728x90 AdSpace

­
Latest News
September 9, 2014

WAZIRI MKUU MH. PINDA AWATAKA WANASHERIA WAWAFIKIRIE KWANZA WATU WA CHINI

 
Waziri Mkuu, mizengo Pinda akizungumza na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (kulia) Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Africa Mashariki (EADB), Vivianne Yeda (kushoto) na Mjumbe wa Bodi ya EADB,Khadija Simba baada ya kufungua Semina ya Wanasheria wa Serikali wa nchi za Afrika ya Mashariki  ya kuwajengea uwezo wanasheria hao katika kuchambua na kufikia mamuzi ya mikataba ya uvunaji maliasili za mataifa hayo,. Semina hiyo ilifanyika kwenye hoteli ya White sands jijini Dar es salaam Septemba 9, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka wanasheria kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki waweke mbele maslahi ya wananchi wa kawaida wakati wanapoingia mikataba na wawekezaji kwenye sekta ya madini.

Ametoa wito huo leo mchana (Jumanne, Septemba 9, 2014) wakati akifungua semina ya siku tano juuya mafunzo ya kuingia makubaliano na mikataba kwenye sekta ya madini kwa wanasheria wa sekta ya umma kutoka nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ulioanza leo kwenye hoteli ya Whitesands jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na washirki wa mkutano huo kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania, Waziri Mkuu Pinda alisema wanapaswa wawajali sana wananchi walio maskini kwa sababu wao hawana fursa ya kuingia kwenye vikao kama vyao na kutoa sauti juu ya kile wanachokitaka.

“Muwapo ofisini kwenu au kwenye miji yenu mikuu, mnapojadiliana na wawekezaji na kufikia makubaliano kuhusu rasilmali za nchi, siku zote muwafikirie hawa watu wa chini, walio maskini ambao ni wengi na wako nje ya majengo yenu.”

“Wao ndiyo wadau wakuu lakini hawana uwezo wa kuingia kwenye vikao kama hivi, sote tunatambua kwamba wameishi na hizo rasilmali kwa vizazi vingi tu. Licha ya umaskini wao, wanaishi juu ya ardhi ambayo chini yake kuna utajiri tele wa madini na rasilmali nyingine.  Ninawasihi sana muwafikirie watu hawa kabla ya kufanya maamuzi yoyote,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Alisema ili jambo hilo liweze kufanikiwa ni lazima, wanasheria kama wadau wa mwanzo kabisa, wakubali kukataa pokea fedha chafu na vishawishi kutoka kwa wawekezaji na siku zote waweke uzalendo mbele kwa maslahi ya nchi zao.

“Rasilmali za bara la Afrika hazijaleta maendeleo kwa wakazi wakazi wa bara hili kwa sababu wanaofaidika ni makampuni makubwa kutoka nje na watu wachache sana wenye nafasi huku walio wengi wakiambulia patupu. Ni theluthi moja tu ya mikataba ya uchimbaji madini inayolifaidisha bara zima la Afrika ikilinganishwa na faida ambayo bara la Amerika Kusini inanufaika nalo.”

Ili kuepukana na hali hiyo, Waziri Mkuu alisema umefika wakati wa kukataa kutoa misamaha ya kodi kwa makampuni ya kimataifa na kuhakikisha kuwa makampuni hayo yanalipa kodi katika kila nchi husika ya Afrika Mashariki. “Natumaini hii semina itasaidia kutufungua macho katika maeneo ambayo mikataba yetu na sheria zetu zilikuwa zinalegalega, ili kuanzia sasa tuweze kunufaika na rasilmali zetu,” alisema.

Alisema umefika wakati wa kuhakikisha Serikali za nchi husika zinaweka sera madhubuti na miongozo ya kisheria itakayohakikisha mikataba inayoandaliwa kwa ajili ya utafutaji na uendelezaji wa madini na rasilmali zake inazinufaisha nchi kwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema semina hiyo ni muhimu kwa sababu wanaolengwa ni wanasheria kutoka Afrika Mashariki na Afrika ndilo eneo pekee lenye rasilmali ambazo bado hazijaendelezwa.

“Semina hii imelenga kuwafunua macho wanasheria wetu ili rasilmali zetu ziweze kuwanufaisha wananchi… ndani ya mikataba tunayoingia kuna mapungufu makubwa kwa maana ya kuwanufaisha wananchi.”

“Inawataka watambue kwamba mfanyabiashara yeyote akija ni lazima anatafuta faida. Na ukilala tu, yeye anapata faida kubwa sana. Wakienda kusaini mikataba hawa wanasheria wanapaswa kuangalia sheria za nchi husika lakini pia wanapaswa kuweka uzalendo mbele na kuacha tamaa. Wanatakiwa wafanye maamuzi kwa niaba ya wananchi,” alisema.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba alisema sekta ya madini ni mojawapo ya sekta zinazokua kwa haraka sana hapa nchini lakini inachangia chini ya asilimia moja ya ajira zote nchini.
KWA HABARI ZAIDI UNGANI NASI KWA KU-LIKE PAGE YETU YA FACEBOOK.. Bonyeza hapa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 blogger-facebook:

Post a Comment

Item Reviewed: WAZIRI MKUU MH. PINDA AWATAKA WANASHERIA WAWAFIKIRIE KWANZA WATU WA CHINI Rating: 5 Reviewed By: Unknown