Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda linasema kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Uganda kuanzia tarehe 27 hadi 29 Novemba 2015 ni baraka na neema ya pekee kwani hakuna nchi ambayo Barani Afrika imepata upendelee wa namna hii kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Ni tukio ambalo linaendeleza maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mashahidi wa Uganda walipotangazwa kuwa watakatifu. Damu ya mashuhuda hawa wa imani imekuwa ni chembe hai ya Ukristo nchini Uganda na ujasiri wa kusonga mbele kwa imani na matumaini katika hija hii ya maisha ya imani
Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Uganda inaongozwa na kauli mbiu “Nanyi mtakuwa mashahidi wangu” Mat. 1.8. Hii ni changamoto anasema Askofu John Baptist Odama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda kwamba, kwa Familia ya Mungu nchini Uganda kuhakikisha kwamba, inajiandaa kikamilifu kwa ajili ya kumpokea na kuadhimisha mafumbo mbali mbali ya Kanisa. Hii ni hija ya kiroho inayolenga kuwaimarisha ndugu zake katika imani.
Maaskofu wanaihamasisha Familia ya Mungu nchini Uganda kufanya maandalizi mazuri ya maisha ya kiroho kadiri ya taratibu zilivyopangwa katika ngazi mbali mbali pamoja na kuhitimisha Ibada ya Misa takatifu kwa kusali kwa ajili ya kuombea nia na hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu nchini Uganda. Hiki ni kipindi muafaka cha kutekeleza matendo ya huruma miongoni mwa maskini, ili kupokea neema na baraka zinazotolewa na Kristo kwa njia ya Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Huu ni utekelezaji pia wa amri ya upendo, toba na wongofu wa ndani pamoja na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani ambayo kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya Mashahidi wa Uganda, leo hii idadi ya Wakatoliki imeongezeka maradufu na kufikia waamini millioni kumi na tatu. Kanisa Katoliki nchini Uganda ni hai na linaendelea kuchangia katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Uganda katika sekta mbali mbali, hususan miongoni mwa maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”.
Waamini wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda wa imani tendaji, kwa kuguswa na pengo kubwa lililoko kati ya maskini na matajiri; kwa kumwilisha imani katika uhalisia wa maisha ili kuachana na mila, desturi na tamaduni zinazosigana na tunu msingi za Kiinjili. Waamini wawe kweli ni waaminifu wa utakatifu wa maisha ya ndoa kwa kuishi kadiri ya mafundisho ya Kanisa. Waamini wawe waaminifu kwa wenzi wao wa ndoa kwa kuachana na vipigo vya wanawake majumbani, udhalilishaji na unyanyasaji wa watoto wadogo; ulevi na umaskini pamoja na kujikinga na janga la Ukimwi, ambalo limekuwa kwei tishio kwa familia nyingi nchini Uganda.
Mashahidi wa Uganda wawe kweli ni mfano wa kuigwa katika maisha na utume wa Familia nchini Uganda kwa kutambua kwamba, Familia ya Mungu Barani Afrika inapaswa kuwajibika barabara. Ni jukumu na wajibu wa Familia ya Mungu nchini Uganda kuenzi na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kudumisha utakatifu na ustawi wa Sakramenti ya ndoa na familia, changamoto ya kukumbatia kweli kanuni maadili.
Mwenyeheri Paulo VI alipotembelea Uganda kunako mwaka 1969 aliwataka Waafrika kuwa ni Wamissionari Barani Afrika, changamoto ya kuambata Kanisa pamoja na kuifahamu imani inayoungamwa, adhimishwa, ishi na kusaliwa! Ni mwaliko kwa Familia ya Mungu nchini Uganda kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kufanya rejea tena kwa Waraka wa kichungaji uliotolewa na Maaskofu Katoliki Uganda kunako mwaka 1993.
Huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu, tayari kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kuwa onesha upendo, furaha, amani. Uvumilivu, utu wema na uaminifu. Lengo ni kusimama kidete kupinga rushwa na mmong’onyoko wa maadili, imani za kichawi na kishirikina; chuki na wivu; uasherati; ukosefu wa haki msingi za kibinadamu, magomvi pamoja na ubinafsi. Maaskofu wanakaza kusema vilema hivi vimeota mizizi katika maisha ya watu wengi nchini Uganda.
Kama sehemu ya maandalizi ya Ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Uganda, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kujisomea Mafundisho Jamii ya Kanisa; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini sanjari na kuwa kweli mashuhuda wa Injili ya haki na utakatifu; umoja na mshikamano wa kitaifa. Baba Mtakatifu anakuja kujenga na kuimarisha madaraja ya wananchi wa Uganda kukutana; anakuja kuendeleza mchakato wa umoja na mshikamano wa kitaifa; haki, amani na upatanisho wa kifamilia; kidini, kitamaduni na kisiasa. Mwaliko ni kumuiga Kristo ambaye alikuja si kwa ajili ya kuhudumia bali kuhudumia na kutoa maisha yake ili yawe ni fidia ya wengi. Wananchi wa Uganda wanahamasishwa kujenga moyo na utamaduni wa kuhudumiana kama ndugu.
Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira “Laudato Si” “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote ni changamoto kwa Familia ya Mungu nchini Uganda kujenga utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii inatokana na ukweli kwamba, binadamu wanachangia kwa kiasi kikubwa katika uharibifu wa mazingira. Ujio wa Baba Mtakatifu nchini Uganda iwe ni fursa ya kujikita katika utunzaji bora wa mazingira. Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda linahitimisha Waraka wake wa kichungaji juu ya ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini humo kuanzia tarehe 27 hadi tarehe 29 Novemba kuwa ni fursa ya kukua na kukomaa; toba na wongofu wa ndani na changamoto ya kuwa kweli ni mashahuda wa imani tendaji
0 blogger-facebook:
Post a Comment