Mpendwa mwana wa Mungu, ninakuletea Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu ikiwa ni Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristu. Sherehe hii ni kati ya sherehe za Bwana na huadhimishwa Dominika inayofuata mara baada ya sherehe ya Utatu Mtakatifu.
Ni sherehe ambayo ina uhusiano wa moja kwa moja na Alhamisi kuu ambapo Fumbo la Ekaristi Takatifu linawekwa katika Kanisa na Yesu Kristu mwenyewe. Siku ya Alhamisi Kuu hatukupata nafasi ya kusherehekea hasa kwa shangwe na nderemo kwa kuwa tulikuwa tayari katika Juma Kuu, Juma la Mateso ya Bwana. Kumbe, Mama Kanisa anatujalia nafasi tena ya kusherehekea na kushangilia kwa vigelegele sherehe hii hivi leo.
Ndiyo kusema katika sikukuu hii tunafanya ukumbusho wa Karamu ya mwisho, ambapo Bwana alikula karamu hiyo pamoja na wanafunzi wake. Ni katika karamu hiyo aliweka sakramenti ya Ekaristi na sakramenti ya Upadre. Mama Kanisa hufanya maandamano katika siku hii ikiwa ni ishara ya ushuhuda wa imani akitangaza ukuu wa Mungu kwa mataifa ambao hujidhihirisha kwa njia ya Ekaristi Takatifu. Ni ishara ya shukrani kwa Mungu kwa ajili ya zawadi ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristu. Ekaristi Takatifu ni chimbuko la Kanisa na hivi tunasherehekea na kushangilia zawadi ya Kanisa kama Safina ya wokovu.
Mpendwa mwana wa Mungu, tunaposherehekea Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana kwa shangwe Mama Kanisa atuwekea Neno la Bwana akitaka polepole kutambua hicho tunachokisherehekea kuwa ni kitu cha thamani kuu. Bwana anasema “twaeni mle na mnywe wote huu ndio mwili na hii ndiyo Damu yangu itakayomwagika kwa ajili ya wengi”. Mwinjili Yohane akikazia na kuleta maana ya maneno haya anamnukuu Bwana akisema “mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni, mtu akila chakula hiki ataishi milele”.
Mpendwa mwana wa Mungu, maneno haya tunayapata katika sura ya 6 ya Injili ya Yohane ambayo ni mahubiri juu ya mkate wa uzima. Katika sura hiyo ya 6 Bwana anaanza na mwujiza wa ongezeko la mikate na samaki ambapo aliwalisha watu 5000 wanaume tu, kumbuka wanawake na watoto hawakuhesabiwa, kumbe walikuwa zaidi!
Walipokwishamaliza kula walikusanya mabaki vikapu 12 na neno juu ya hili: hakika huyu ndiye Nabii anayekuja ulimwenguni. Muujiza huu ulionesha upendo wake kwa watu na kwa namna hii alitangaza kuwa ataweka kitu kingine zaidi ya hicho anapomalizia kazi yake ya kitume hapa duniani. Kukusanya vikapu 12 mabaki, tayari kunaashiria kutoisha kwa Ekaristi Takatifu atakayoiweka baadaye.
Hawa watu aliowalisha kwa mikate na samaki baadaye walitaka kumfanya awe mfalme na hapa ndipo anagundua ufinyu wa mawazo na mwono wao na hivi anataka wasonge mbele toka hatua hiyo na kukifanyia kazi chakula kisichoharibika yaani chakula cha uzima wa milele-ndiyo Ekaristi Takatifu Mwili na Damu yake.
Katika majadiliano, Bwana alipokwisha kuwaambia chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu, wanauliza hivi awezaje kutupa mwili wake mtu huyu tuule? Ni kweli maneno ya Bwana ni magumu kama yale aliyomwambia mwanamke msamaria yaani yakumpa maji ya uhai na mwanamke anashangaa! (Yn 4:14-15).
Kwetu sisi leo maneno kama mkate wa mbinguni ni rahisi kuyaelewa yaani Neno la Mungu ambalo hujifungamanisha na maisha yetu katika Yesu Kristu mwenyewe. Ndiyo kusema Yesu ndiye mkate wa uzima. Tunampokea Bwana na anakuwa maisha yetu na hivi tunazaliwa upya katika upendo kwa wengine na hii ndiyo maana ya Ekaristi Takatifu.
