadhaa
yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha
kuwa mengine hayawezekani kutekelezeka, ikiwa ni pamoja na muundo wa serikali
tatu kwa maelezo kuwa idadi ya watu waliotaka muundo huo ni ndogo.
“Tunampongeza
Rais Jakaya Kikwete kwa kutoa wazo la kuandikwa kwa Katiba Mpya na kuteua
wajumbe wa Bunge la Katiba. Tunaamini kilichoandikwa katika Rasimu hiyo
alikikubali na kubariki kutolewa kwa rasimu hiyo kwa sababu alijua ndiyo maoni
ya wananchi,” linasema tamko hilo.
“Pia
tunaamini kuwa mwenye kutoa hoja (Rais Kikwete) alikuwa na uwezo wa kuzuia
rasimu hiyo isitolewe endapo kuna ibara ambayo ina mwelekeo ambao ungekuwa
hatari kwa mustakabali wa taifa letu.”
Jumuiya hiyo
imesema kitendo cha Rais Kikwete kupingana na kilichomo katika rasimu ya Katiba
kimeshusha hadhi ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Hotuba hiyo
ilishusha hadhi ya kazi nzuri iliyofanywa na wajumbe wa Tume ambao waliteuliwa
na rais mwenyewe kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi,” linasema tamko
hilo.
“Jambo hili
linaweza kufananishwa na mama anayeamua kubeba mimba, kuilea mimba hiyo kwa
gharama na kujifungua kwa uchungu halafu mtoto akishazaliwa, badala ya kufurahi
anaamua kumtelekeza.”
Ushauri kwa
Vyama.
Tamko hilo
linasema: “Viongozi wa vyama vya siasa na wabunge waheshimu uhuru wa mawazo ya
wanachama wao hata kama watatofautiana katika hoja moja au nyingine na
wasitumie nafasi zao kulazimisha wanachama wote kukubaliana na mawazo yao.”
Jumuiya hiyo
imeifananisha hatua hiyo na udikteta kwa wanachama wa chama husika.
“Katika
jambo hili CCT inahimiza wabunge wote waangalie masilahi ya kitaifa kwa upana
zaidi na siyo ya vyama vyao.”
Inasema
licha ya kuwa wakati wa kutoa maoni CCT ilipendekeza muundo wa serikali moja,
inakubaliana na pendekezo la kuwapo serikali tatu kwa sababu ni maoni
yaliyotolewa na wananchi walioamini kuwa zitamaliza kero za muungano.
Lugha za
Kejeli.
Katika tamko
hilo, CCT imeshangazwa jinsi vikao vya Bunge la Katiba vilivyotawaliwa na mjadala
wa muundo wa serikali, huku mambo mengine ya msingi yaliyomo katika rasimu ya
Katiba yakiwekwa.
“Lugha
zisizo za kiungwana zinazotolewa na baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba kwa
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba zinaonyesha ni jinsi gani wabunge hao
wasivyoheshimu uteuzi wa wajumbe wa Tume hiyo,” linasema tamko hilo.
Katika tamko
hilo, CCT pia iligusia suala la udini, maadili, kukosekana kwa uvumilivu wa
kisiasa nchini, mauaji ya raia, uchaguzi, umasikini na ulipaji wa kodi, hasa
kwa mashirika ya dini.
0 blogger-facebook:
Post a Comment