Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Gabriel Mmole wa Jimbo Katoliki Mtwara la kung’atuka kutoka madarakani kadiri ya Sheria za Kanisa Namba 401, Ibara ya 1. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Askofu msaidizi Titus Joseph Mdoe kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Mtwara. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Titus Mdoe alikuwa ni Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania.
Askofu Titus Joseph Mdoe alizaliwa kunako tarehe 19 Machi 1961 huko, Lushoto, Jimbo Katoliki la Tanga. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikuhani, akapadrishwa kunako tarehe 24 Juni 1986 kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Tanga. Kunako tarehe 16 Februari 2013, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akamteua kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na kusimikwa rasmi na Kardinali Polycarp Pengo tarehe Mosi, Mei 2013, ili kuendeleza kazi ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu.
Katika mahubiri ya kumsimika Askofu Mdoe, Kardinali Pengo alikaza kusema kwamba, jambo la msingi ambalo Askofu anapaswa kukumbuka ni kwamba, Uaskofu ni utumishi na wala si madaraka na kwamba, ameteuliwa si kwa masitahili yake binafsi, bali ni kwa ajili ya mpango wa Mungu kwa Kanisa lake. Askofu awe tayari kujisadaka na kwenda mahali popote pale atakapotumwa kwa ajili ya kuwatangazia maskini Injili ya furaha.
0 blogger-facebook:
Post a Comment