Kwa Ufupi.
- Ni vyema kuacha kususa vikao vya Bunge la Katiba na kufanya majadiliano.
- Awataka Ukawa kuacha kususia Bunge la Katiba, asema busara zaidi zinatakiwa kutumika kupitia majadiliano kwa lengo la kumaliza mgogoro uliopo.
Aliyekuwa
msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa amesema Rais Jakaya Kikwete
aliteleza kueleza msimamo wake na ambao baadaye ulibainika kuwa wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba, Machi 21,2014.
Tendwa, ambaye
alistaafu Agosti mwaka jana na nafasi yake kuchukuliwa na Jaji Francis Mutungi,
alitoa kauli hiyo jana(Julai 10,2014) katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini
kwake jijini Dar es Salaam.
Tendwa,
ambaye alikuwa Msajili kwa miaka 13, alisema akiwa kiongozi mkuu, Rais Kikwete
alipaswa kutoa mwongozo wa uendeshaji wa Bunge Maalum la Katiba.
“Sikuwapo
nchini, lakini kwa kadri ninavyoelezwa, kama hiyo ni kauli yake, basi
alijisahau kusemea msimamo wa chama chake, (CCM) na sera yake ya serikali mbili
katika bunge hilo,” alisema.“
Rais ni
mtendaji, alipaswa kutoa guidelines (miongozo) ya jinsi ambavyo Bunge Maalum la
Katiba linatakiwa kufanya.
Alichokisema,
aliteleza.“Alijisahau na kurudi kwenye chama kwa sababu hiyo ndiyo sera ya
chama chake, ” alisema Tendwa.
“Na siyo
yeye tu (Kikwete) kwani nimemsikia hata Dk Shein (Rais wa Zanzibar na
mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi), akisema kuwa msimamo wa CCM ni serikali
mbili,” aliongeza Tendwa.
“Nimemsikia
Makamu wa Pili wa Rais (Balozi Seif Ali Iddi) akisema hivyo na Rais
wangu (Kikwete) katika mikutano mbalimbali ya hadhara, naye amelisema hilo.”
Madai ya kuibeba CCM.
Tendwa ambaye katika uongozi wake wa miaka 13 alikuwa akituhumiwa mara kwa mara na vyama vya upinzani kuwa anakibeba chama tawala, alisema: “Nadhani na yeye (Rais Kikwete) kasema. Nadhani alijisahau kuwa ni kiongozi wa taifa.”
“Rais ni mtendaji na mimi nasema aliteleza. Turudi katika hoja kwa kujadili rasimu iliyoko mezani.”
Kauli hiyo
imekuja kipindi ambacho baadhi ya viongozi wakiwamo wa vyama vya siasa nchini,
Dk Wilbroad Slaa (Chadema), Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif
Shariff Hamad na pia aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba, pia kumkosoa Rais Kikwete.
Kwa nyakati
tofauti, wameeleza kuwa Kikwete ndiye mtu pekee anayeweza kutuliza mvutano
ulioibuka katika mchakato huo unaoendelea kwenye Bunge la Katiba.
Ulikoanzia Mzozo.
Machi 21,2014
wakati akifungua Bunge Maalum la Katiba, Rais Kikwete aliipinga Rasimu ya
Pili ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba, akigusia mambo saba ya
msingi yaliyomo katika rasimu hiyo na kutaka yatazamwe kwa kina, kubainisha
kuwa mengine hayawezi kutekelezeka.
Miongoni mwa mambo hayo ni muundo wa Muungano kuwa wa serikali tatu uliopendekezwa katika rasimu hiyo.
Kikwete,
ambaye alisema anatoa maoni yake binafsi, alipinga waziwazi pendekezo la
serikali tatu na kuegemea katika muundo wa serikali mbili unaoungwa mkono na
CCM, huku akifafanua kuwa idadi ya watu waliopendekeza muundo wa serikali tatu
ilikuwa ndogo.
Walilosema Wengine.
Julai 7,2014, wakati akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na televisheni ya ITV, Maalim Seif alimtupia lawama Rais Kikwete kuwa amechangia kuukoroga mchakato wa katiba kwa kufuata msimamo wa chama chake, badala ya maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu ya pili ya katiba.
Maalim Seif, ambaye alilenga kauli iliyotolewa na kiongozi huyo wa nchi wakati akifungua Bunge la Katiba, alisema kauli ya Rais Kikwete imeondoa imani ya wananchi kuhusu kupatikana kwa katiba inayotokana na maoni yao.
Alisema
mchakato huo hivi sasa unamtegemea Rais pekee, huku akisisitiza kuwa hakuna
binadamu aliyekamilika na kumshauri kutafuta uwezekano wa kuweka mambo sawa,
ili kujenga tena imani kwa wadau wote.
