Askofu Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Tanzania, ameitaka Familia ya Mungu nchini Tanzania na kwa namna ya pekee wanasiasa kulinda, kutetea na kudumisha maadili, tamaduni na mapokeo mema dhidi ya utamaduni wa kifo na mmomonyoko wa maadili na utu wema; mambo yanayopata shinikizo katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kutoka katika nchi za kigeni. Mambo haya ni hatari kwa maisha na utume wa ndoa na familia ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Amewataka wanandoa kusimama kidete kulinda kutetea na kushuhudia Injili ya Familia inayofumbatwa katika Injilia ya Uhai.
Askofu Sangu amebainisha hayo hivi karibuni katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi takatifu kwenye Kanisa la Mtakatifu Yohane Parokia ya Bariadi, Jimbo Katoliki Shinyanga alipokuwa akifanya hija ya kitume Jimboni humo. Askofu Sangu ametolea mfano wa ndoa za jinsia moja. Amewaelezea watu wanaolazimisha mawazo ya namna hiyo kuwa ni matajiri ambao lengo lao ni kutafuta starehe na anasa. “Wanatumia fedha zao kuishawishi jamii ya ulimwengu ikubaliane na suala hilo ambalo hata wanyama wasiokuwa na akili hawawezi kulikubali.”
Ameitaka jamii na viongozi wa serikali kuwa makini na mawazo hayo mabaya ambayo yanaingizwa katika nchi za Afrika ikiwemo Tanzania, yakiwa na lengo la kuharibu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ambazo ndiyo chimbuko la mambo yote. Amewaomba Wakristo wote kuhakikisha wanawalea watoto wao kwa kuzingatia misingi ya imani na mafundisho ya Kanisa kwa kuwa malalamiko mengi ya kimaadili yanayotolewa dhidi ya vijana hivi sasa yanatokana na wazazi wengi kutotimiza wajibu huo.
Katika hatua nyingine Askofu Sangu ameendelea kuwahimiza watu wote kupendana na kuthaminiana ili wasiingie katika machafuko na kuuana wenyewe kwa wenyewe kwa sababu tu ya tofauti za itikadi za dini na siasa. Jimbo Katoliki Shinyanga litakuwa na ustawi na maendeleo ya kweli endapo tu kila mmoja atashinda roho ya ubinafsi na kuwa na moyo wa upendo kwa Mungu, Kanisa na jirani. “Pamoja na mchango mkubwa wa kulijenga Jimbo letu la Shinyanga uliofanywa na waasisi walitutangulia wakiwemo maaskofu na waamini, hatuna budi kuendelea kulijenga jimbo ikizingatiwa kuwa, hivi sasa halitegemei misaada kutoka kwa wafadhili,” ameshamasisha Askofu Sangu.
Katika ziara yake hiyo, amewataka waamini wa Parokia ya Bariadi Jimboni Shinyanga kuanza kufanya maandalizi ya kuanzishwa kwa Jimbo Jipya la Bariadi ambalo litatokana na kugawanywa kwa jimbo la Shinyanga, ili kusaidia kusogeza huduma za kichungaji kwa waamini. “Kwa muda mfupi niliotembelea maeneo mbalimbali ya jimbo la Shinyanga, nimejiridhisha kuwa, jimbo hili ni kubwa. Hivyo tuanze mchakato wa kuhakikisha kuwa, Bariadi linakuwa ni Jimbo jipya ambalo litajitegemea siku za mbeleni,” amesema.
Kufuatia tamko hilo, askofu Sangu pia ameitangaza Kituo cha Mtakatifu Luka iliyopo eneo la Sima mjini Bariadi kuwa Parokia Teule, na amependekeza hapo ndipo pajengwe Kanisa Kuu la Jimbo hilo Jipya. Ameahidi kuteua Padri haraka iwezekanavyo ili kutoa huduma katika Kanisa hilo kituoni hapo. Amewaomba waamini wa Parokia ya Bariadi kuanza kufanya maandalizi ikiwemo kujenga Kanisa kuu la Jimbo wakati taratibu nyingine za kuanzishwa kwa jimbo hilo zikiendelea kufanyika.
Wakati huo huo, Askofu Sangu amemteua Padri Kizito Nyanga aliyekuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha CUEA Jijini Nairobi nchini Kenya kuwa msimamizi wa muda wa Parokia ya Bariadi kufuatia aliyekuwa Paroko wa Parokia hiyo Padri Fabian Kushoka kuteuliwa kuwa mlezi katika Seminari Kuu ya Ntungamo - Bukoba.
Pia amemteua Padri Richard Makoye ambaye amepewa Daraja Takatifu la Upadri hivi karibuni katika Parokia ya Shinyanga mjini kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bariadi. Askofu Sangu alikamilisha ziara yake ya siku tatu katika Parokia ya Bariadi na kuelekea kwenye Parokia za Udekano wa Nassa ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kichungaji kwa parokia zote za Jimbo la Shinyanga tangu alipowekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga.
Na Joachim Mahona, Shinyanya.
0 blogger-facebook:
Post a Comment