728x90 AdSpace

­
Latest News
October 8, 2015

HURUMA YA MUNGU IPEWE KIPAUMBELE CHA KWANZA!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 6 Oktoba 2015 amekaza kusema, ni vigumu kwa huruma ya Mungu kuweza kupenya katika moyo mgumu wa kiongozi wa Kanisa, changamoto kwa watu kama hawa ni kuhakikisha kwamba, wanakimbilia huruma ya Mungu badala ya kujikita katika mawazo, sheria na taratibu walizojiwekea wenyewe!
Liturujia ya Neno la Mungu inaomwonesha Yona alivyokuwa na shingo ngumu kukubaliana na maagizo ya Mwenyezi Mungu, lakini hatimaye, anasalimu amri na kutoka kifua mbele kuanza kutangaza mapenzi ya Mungu, akiwataka wananchi wa Ninawi kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Kutokana na mahubiri haya, wananchi wa Ninawi wakatubu na hatimaye, wakafanikiwa kuonja huruma, msamaha na upendo wa Mungu katika maisha yao.
Lakini nabii Yona hakufurahia sana kuona Mwenyezi Mungu akiwaonjesha huruma na msamaha wananchi wa Ninawi. Alitaka Mwenyezi Mungu awashikishe adabu. Hii ndiyo historia ya maisha ya Yona anasema Baba Mtakatifu inayojikita katika sura kuu tatu: Sura ya kwanza inamwonesha Yona akikaidi utume aliokabidhiwa na Mwenyezi Mungu; Sura ya pili ni utii unaooneshwa na Yona kiasi cha kumjalia kufanya muujiza wa wananchi wa Ninawi kutubu na kumwongokea Mungu. Sura ya tatu inaonesha pia ukakasi katika kupokea huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Nabii Yona pamoja na safari yote ya maisha ya kiroho hakupenda kumwona Mwenyezi Mungu akiwasamehee wananchi wa Ninawi baada ya kutubu na kumwongokea Mungu, kwani alidhani kwamba, kazi yake ilikuwa bure. Hapa Yona aliweka mbele mawazo, sheria na kanuni zake, akasahau kuambata huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata Yesu Kristo hakueleweka vyema na watu wa nyakati zake, alipokazia kwa namna ya pekee huruma katika maisha na utume wake. Kwa njia hii akasigana na wakuu wa Makuhani na Walimu wa sheria. Walishindwa kuelewa kwanini Yesu alimsamehe yule mwanamke aliyefumaniwa akizini! Wakashikwa na bumbuwazi kumwona akila na kushirikiana na watoza ushuru pamoja na wadhambi.
Wote hao walisahau kwamba, huruma na msamaha vilikuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Yesu, jambo linalojidhihirisha kwa namna ya pekee hata katika Zaburi, inayowaalika waamini kumngoja Bwana kwani Bwana ni mwingi wa huruma na msamaha, kwake wokovu unapatikana. Baba Mtakatifu Francisko anawataka viongozi wa Kanisa kuwa na moyo wa wenye huruma na mapendo na kamwe wasiifanye mioyo yao kuwa migumu kiasi cha huruma ya Mungu kushindwa kupenya katika maisha ya watu; changamoto katika maisha, utume na huruma ya Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya kuzindua na hatimaye kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, iwe ni fursa ya kumwomba Yesu Kristo ili aweze kuwasaidia waja wake kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anataka rehema na wala si sadaka. Waendelee kuomba  Mwenyezi Mungu ili awakirimie huruma, aponye dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 blogger-facebook:

Post a Comment

Item Reviewed: HURUMA YA MUNGU IPEWE KIPAUMBELE CHA KWANZA! Rating: 5 Reviewed By: Unknown