Julai 4,2014, Dk
Slaa, wakati akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jijini Dar es
Salaam, alimtaka Rais Kikwete kujitokeza hadharani kutafuta suluhu ya kupata
mwafaka wa mchakato wa Katiba Mpya kwa kuwa hakuna mamlaka nyingine zaidi
inayoweza kuunusuru.
Naye Jaji
Warioba kwa nyakati tofauti amemshauri Rais Kikwete kuchukua hatua
zitakazoondoa matatizo katika Bunge la Katiba ili kuwezesha mchakato huo
kukamilika.
Alisema ni
muhimu kiongozi huyo mkuu wa nchi kuweka kando tofauti za mawazo na mitazamo
ili kupata Katiba Mpya kwa masilahi ya Taifa.
Mwanzoni mwa
wiki, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya na naibu waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Godfrey Zambi alifichua kuwa msimamo wa serikali mbili unaoonyeshwa
na wabunge wa chama hicho ni maagizo ya Kikwete.
Awashauri UKAWA.
Kuhusu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Tendwa aliwashauri wajumbe wote wanaounda umoja huo kurejea bungeni ili kujadili vipengele vinavyogusa maslahi ya wananchi na kuweka kando sura ya kwanza na sita zinazohusu muundo wa Serikali.
Aliwataka
wajumbe wanaounda Ukawa kuacha kususia vikao na kutoka kwenye Bunge
la Katiba kama walivyofanya tangu Aprili 16,2014 na kusema kuwa busara zaidi ndizo
zinazotakiwa kutumika kupitia majadiliano kwa lengo la kumaliza mgogoro
uliopo na kuwezesha mchakato kuendelea.
Alisema
rasimu siyo katiba bali ni andiko linaloweza kubadilishwa na kuvunjwa vunjwa,
hivyo wajumbe wa Ukawa warudi bungeni na kuandaa rasimu ya katiba itakayokwenda
kupigiwa kura na wananchi.
“Unatoka nje
na unasema hurudi, wewe ni nani? Kunahitajika hapa uvumilifu wa kisiasa.
Watu hawa
(Ukawa) na wengine wanatakiwa kuaminiana katika mchakato huu. Warudi bungeni
wajadili vifungu vya katiba vinavyowagusa wananchi.
“Wasijadili
pekee muundo wa Muungano, wajadili vifungu vinavyohusu wananchi, kisha
iandikwe rasimu itolewe kwa wananchi kwa muda mwafaka na wao waende
huko wawaelimishe ili wafanye uamuzi sahihi.
“Hoja ya
msingi iwe upigaji kura uwe wa serikali mbili au tatu kwa kuwa vifungu vingine
vimekwishaafikiwa,” alisema Tendwa.
Aliongeza
kuwa inashangaza kuona tangu wajumbe hao watoke bungeni ofisi ya msajili wa
vyama vya siasa haikutakiwa kuendelea kukaa kimya kuhusu Ukawa wanaojitangaza
kinyume cha kanuni na sheria.
“Ofisi
hiyo (ya msajili) imekuwa kimya, haisemi lolote kuhusu Ukawa. Hawana uhalali wa
kisheria na mamlaka. Kwa hiyo msiwakuze bure bila sababu ya msingi kwani
hatujui wameanzia wapi, mizizi yao ipo wapi,” alisema.
Kuhusu
lugha inayotumiwa na wajumbe kwenye Bunge la Katiba, Tendwa alisema ni ya
mitaaani na wakati mwingine watoto hutumia lugha nzuri kuliko ya wabunge hao.
“Lugha ya
matusi kuingizwa bungeni ni aibu. Hata watoto hawafanyi hivyo, lakini wabunge
tunaowategemea kabisa ndio wamekuwa wakitumia maneno ya kibabe na kejeli.
Wanatakiwa
kujifunza kuwa wanapoingia bungeni lazima lugha za mitaani waziache nje,”
alisema.
Bunge la
Katiba linatarajiwa kuendelea tena Agosti 5,2014, huku kukiwa na wasiwasi kama
wajumbe wa Ukawa watarejea au la baada ya kususia vikao hivyo.
Mwenyekiti
wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta tayari ameitisha kikao cha Kamati ya
Mashauriano chenye wajumbe 27 kitakachofanyika jijini Dara es Salaam Julai 24
kwa lengo la kuinusuru katiba hiyo na kuwashawishi Ukawa kurejea bungeni.
Wakati
akistaafu, Tendwa alisema anajivunia kuifanya ofisi ya Msajili iwe ya kisasa,
akisema aliteuliwa bila ya kupewa adidu za rejea na alitegemea kuwa ofisi hiyo
ingekuwa na wanasheria, lakini alijikuta mtu pekee mwenye taaluma hiyo.
0 blogger-facebook:
Post a Comment