Tajiri hana dhiki kama waliyonayo fukara na walala hoi wengine. Tajiri akiumwa anaweza kupata huduma popote tena kwa haraka na kwa uhakika. Mwenye mali hana sababu ya kumpigia magoti yeyote yule ili kupata msaada. Kinyume chake, mtu fukara itamlazimu kumpigia magoti tajiri ili apate msaada. Hata katika biblia ni wahitaji na fukara tu ndiyo wanaomwendea Yesu na kumpigia magoti. Mathalani, kulikuwa mtu mmoja Mgerasi aliyepagawa na shetani: “Yesu aliposhuka chomboni, mara alikutana na mtu ambaye ametoka makaburini mwenye pepo mchafu, na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia.” (Mk. 5:6). Halafu “akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsii na kumpigia magoti” (Mk. 1:40).
Lakini leo tutaona filamu mpya ya mtu tajiri mwenye „mapesa” mengi sana au mwenye „vijisenti vyake” anapiga magoti. Yesu akiwa njiani katika harakati zake za kupita huko na huko “mtu mmoja (tajiri) akaja mbio akampigia magoti.” Huyu mtu hatutajiwi jina wala umri wake, ila mwinjili Mateo anasema alikuwa kijana. Tunajiuliza kulikoni tajiri huu asiye na shida yoyote, na hatujasikia kuwa anaumwa, lakini anamkimbilia Yesu na kumpigia magoti. Yawezekana analo tatizo kama la mmojawapo tuliyewataja hapo juu la ugonjwa au kupagawa na shetani. Hebu tumfuatilie kwa karibu.
Baada ya kupiga magoti anamwuliza Yesu: “Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?” Anasema “kuurithi, kustahili, kupokea, kuwa na uzima wa milele. Na anauliza: “nifanye nini?” yaani nifanyeje ili nistahili zawadi hiyo ya uzima wa milele. Yesu anamjibu “Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu.” Kwa tamko hilo yaonekana kama vile Yesu anamwambia kuwa “Wewe unayo tayari majibu ndani mwako,” yaani binadamu anaye tayari mwalimu anayemfundisha ukweli ndani mwake. Mungu ndiye mwalimu mwema ndani ya dhamiri ya kila mtu, kwani wote tunafundishwa na Amri, Sheria au Neno la Mungu lililomo ndani mwetu.
Ndiyo maana Yesu anamworodheshea mambo hayo ambayo ni amri za Mungu zilizoandikwa dhamirini mwa kila mtu: “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, waheshimu baba yako na mama yako.” Orodha hii ya amri za Mungu haijakamilika na tena ni amri zihusuzo mahusiano kati ya binadamu tu. Kumbe amri tatu zinazomhusu Mungu zimeachwa. Hali hii inaonesha kuwa Yesu anataka kutufundisha jambo juu ya mahusiano na maelekeo yetu ya maisha, yaani namna gani sisi tunamwelekea binadamu mwenzetu na namna tunavyomwelekea Mungu, aidha pengine hatuelewi jinsi gani Mungu mwenyewe anamwelekea binadamu. Kadhalika anataka kutuangalisha kuwa makini na kile tunachokidhani kuwa ni muhimu na chema katika maisha. Kwa vile Mungu anamwelekea na kumwangalia binadamu, sisi pia yatubidi tumwelekee binadamu kwa namna ile ambayo Mungu anamwelekea huyo binadamu. Kwa hiyo kuhusu kushika amri Yesu anaona inatosha alichofanya huyu bwana.
Lakini bwana mwenyewe yaonekana hakuridhika ndiyo maana anadakiza mara moja: “Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu.” Kisha Yesu anamwangalia – kwa kigiriki emblepsas – yaani kuangalia kwa kina au kwa ndani na kumpenda. Yesu amempenda kwa sababu amemwona anayo hali na mazingira mazuri ya kumwezesha kupiga hatua ya juu zaidi katika maisha, yaani Yesu amemwona mtu huyu kuwa anakosa furaha ya dhati licha ya kufaulu kwake kuzishika amri hizo. Ili kuwa na furaha na heri kamili, kuna madai yake ambayo yabidi kuwajibika nayo, yaani kuwa waaminifu kwa maisha yaliyo ndani mwetu.
Lengo la kuwajibika huko ni utimilifu wa furaha kama anavyosema Yohane: “Mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (Yoh. 10:10) kadhalika “ili furaha yangu iwe ndani mwenu na muwe nayo haswa.” Kwa hiyo tendo la mtu huyu la kushika amri ni jema sana, lakini halimfikishi kwenye uzima wa ukamilifu wa furaha. Yesu anamwelekeza jinsi anavyoweza kuwasili au kufika katika furaha hiyo kamili. Anamwambia: “Umepungukiwa na neno moja.” Hapa tafsiri hii imeongezwa chumvi, kwani kwa kigiriki “Hen soi husterei”linamaanisha “Unakosekana na kitu” “Kuna kitu unapungukiwa.” Kisha anamwambia “Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.” Hazina ya mbinguni inamaanisha Mungu.