Bwana anasonga mbele katika mahubiri yake akisema aulaye mwili wangu na kuinywa Damu yangu anao uzima wa milele na atafufuliwa siku ya mwisho. Kama vile yeye ambavyo alikufa na kufufuka basi aulaye mwili wake anajiunganisha na yeye na kujipatia asili ya Bwana, anajitoa yeye mwenyewe kwa ajili ya Bwana ili aweze kuendelea kuteseka, kujitoa na hatimaye kufufuka katikati ya maisha yetu.
Katika hili tunamwona Mtakatifu Paulo akisistiza kwamba kabla ya kula mkate huu mtakatifu lazima kujichunguza kwanza ili kuona kama anastahili kweli na hivi kuweza kuruhusu Kristu aendelee kuishi ndani mwake na katika jumuiya (1Kor 11:28) Katika hili lazima kutambua kuwa kabla ya Ekaristi lazima kujiandaa kiimani, kama kweli tunataka kugeuzwa na kuwa Kristu mwingine.
Katika hali ya kawaida mkristu hapokei Ekaristi bila kusikia Neno la Mungu, ambalo kwanza huangaza maisha yake na humfanya aingie katika ulimwengu wa Kristu, ndiyo kusema lazima kwanza agundue nani ni Kristu, anasema nini, anafundisha nini na akisha kumpokea Kristu anataka nini baadaye katika maisha ya watu na jumuiya kwa ujumla. Bila hili ni vema tukasubiri kwanza kabla ya kuanza kuandamana.
Katika Fumbo la Ekaristi, ipo hatua nyingine muhimu kadiri ya utamaduni wa kanisa tangu zamani. Hatua hii ni ile ya kumwabudu Bwana, ni hali ya kukaa mbele ya Ekaristi Takatifu Kristo mwenyewe na kumweleza hali yako, kumsifu na kumtukuza ukichota nguvu kwa ajili ya maisha ya pamoja katika jumuiya. Mmoja huenda pale mbele ya Bwana aliyeupendo vunjika ili apate naye kuwa kipande cha upendo kwa wengine. Hali ya kuabudu na kusifu huwa yenye kuzaa matunda kama tunashiriki Misa Takatifu yaani maadhimisho ya kijumuiya, ndiyo maana katika sherehe hii huanza Misa na baadaye kusifu na kuabudu.
Tunapopokea Mwili na Damu ya Bwana, tunapokea mwanga katika maisha yetu maana alisema mimi ni taa ya maisha yako, ni ukweli na uzima kumbe pia twahuishwa na Bwana anayetaka toka maisha hayo tukafanye vivyo hivyo daima mpaka ajapo. Anatualika kwa njia ya Ekaristi tuishi uhuru wa wana wa Mungu aliotupatia Bwana (Lk. 4:18 na kuendelea).
Tunaalikwa kukumbuka Wana wa Israeli walipopatwa na taabu jangwani, ilikuwa ni “neno la Mungu” lililowaletea manna hukohuko jangwani.
Chakula hiki kilikuwa ni chakula kipya kabisa. Ndiyo kusema mwandishi ataka kusema kuwa Neno la Mungu ni nguvu na nyenzo ya kutatua matatizo mbalimbali katika maisha yetu, hata kama tutakuwa tumekata tamaa. Hali hii ndiyo ambayo tunaipata katika sehemu ya Injili ya leo.
Ndugu Mkristu, Mtakatifu Paulo anapowaandikia Wakorinto anakuja na Ekaristi Takatifu kama chimbuko na ndilo chimbuko la umoja. Anakemea utengano uliopo kwa sababu ya fikra tofauti maana wengine walikuwa wamebaki na mawazo ya kipagani. Anasema “Je, Kikombe kimoja tukibarikicho si ushirika wa Damu ya Kristu? Mkate tuumegao Je! Sasa ya nini kuhukumiana na ufukuzana katika jumuiya? Je, inawezekanaje katika vurugu kama hizo tukaketi na kunywea kikombe kimoja?
Basi Mtakatifu Paulo anakemea hilo katika jumuiya Wakorinto na jumuiya yako hivi leo. Yafaa kwa hakika katika adhimisho hili la sherehe ya Mwili na Damu kujifunza mapendo na huruma, msamaha na upole ili Kristu aishi ndani mwetu nasi tuishi ndani mwake.
Mpendwa msikilizaji, tunaposherehekea tunapaswa kufikiri kwa undani sana nini maana ya fumbo hili kuu na mwisho lazima, tafakari yetu imalizikie katika neno moja “PENDANENI KAMA NILIVYOWAPENDA NINYI”. Ninakutakieni furaha tele nikikukumbusha maneno ya Bwana “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu hadi nitakaporudi”. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.
0 blogger-facebook:
Post a Comment