Yaonekana mtu huyu anashikilia amri na kutumia mali yake kibinafsi na amemkosa Mungu. Yesu anamwambia chagua moja. Uyatumie mali yako kwa ajili ya ndugu hapo utakuwa na hazina ya Mungu. Lengo la mtu huyu lilikuwa ni kutaka kuongeza mali aliyo nayo, kumbe Yesu anamwalika kushikilia jambo moja, yaani ayatoe mali yake kwa ajili ya wengine kwa upendo. Yesu hataki kumfukarisha bali kutajirisha maisha ya kibaolojia ya mtu huyu ili yaweze kuvaa maisha ya milele, ya upendo. Huo ni mpito muhimu katika ulimwengu huu kwani tumefanywa kwa ajili ya Mungu. Tusipogawa utajiri kwa wengine tutakapofika mpakani au kwenye mizani wanapokagua uzito na mali tuliyobeba yote yatanyang’anywa. Kumbe, tukigawa utajiri huo kwa wengine, mali hayo hugeuka kuwa upendo ambao ni utajiri wenye uzito unaohitajika. Hayo ndiyo maelezo ya mbingu, ndiyo maisha ya Mungu.
Bwana yule aliposikia maneno hayo, “akakunja uso” kwa Kigiriki stugnasasmaana yake ni kushtuka, kugutuka, changanyikiwa. “Akaenda zake kwa huzuni kwa vile alikuwa na mali nyingi.” Mali au pesa ina maana ili kutengeneza urafiki. Kama mmoja ni rafiki ya mali tu anakuwa mtumwa wa mali. Kwa hiyo bwana huyu alikuwa mtumwa aliyepagawa na shetani sawa tu na yule Mgerasi. Shetani alimwendesha hata hakutaka kupokea Neno la Yesu linaloweza kumpa uhuru, badala yake akaondoka huku amepagawa na shetani wa utajiri wake. Mapato yake anabaki na huzuni, mwenye uchungu, na kuhuzunika.
Ndugu zangu, moyo wa mtu umefanywa na upendo usio na mwisho kama kisemavyo kitabu cha Mhubiri. “Mungu ameweka jambo lisilo na mwisho.” Tunapokuwa watumwa wa mali hapo tunajikosesha furaha ya kweli. Hitaji la kuwania furaha isiyo na mwisho liko daima mioyoni mwetu. Kwa sababu tumeumbwa kwa ajili ya furaha. Lakini hakuna kiumbe kinachoweza kutosheleza hitaji hilo, ndiyo maana bwana tuliyemsikia leo hana jina kwani mtu huyo anawakilisha hali aliyo nayo kila mmoja wetu. Kuhuzunika kwa bwana huyu kwamaanisha alishindwa kuchukua maamuzi magumu yatakayomwongoza kwenye furaha ya kweli.
Bwana huyu alipoteza fursa ya kuwa na utu wa kuwa na uzima uliojaa upendo na furaha kama alivyotarajia, kwa sababu hakutaka kutoa maamuzi magumu. Baada tu ya kuondoka bwana yule, Yesu anaangalia huku na huko kisha anawaambia wanafunzi wake kwa masikitiko. “Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!” “Ulimwengu haumtupi mtu.” Ulimwengu unaweza kutupatia mali, lakini hauwezi kutupatia uzima wa milele. Tukitaka kupata uzima wa milele budi tutumie mali ya ulimwengu huu kwa ajili ya wengine. Kwa mara mbili Yesu anasema “ni vigumu” kupata utajiri wa kweli (uzima wa milele) huku umeng’ang’ana na utajiri wa uliwengu huu.
Kisha Yesu anatoa mfano kuonesha ugumu huo anaposema: “Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” Picha anayotaka kuitoa Yesu ni kuwa Utajiri una nguvu kali sana ya kumshawishi na kumtawala mtu. Kujinasua na utawala huo ni vigumu sana, na kunahitajika muujiza wa Roho mtakatifu, anayetupa uelewa wa uzima wa kweli, yaani pale tunapojitambua kuwa sisi ni binadamu wenye hali ya kimungu.
Petro anafikiri kisha anauliza: “Tazama sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe.” Yesu anamjibu “Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili.” Orodha hiyo ina watu au vitu saba (namba inayoonesha ukamilifu). Tena hasemi kuacha vitu hivyo vyote kwa mara moja, bali anatumia neno “au” kumaanisha kimoja wapo, yaani moja ya vitu kama hivyo kinaweza kukupagawiza kama shetani, hivi yabidi kujinasua nacho.
Kwa hiyo, mtu anayeichagua Injilli atakuwa na maisha kamili ya furaha. Yesu anaendelea kuorodhesha vitu atakavyopata zaidi katika ulimwengu huu hadi mara mia, nayo ni “nyumba, ndugu waume, ndugu wake, na mama, na watoto na mashamba pamoja na udhia; lakini baba hatamkwi kwa sababu huyo ni ishara ya utawala. Kwa hiyo katika ulimwengu wa ufalme wa Mungu hakuna ubaba, bali sisi sote ni ndugu na jamaa sawa. Inabidi kila mmoja ajihoji mwenyewe juu ya utajiri na vipawa alivyo navyo na majibu ayatoayo kwa wahitaji. Tuangalie kutoambatana na mali ya ulimwengu na kukosa furaha iliyo ndani mwetu tuliyopewa na Mungu.
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
0 blogger-facebook:
Post a Comment